Rais Jakaya Kikwete amezitaka taasisi za fedha nchini kutoa mikopo kwa bei nafuu kwani riba ya asilimia 18 ni kubwa na inawafanya walalahoi washindwe kunufaika na huduma hiyo.Rais Kikwete alitoa agizo hilo jana alipokuwa akizindua mradi wa nyumba za gharama nafuu zilizojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), katika eneo la Kibada jijini Dar es Salaam
“Wizara, Benki Kuu na taasisi za fedha zikae na kuhakikisha hilo linafanyika, hiyo itaondoa watu kufikiria rushwa katika maeneo yao ya kazi ili kuweza kupata fedha za kufanyia maendeleo yao,” alisema Rais Kikwete alisema na kuongeza;
“Siridhiki na kasi ya benki na sidhani kama zinakopesha watu wa chini na ndiyo maana watu hawajui na hawakopi huko. Mikopo ndiyo itakayowasaidia watu kumiliki nyumba.”
Alisema ni muhimu pia wizara ikaangalia ni jinsi gani ya kupunguza gharama za vifaa vya ujenzi kwa watu wote ikiwa ni pamoja na ununuzi wa viwanja ili watu waweze kujenga.
Rais Kikwete alitoa changamoto kwa NHC akilitaka shirika hilo kufikiria kuanzisha taasisi yake ya fedha ili iweze kuwakopesha wateja wa nyumba zake na pia kulikopesha shirika hilo.
“Anzisheni ili muweze kukopa kwenye taasisi yenu, hiyo itasaidia katika kufanikisha mambo, mtaweza kupunguzaa riba na wengine watajifunza kwenu,”alisema Rais Kikwete.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu alisema kuwa mradi huo una nyumba 290 na zitakuwa zikuzwa chini ya Sh 50 milioni.
Alisema pamoja na hayo shirika linakabiliwa na changamoto mbalimbali kama kununua ardhi kwa gharama kubwa kwenye halmashauri hapa nchini.
“Pia kutengeneza miundombinu ya eneo la miradi yetu nayo ni gharama kubwa wakati ni kitu ambacho kilitakiwa kifanywe na mamlaka zingine,”alisema Mchechu.
Aliiomba Serikali kuondoa kodi kwenye mauzo ya nyumba ambazo hazizidi Sh 100 milioni kwani hiyo itasaidia watu wengi kuweza kununua nyumba kwa gharama ndogo.
Hata hivyo Rais Kikwete alisema hawezi kuruhusu kodi kuondolewa kwenye mauzo hayo bali atakachoweza kusaidia ni kupunguzwa kwa kodi hiyo.
“Mimi kwenye hilo la kufuta sipo ila kwenye kupunguza tunaweza tukafanya hivyo kwa kujadiliana na mamlaka husika kwa kuwa kodi ndiyo inayoiendesha Serikali yetu,”alisema Rais Kikwete.
Azionya halmashauri
Katika hatua nyingine rais Jakaya Kikwete amezionya Halmashauri zote nchini kuacha kufanya ardhi kuwa ni chanzo cha mapato kwa kuuza kwa bei ghali, kwani tabia hiyo itasababisha wananchi washindwe kuinunua.
Pia, amezitaka taasisi za fedha nchini kupunguza riba katika mikopo wanayotoa kwa wananchi ili waweze kumudu kukopa na kufanya maendeleo yao..
Alisema ni muhimu kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kusimamia jinsi gani Halmashauri zinasimamia ardhi ili isiwe ya gharama kubwa.
“Halmashauri zisigeuze ardhi kuwa chanzo cha mapato, hiyo ni mbaya sana na hatutafika pazuri, kwani watu watashindwa kununua ardhi,” alisema Rais Kikwete na kuongeza. Ni muhimu wajue ardhi ni huduma na siyo sehemu ya kujipatia mapato.”


Post a Comment