NA RAMADHANI ALI
/MAELEZO 8.1.2013
Rais mstaafu wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mzee Ali Hassan Mwinyi amesema Zanzibar ni miongoni mwa
nchi chache Duniani zinazoendelea kutoa Elimu bila malipo tokea kuasisiwa
Mapinduzi matukufu ya mwaka 1964.
Akizungumza katika
ufunguzi wa Skuli mpya ya Sekondari ya Mapinduzi, Chaani katika maadhimisho ya
sherehe za kutimiza miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mzee Mwinyi amesema
mafanikio hayo yanatokana na viongozi shupavu wa Mapinduzi na wale waliofuatia
kuongoza Zanzibar.
Amewapongeza viongozi na
wananchi wa Zanzibar kwa jumla kwa kuendeleza malengo ya Mapinduzi ya 1964 ya
kuimarisha maendeleo katika nyanja mbali mbali.
Rais mstaafu amewahimiza
wananchi kuendeleza Umoja kwani bila umoja na mshikamano hakuna maendeleo
yatakayopatikana.
Amewashukuru wahisani
wanaosaidia maendeleo ya Zanzibar hasa katika nyanja ya elimu na afya na
amesema misaada yao itaendelea kuthaminiwa .
Amewataka wazee wa
Chaani kuendelea kuwasimamia watoto wao na kuhakikisha wanaitumia skuli hiyo
katika kubadilisha uwezo wao wa kusoma kuwa bora zaidi.
Akizungumza katika
sherehe hiyo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Ali Juma Shamhuna amesema
baada ya kupata msaada wa skuli mpya 19 za sekondari na Benki ya Dunia na skuli
mbili msaada wa BADEA, Wizara yake inatilia mkazo katika kuondosha tatizo la
walimu wa sayansi linalokabili Skuli nyingi za Zanzibar.
Amesema Nigeria
imewapatia msaada wa walimu 13 wa sayansi na tayari wamefanya mazungumzo na nchi
ya Marekani, Uingereza, Ghana, India, Palestina, Misri na Oman na wote
wameonyesha azma ya kusaidia kupunguza tatizo hilo.
Ameongeza kuwa Chuo
Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) kwa kuliona tatizo la walimu wa sayansi,
kimeanzisha Skuli ya Sekondari ya sayansi na Chuo cha Ufundi Karume kimeimarisha
somo la hesabu na ameeleza matarajio yake kwamba baada ya miaka mitatu tatizo
hilo litapungua.
Waziri Shamhuna ameahidi
Wizara yake itawaajiri wahitimu wote wa digrii ya sayansi na kuwapa mafunzo ya
ziada walimu wa sayansi ambao wameajiriwa ili kukabiliana na changamoto
hiyo.
Skuli ya Sekondari ya
Mapinduzi, Chaani imegharimu shilingi bilioni 1.32 na imejengwa na kampuni ya
Chaina Railway Jian Chang Engineering Co. LTD ya
China.
IMETOLEWA NA HABARI
MAELEZO
Post a Comment