Mwenyekiti wa shirikisho la vyama vya wachimbaji madini (FEWATA) nchini, Bw.John Wambura Bina (mwenye mashada) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo kwenye picha) wakati akitoa shukurani zake kwa kuchaguliwa hivi karibuni kushika wadhifa huo.Kulia ni makamu mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini mkoa wa Manyara,Bw. Hamisi Rashidi.(Picha na Nathanieli Limu).
Na Nathaniel Limu.
Wachimba madini nchini wamehimizwa kujenga utamaduni wa kutii sheria zilizowekwa pamoja na kulipa kodi/ushuru, ili kujijengea mazingira mazuri ya kupewa misaada mbali mbali ikiwemo Kukopesheka.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini (FEWATA) nchini John Wambura Bina, wakati akitaja vipaumbele vyake siku chache baada ya kuchaguliwa kushika wadhifa huo hivi karibuni.
Amesema utamaduni wa kutii sheria na kulipa kodi kwa wakati, ndiyo njia pekee itakayosaidia mchimbaji madini husika kuaminika popote pale.
Bina ambaye pia ni mjumbe wa chama cha watafiti na wachimbaji madini (SIREMA) mkoa wa Singida, amesema atahakikisha wachimbaji wadogo wanapata elimu ya ujasiriamali, ili uboreshaji wa shughuli zao ziwe za tija zaidi.
Kwa upande wa Serikali, Bina amesema washirikiana kwa karibu na serikali kwa lengo la kuwaendeleza wachimbaji wadogo wa madini watoke walipo wafikie hatua ya kuwa wachimbaji wa kati na kisha wachimbaji wakubwa.
Wakati huo huo, makamu Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini mkoa wa Manyara Hamisi Rashid, amesema wachimbaji nchini kote wanayo matarajio makubwa kwa uongzi ulio chini ya Bina, kwamba utafanya mapinduzi makubwa ya kuwainua wachimbaji.