Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete akimpokea mgeni wake, Rais wa
Madagascar , Mheshimiwa Andry Rajoelina mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam leo, Ijumaa, Desemba 14,
2012 kwa ziara ya siku mbili nchini.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika mazungumzo
na Mgeni wake,Rais wa Madagascar , Mheshimiwa Andry Rajoelina mara baada ya
kuwasili nchini leo.Picha na Fredy Maro, Ikulu.
Rais wa Madagascar,
Mheshimiwa Andry Rajoelina amewasili mjini Dar Es Salaam mchana wa leo, Ijumaa,
Desemba 14 kwa ziara ya kikazi ya siku mbili nchini.
Kwenye Uwanja wa Ndege wa
Julius Nyerere mjini Dar Es Salaam ambako ndege iliyomleta Rais Rajoelina ilitua
saa sita na dakika 45 mchana, amelakiwa na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.
Rais Kikwete na Rais
Rajoelina wamekula chakula cha mchana na wanatarajiwa kuanza mazungumzo rasmi
baadaye leo.
Rais Kikwete ambaye ni
Mwenyekiti wa Tume ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa
Afrika (SADC) amepewa jukumu na viongozi wenzake ndani ya Jumuia hiyo kukutana
na viongozi wa Madagascar kuwalezea maamuzi ya mkutano wa viongozi hao wa SADC
uliofanyika mwishoni mwa wiki mjini Dar Es Salaam.
Rais Kikwete tayari
amekutana na kufanya mazungumzo na Mheshimiwa Marc Ravalomanana, kiongozi wa
zamani wa Madagascar aliyeondolewa madarakani na Rajoelina.
Kwenye mkutano na waandishi
wa habari uliofanyika Ikulu, Dar Es Salaam, mwanzoni mwa wiki hii, Mheshimiwa
Ravalomanana alithibitisha kuwa amekubaliana na maamuzi ya viongozi wa
SADC.
Miongoni mwa mambo mengine,
viongozi hao wa SADC wanataka viongozi hao wawili wa Madagascar washawishiwe na
wakubali kutogombea katika Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika nchini humo
mwakani.


Post a Comment