Picha
Dar
DARAJA la Mnung’una lililopo Kijiji cha Msisi,
linalounganisha barabara kuu ya Singida hadi Mwanza limebomoka kutokana na mvua
kubwa zinazoendelea kunyesha mkoani hapa.
Hali hiyo imesababisha foleni kubwa ya magari
yaliyokwama yanayokadiriwa kufikia zaidi ya 500. Pia mawasiliano kati ya mikoa
mbalimbali ikiwamo ya Kanda ya Ziwa na nchi jirani yamekatika.
Mmoja wa madereva walioathirika na kubomoka kwa daraja
hilo, George Medadi, aliyekuwa akitokea Mwanza kuelekea Dar es Salaam, alisema
daraja hilo limekatika kutokana na kujengwa chini ya kiwango.
Aidha, wenyeji wa kijiji hicho walisema kalavati
zilizotumika kujengea daraja hilo ni zile zilizowekwa wakati wa uongozi wa
Nalaila Kiula alipokuwa Waziri wa Ujenzi.
Mkuu wa Wilaya ya Singida, Queen Mlozi, alisema kwa
kuanzia wameimarisha ulinzi katika eneo hilo pamoja na kufungua kituo kidogo cha
kutolea huduma ya afya na kudhibiti uwezekano wa kutokea kwa magonjwa ya
mlipuko.
“Pia tumefungua barabara ya Singida-Ndago–Misigiri kwa
ajili ya kutumiwa na mabasi ya abiria na yale yenye uzito chini ya tani 10. Vile
vile tunaangalia uwezekano wa kuangalia ni namna gani watu waliokwama wanapata
chakula,” alisema.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Singida, Mhandisi Yustaki
Kangole, ambaye alifika na wahandisi wa Kampuni ya Chico, alisema wamekubaliana
wafukie shimo kwa vifusi vya mawe makubwa ili barabara hiyo ianze
kutumika.
Wakati huohuo, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Edward ole
Lenga, alisema raia mmoja wa China, amefariki dunia baada ya gari lake kusombwa
na maji ya Mto Kaka jirani na Kijiji cha Gumanga.
Alisema Mchina huyo ambaye hajafahamika jina, alisombwa
na maji ya mto juzi, majira ya jioni wakati akikatisha katika mto huo akiwa na
mtoto wake aliyenusurika kifo.
Post a Comment