Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk
Shukuru
Kawambwa.
TUMEKUWA
tukisisitiza mara kwa mara kwamba muundo wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu
ya Juu (HELSB), una walakini mkubwa.
Bila
kutafuna maneno, tumekuwa tukisema kwamba bodi hiyo haiwezi kufanya kazi zake
kwa ufanisi kutokana na kasoro za kisera na kimuundo ambazo zimeifanya bodi hiyo
kufanya kazi kama idara ya Serikali.
Kama hiyo haitoshi, wizara husika nayo imekuwa sehemu ya tatizo, kwani nayo pia imeshindwa kuisimamia bodi hiyo ili itekeleze sheria zilizopitishwa na Bunge kuhusu mikopo ya wanafunzi.
Ni jambo la
kufadhaisha kuona viongozi wa wizara husika wakiungana na HELSB kulalamika
badala ya kubuni mbinu za kutatua matatizo yanayowasibu wanafunzi wa elimu ya
juu katika kupata mikopo.
Alisema hadi Septemba mwaka huu, fedha zilizokusanywa ni Sh23.3 bilioni kutoka kwa wanafunzi 48,235 tu na kwamba kiwango hicho ni chini ya asilimia 50 ya fedha zilizotakiwa kurudishwa.
Katika
kuonyesha jinsi wizara yake ilivyokata tamaa kuhusu uwezekano wa mikopo hiyo
kurejeshwa, alisema wanafunzi hao wasiporejesha mikopo hiyo watafuatiliwa na
wakala maalumu aliyeajiriwa na HELSB kwa lengo la kuwafuatilia ambao
hawajarejesha mikopo hiyo.
Kama tulivyosema hapo juu, kauli hiyo inaonyesha bayana kwamba ni ya mtu aliyekata tamaa. Huku akikiri kwamba tatizo hilo limekuwa changamoto kubwa kwa wizara yake, alisema wanafunzi hao waliorejesha mikopo ndiyo wamegundulika na kwamba idadi kubwa zaidi bado haijagundulika na haijulikani wako wapi na wanafanya kazi gani.
Pamoja na kusema HELSB imeajiri wakala maalumu wa kufuatilia ambao hawajarejesha mikopo, Waziri Kawambwa alisema ameiambia bodi hiyo kwamba hatakuwa na uhusiano mzuri na bodi hiyo kabla haijafanya kazi ya kuhakikisha mikopo hiyo inarejeshwa, hivyo kuitaka bodi hiyo kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha fedha hizo zinarejeshwa.
Jambo la
kushangaza ni kuona anapata kigugumizi kuifukuza bodi hiyo na kuteua mpya
itakayokuwa na dhamira na uwezo wa kuhakikisha mikopo hiyo inarejeshwa, tena
katika kipindi kifupi. Tatizo hapa ni utamaduni wa kuleana na kulindana na
hakuna mwenye uchungu wa kuhakikisha fedha hizo ambazo zimetokana na kodi za
wananchi zinarejeshwa.
Tunapata
wakati mgumu kuelewa jinsi watu wanavyoweza kuchukua mikopo halafu wakaingia
mitini, licha ya kusaini mikataba iliyotayarishwa na wanasheria wasomi na kuwapo
sheria ya Bunge inayosimamia mikopo hiyo.
Hatutaki
kuamini kwamba mikataba hiyo ilitayarishwa na kusainiwa kienyeji, kwa maana ya
kutobainisha anuani za makazi na wakopaji kutokuwa na wadhamini ambao mali zao
(collateral) zinakamatwa na kunadiwa pindi wadhaminiwa wanapotoweka
kusikojulikana kama Waziri Kawambwa anavyodai.
Matatizo yote hayo yasingetokea kama Bodi ingekuwa na watu wabunifu na waadilifu. Tunaambiwa baadhi ya wafanyakazi wake wamepelekwa mahakamani kwa madai ya kuchota mamilioni ya fedha za mikopo.
Ushauri
wetu kwa Waziri Kawambwa ni kuisafisha bodi hiyo na kuteua mpya itakayoleta
ufanisi. Vinginevyo fedha hizo za wananchi zitakuwa zimekwenda kwa mganga,
hazitarejeshwa ng’o.


Post a Comment