MTUHUMIWA anayedaiwa kumuibia rais mstaafu Ally Hassan
Mwinyi sh.milioni 37, Abdallah Nassor Mzombe (40) zikiwa ni kodi ya pango katika
nyumba mbili zinazomilikiwa na rais huyo, ameiambia mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu Dar es Salaam, kuwa anajua siri nyingi za Mwinyi ambazo kamwe hawezi
kuzisema mahakamani hapo.
Mbele ya Hakimu Mkazi, Jenevitus Dudu, katika utetezi
wake, mbali ya kukataa kutenda kosa hilo, Mzombe alidai amefanya kazi nyingi na
kushirikishwa na mzee Mwinyi mambo mengi ya wazi na ya siri ambayo hata watoto
wake wa kuzaa hawayajui na kwamba anashangazwa kuona sasa anashtakiwa kwa makosa
ya kumuibia fedha hizo.
Mzombe ambaye wakati akitoa utetezi wake alikuwa
akiangua kilio na kulitaja jina la Mungu, alidai ameanza kufanya kazi za Mwinyi
tangu mwaka 1996 na kwamba Mwinyi amekuwa
akimuamini.
Alidai kuwa hakukuwa analipwa mshahara maalumu na
Mwinyi kwani alimchukulia kama mwanae.
“Mzee Mwinyi aliniamini sana na hata mambo mengine
ambayo amekuwa akituma nifanye siwezi kuyasema hapa mahakamani, kwani hata
watoto wake hakuwahi kuwashirikisha…
hizo nyumba mbili mnazodai mimi nimemuibia fedha si
kweli, kwani Mzee Mwinyi amekuwa akinipa zaidi ya shilingi milioni 300 bila
kuandikishiana sehemu niende nikamnunulie nyumba, mashamba, nikamjengee majumba
na nimekuwa nikifanya hivyo na kuandika jina
lake.
“Mwendesha Mashtaka naomba nikuulize, unaujua uhusiano
wetu na Mwinyi? usitake niseme mengi hapa..hivi unafahamu kuwa nilishakaa na
Mwinyi tukajifungia na kuongea na kukubaliana kwamba ninavyomfanyia shughuli
zake hizo kwa uaminifu tena bila hata watoto wake hawajui ipo siku ataninunulia
nyumba? lakini hadi leo nyumba hajaninunulia,”
alidai.
“Mheshimiwa hakimu, mimi sina crown, sina fedha na hao
wapangaji waliokuja kutoa ushahidi kuwa walinipa kodi mimi sikumpelekea Mwinyi
ni waongo na sijawahi kugombana nao isipokuwa mpangaji mmoja ambaye tangu mwanzo
nilimuona kama ni mkorofi.
“Kwa kuwa Mwinyi ni kiongozi mkubwa ni wazi mashahidi
hao wanaweza wakawa walishinikizwa kuja kutoa ushahidi wa kunikandamiza, ila
nasema sina madaraka, fedha na mashahidi ambao nilikuwa nategemea waje kunitolea
ushahidi wananipiga chenga kwa sababu wapo karibu na Mzee Mwinyi….kikubwa hapa
naomba mahakama initendee haki,” alidai Mzombe huku akiangua
kilio.
Kuhusu wizi wa fedha za kodi nyumba hizo za Mikocheni
na Msasani, Mzombe alidai kushangazwa na tuhuma hizo, kwani ni rais Mwinyi ndiye
aliyempa fedha za kwenda kumnunulia nyumba hizo na alikuwa akizisimamia wakati
wa kufanyiwa ukarabati.
Bada ya kumaliza utetezi huo, Hakimu Dudu alisema
hukumu ya kesi hiyo ataitoa Februari 12 mwaka
huu.
Oktoba 9 mwaka jana, rais All Hassan Mwinyi alifika
mbele ya Hakimu Dudu na kutoa ushahidi wake, lakini hata hivyo wana usalama
ambao walikuwa wakimlinda waliwazuia waandishi wa habari kuingia mahakamani
kusikiliza ushahidi huo.
Katika kesi hiyo, Mzombe anadaiwa kuwa kati ya Januari
Mosi, mwaka 2011 na Julai mwaka 2012 huko Mikocheni, akiwa Wakala wa rais huyo
alimwibia sh milioni 17 ambazo ni pato la kodi ya nyumba yake iliyopo eneo la
Mikocheni.
Aidha, alidai kuwa kati ya Januari Mosi, mwaka 2011 na
Julai 10, mwaka huu huko Msasani Village, Wilaya ya Kinondoni, mshtakiwa
alimwibia rais huyo sh. milioni 19.8 ambayo ilikuwa ni kodi ya nyumba namba 55
iliyopo kwenye Kitalu C.
CHANZO http://www.freemedia.co.tz
Post a Comment