Upinzani nchini Misri umeitisha maandamano makubwa mitaani kesho Jumanne, kupinga kura ya maoni juu ya mswada wa katiba ambao kwa kiasi kikubwa uliandikwa na washirika wa kiislamu wa rais Mohammed Mursi. Kura hiyo inatarajiwa tarehe 15 mwezi huu.
Katika tangazo lililosomwa katika mkutano na waandishi wa habari, msemaji wa kundi la upinzani lijulikanalo kama National Salvation Front, Sameh Ashour, amesema hawautambui mswada huo wa katiba kwa sababu hauwakilishi wananchi wa Misri. Amesema wanapinga kura ya maoni juu ya mswada huo, kwa sababu itawagawa zaidi wananchi. Ashour amesema chama chao kinataka maandamano mjini Cairo na katika miji mingine ya nchi, kukataa kile alichokiita uamuzi unaopuuza matakwa yao halali.
Katika tangazo hilo, upinzani vile vile umewalaani wanamgambo wanaoliunga mkono kundi la Udugu wa Kiislamu la rais Mursi, likiwaita magaidi. Wito huo wa maandamano mengine unaashiria kuendelea kwa mzozo wa kisiasa nchini Misri, licha ya hatua iliyochukuliwa na rais Mohammed Mursi Jumamosi kuachana na sheria aliyoiweka kujilimbizia madaraka.