Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya watu wa China Bibi Chen Qiiman Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi Seif Ali Iddi akipokea zawadi ya picha za kuchora kutoka kwa Balozi wa Jamuhuri ya Watu wa China Bibi Chen Qiiman.
Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo Zanzibar Bibi Chen Qiiman pamoja na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakifurahia moja ya picha za michoro ya opera iliyosanifiwa na wataalamu wa fani ya sanaa kutoka China.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akipokea moja ya Seti ya TV kati ya mbili alizopatiwa zawadi kutoka Ubalozi Mdogo wa Jamuhuri ya Waztu wa China Zanzibar kwa ajili ya Ofisi yake.
Jamuhuri ya Watu wa China imesisitiza kwamba Zanzibar itaendelea kuwa mshirika wake Mkuu katika kudumisha udugu na ushirikiano wa muda mrefu uliojengeka kupitia Nyanja za maendeleo, Kiuchumi na ustawi wa Jamii.
Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo Zanzibar Bibi Chen Qiiman ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif katika hafla fupi ya kumkabidhi zawadi ya Seti mbili za Tv kwa ajili ya Ofisi yake.
Balozi Chen Qiiman amesema ushirikiano wa sekta ya afya hivi sasa umepiga hatua kubwa ambapo vipindi maalum vimeandaliwa kwa pamoja kati ya wataalamu wa afya wa pande hizo mbili katika kuwafundisha wananchi kuelewa vyema elimu ya afya.
Ameisema Taaluma hiyo imeelekezwa zaidi kwa wananachi wa kawaida hasa wale wa vijijini kuweza kujipatia elimu ya kujikinga na maradhi mbali mbali kupitia vipindi hivyo muhimu.
Akizungumzia sekta ya Ujenzi Balozi Chen Qiiman ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa hatua zake za ushirikiano inayotowa kwa wahandisi wa Kampuni za Jamuhuri ya Watu wa China zinazoendeleza ujenzi wa majengo tofauti visiwani Zanzibar.
Balozi Chen amesema hatua hiyo ya ushirikiano imetowa fursa kwa wajenzi hao kuendeleza harakati zao za ujenzi na kufikia muda muwafaka wa kukamilisha kazi zao kwa mujibu wa mikataba inavyofungwa.
Hata hivyo Balozi Chen amesema zipo hitilafu za kiufundi zilizojitokeza wakati wa ujenzi wa jengo la uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar ambazo tayari zimeshapatiwa ufumbuzi na vifaa kwa ajili ya marekebisho ya hitilafu hizo vitawasili nchini muda wowote kuanzia sasa ili kukamilisha ujenzi huo.
Akitoa shukrani zake mara baada ya kupokea zawadi hizo za Seti za Tv Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, amesema China na Zanzibar zina Historia ndefu ya ushirikiano ambao unafaa kudumishwa kwa maslahi ya wananchi wa Nchi hizo mbili.
Balozi Seif amesema mpango maalum wa Jamuhuri ya Watu wa China wa kuwapatia mafunzo watendaji wa Serikali, Viongozi pamoja na misaada ni uthibitisho kamili wa kukuwa kwa ushirikiano huo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amemuhakikishai Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo Zanzibar Bibi Chen Qiiman kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu kwa ndugu zao wa China wanaotoa huduma Zanzibar katika Nyanja tofauti.
Amemuomba Balozi Mdogo wa China kufikiria kuongeza fursa zaidi za masomo ya ngazi ya juu kwa wanafunzi wa Zanzibar katika ngazi ya udaktari ili kupunguza uhaba wa madaktari uliopo nchini.