BAADHI ya
walimu na wazazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe wameiomba Serikali kutenga
bajeti maalumu kwa ajili ya kuboresha elimu ya awali ili madarasa hayo yasiwe
mzigo kwa walimu wakuu.
Uchunguzi uliofanywa na
mwandishi wa habari hizi eneo hilo umebaini licha ya Serikali kusisitiza kila
shule ya msingi kuwa na darasa la awali, baadhi ya maeneo haitoi fungu lolote
kuendesha madarasa hayo.
Akizungumza hivi
karibuni ofisini kwake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kwagunda, David Kituja
iliyopo Kijiji cha Kwagunda Korogwe, alisema darasa la awali shuleni hapo
hutumia bajeti ile ile ya shule ya msingi, jambo ambalo limekuwa mzigo kwa
walimu wakuu hivyo kushauri kuongeza fungu kuboresha darasa
hilo.
“Madarasa ya awali kweli
ni tatizo, maana inasikitisha Serikali inasisitiza yaanzishwe kwa kila shule
lakini hakuna bajeti yoyote iliyotengwa kuyahudumia…mwalimu unalazimika kubana
upande wa bajeti ya msingi uitumie kwenye darasa la awali sasa hii ni changamoto
kweli kweli,” alisema Kituja.
Kwa upande wake, mmoja
wa wazazi, Vedastus Mhilu alisema, changamoto ya kipato kwa wazazi wengi
vijijini bado ni tatizo kubwa kwa uchangiaji wa madarasa hayo jambo ambalo
husababisha elimu hiyo kuendeshwa kwa kubabaisha.
“…Huku wazazi wengi ni
wakulima kwa hiyo ile fedha tunayoipata haitoshelezi kuwapeleka watoto wetu
kusoma madarasa ya awali au kuchangia ada na hata michango ya chakula, si kwamba
hatupendi watoto wetu wapitie elimu hiyo ya awali tatizo ni kipato,” alisema
Mhilu.
Aidha Mwalimu Mkuu wa
Shule ya Msingi Kwashemshi, Jonathan Mzava alisema kwa upande wao wameweza
kuanzisha madarasa ya awali kwa ushirikiano na Serikali lakini kikwazo ni namna
ya kupata walimu wa kudumu kuwafundisha watoto hao muda wote.
“Hapa shuleni ninao
wanafunzi kama 100 hivi wa elimu ya awali, madarasa haya yanaendeshwa kwa msaada
wa Serikali ila mwakani nafikiria kuwashirikisha wazazi ili tuweze kuiboresha
zaidi…nitawaomba wachangie kiasi kidogo ili tuweze kupata walimu ambao muda wote
watakuwa wanawafundisha watoto tofauti na sasa ambapo natumia walimu wa shule ya
msingi,” alisema Mzava.
Akizungumzia kuhusu
elimu ya awali, Kaimu Ofisa Elimu Sekondari, Shaban Shemzighwa alisema hakuna
walimu wanaoajiriwa maalumu kama walimu wa madarasa ya awali hadi sasa, hivyo
shule zenyewe hujitegemea kimgawanyo wa walimu kuendesha elimu hiyo
Post a Comment