Kwa vyovyote vile utakuwa umewahi kuusikia au hata kupata uzoefu kuhusu ugonjwa wa kisukari. Eidha kwa kuwa na ndugu, rafiki wa karibu au wewe mwenyewe kuwa mwathirika wa tatizo hili. Tatizo la kisukari linaongezeka siku hadi siku, hususani kutokana na kuongezeka kwa tatizo la unene. Sababu kubwa si ngumu kuifahamu, ni ulaji wa chakula unaozidi mahitaji ya miili yetu. Kwa lugha rahisi tunaweza kusema, kula chakula bila kufanya mazoezi.
Ziko aina kuu mbili za ugonjwa wa kisukari. Ule unaotokea kwa sababu ya upungufu wa homoni ya insulin mwilini( Type 1 diabetes), na ule unaotokana na homoni ya insulin kutokufanya kazi, japo kuwa inatengenezwa kwa kiwango hata zaidi ya kawaida, (Type 2 diabetes). Asilimia 90 ya wagonjwa wa kisukari wana kisukari cha aina ya pili(type 2 diabetes). Hivyo basi maelezo mengi yatakayoandikwa hapa yatahusiana na kisukari cha aina ya pili.
Kisukari aina ya pili(Type 2 diabetes) ni nini haswa?
Ugonjwa huu huathiri uwezo wa mwili kutumia sukari, protini, mafuta na wanga. Miili yetu inahitaji vichocheo mbali mbali ili kutengeneza nguvu na chembe hai na kutufanya tuendelee kuishi. Ugonjwa wakisukari huaribu uwezo wa mwili kufanya kazi wakati wa kawaida na hata wakati wa mazoezi. Katika hali ya kawaida miili yetu hubadilisha sukari na wanga na kuwa glukozi au sukari kwa lugha ya kawaida, ambayo hutumika mwilini kutengeneza nguvu zinazotuwezesha kuishi na kufanya shughuli za kila siku. Glukozi husafirishwa katika damu na kupelekwa katika misuli, sehemu ambako kiasi kikubwa cha glukozi hutumika kutengeneza nguvu na joto. Insulin, homoni itengenezwayo na kongosho, inahitajika kuwezesha glukozi kuchukuliwa na misuli.
Kwa maana hiyo basi, ili glukozi iweze kutumika kutengeneza nguvu na joto, homoni inayoitwa insulini inatakiwa kuwepo. Glukozi ikishaingia kwenye misuli, inatumika kutengeneza nguvu na joto au kutunzwa kwa matumizi ya baadaye Katika aina hii ya kisukari, ukikumbuka hapo awali tuligusia kwamba, homoni ya insulin inatengenezwa lakini kutokana na sababu fulani(ambazo tutakuja kuziongelea siku nyingine) inashindwa kufanya kazi.(Kumbuka ktk kisukari cha aina ya kwanza, uwezo wa kongosho kutengeneza insulin unakuwa mdogo, hivyo kuathiri kiwango cha insulin inayotengenezwa). Kitendo cha insulini kutokufanya kazi licha ya kutengenezwa kwa kiwango cha kawaida na wakati mwingine kiwango cha juu, kinatokana na misuli kuwa sugu kwa insulin.Tatizo la mwili kuwa sugu kwa insulin linajulikana kitaalamu kama insulinresistance. Kinachotokea ni kushindikana kwa sukari kuingia katika misuli hivyo kubaki katika damu. Hii husababisha sukari kuwa nyingi zaidi ya kawaida katika damu.Sukari kuwa nyingi katika damu kwa muda mrefu, kunaweza kusababisha magonjwa ya moyo, kufeli kwa figo , upofu na matatizo ya mishipa ya fahamu.
Tofauti na aina ya kwanza ya kisukari, ambacho husababishwa na matatizo yanayouwa chembehai zinazotengeneza insulin kwenye kongosho, ugonjwa wa kisukari cha aina ya pili unauhusiano mkubwa na mifumo ya maisha hususani lishe na mazoezi. Watu wenye uwezekano mkubwa wa kupata tatizo hili wana historia ya ugonjwa huu katika familia zao, na pia mara nyingi wanakuwa na magonjwa ya shinikizo la damu na moyo. Mara nyingi ugonjwa huu huwapata watu wenye maisha ya kibwanyenye, ambayo huwafanya kula chakula kingi zaidi ya mazoezi. Wengi wao wanakuwa ni wanene na wenye mafuta mengi mwilini. Kinachotumika kuzuia ugonjwa huu wa kisukari aina pili, ndicho kinchotumika kuzuia usilete madhara makubwa kama magonjwa ya moyo na figo. Na si kitu kingine bali mazoezi na lishe bora.
Mazoezi yanaweza saidia Matokeo ya tafiti chungu nzima yameyapa mazoezi kipau mbele katika kuzuia, na kutibu ugonjwa wa kisukari aina pili, kwa sababu mazoezi yanauwezo wa kupunguza usugu wa insulin unaosababisha homoni hii isifanye kazi. Kufuatia mazoezi ya mara kwa mara, chembe hai za mwili zinaweza kutumia insulin kuchukua sukari kutoka kwenye damu, kuitumia na hivyo kuipunguza.
Mazoezi pia yanaweza kupunguza uwezekano wa kupata magonjwa ya moyo kwa kupunguza kiasi cha mafuta mwilini na shinikizo la damu. Kwa kila kilo tano mtu mwenye kisukari anazopoteza, anapunguza usugu wa insulin kwa asilimia ishirini.
Ushauri wa mazoezi
Kama unakisukari aina ya pili, unashauriwa kufanya mazoezi yafuatayo
1. Mazoezi yanayoufanyisha kazi mfumo wa damu na moyo(cardiovascular exercise):
Weka lengo la kufanya mazoezi ya wastani, kama vile kutembea, na mazoezi mengine yasiyotumia nguvu nyingi kama vile kuendesha baiskeli na kuogelea, angalau mara tatu mpaka nne kwa wiki. Kumbuka, kufanya mazoezi ya namna hii kila siku kunaleta matokeo mazuri zaidi.
2. Mazoezi ya kunyanyua au kusukuma vitu vizito(Resistance exercise):
Watu wengi hukosa kufanya mazoezi haya, kwa kudhani kwamba ni kwa ajili ya wabeba vyuma na wapiganaji tu. Mazoezi haya ni muhimu sana, na siku zijazo nitaelezea kwa undani umuhimu wa mazoezi haya. Weka lengo la kufanya mazoezi ya kunyanyua au kusukuma vitu vyenye uzito wa wastani angalau mara mbili kwa wiki. Akikisha unafanyisha kazi misuli yote muhimu ya mwili wako. Fanya walau marudio kumi mpaka kumi na tano kwa kila aina ya msuli.
3. Mazoezi ya kulainisha viungo(flexibility exercises):
Angalau mara mbili au tatu kwa wiki fanya mazoezi ya kunyoosha viungo muhimu vya mwili ili kulainisha viungo na misuli. Fanya kwa angalau dakika kumi na tano mpaka thelathini, mara mbili mpaka nne kwa kipindi. Undani zaidi kuhusu mazoezi haya, utaelezewa katika makala zifuatazo. Makala hii inagusia aina ya mazoezi tunayotakiwa kufanya ili kupunguza uzio na sukari mwilini.
Post a Comment