SERIKALI ya Zimbabwe imesema kwamba mpaka sasa kiasi cha fedha ambacho kipo kwenye akaunti ya Serikali ni Dola 217.
Kiasi hicho ambacho ndicho kinachotajwa kulinda akaunti hiyo ya Serikali ni sawa na Sh347 za Tanzania, huku nchi hiyo ikielekea katika uchaguzi mkuu miezi michache ijayo.
Akizungumza jana nchini humo, Waziri wa Fedha wa nchi hiyo Tendai Biti alisema kwamba kiasi hicho cha fedha ndicho kilichobaki katika akaunti hiyo baada ya kuwalipa wafanyakazi wake mishahara wiki iliyopita.
Biti alisema kwamba kwa sasa Serikali ya nchi hiyo inakabiliwa na ukata mkubwa kutokana na kutokuwepo fedha katika akaunti ya Serikali huku vyanzo vingi vya mapato vikiwa bado havina uhakika.
Kwa mujibu wa Biti ambaye pia ni Katibu Mkuu wa chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change, MDC alisema kwamba kutokana na hali hiyo, Rais Robert Mugabe amemwagiza kuanza kuwasiliana na wafadhili kwa ajili ya kupata misaada kutoka nje.
Mataifa mengi wafadhili hasa yale ya Magharibi, yameipa kisogo Zimbabwe kwa kuiwekea vikwazo vya kiuchumi vinavyowalenga zaidi washirika wa Rais Robert Mugabe na Chama cha Zanu-PF.
Biti alisema kwamba nia ya Rais Mugabe kumwagiza kwa wafadhili wa kimataifa ni kutaka wasaidie uchaguzi mkuu ujao na kuwezesha kufanyika kwa kura ya maoni kuhusu Katiba Mpya ya nchi hiyo, masuala ambayo jumuiya ya kimataifa imekuwa ikiyatolea macho.
Chama cha upinzani cha MDC ambacho Biti ni miongoni mwa viongozi wakuu kipo katika Serikali ya mseto, huku kikiungwa mkono na mataifa mengi wafadhili ambayo yamekuwa yakidai kuwa Serikali ya Rais Mugabe imekuwa ikikandamiza demokrasia nchini humo.
“Rais Robert Mugabe na Waziri Mkuu, Morgan Tsvangirai wameandika barua maalumu wakiiagiza wizara yangu na Wizara ya Sheria kutuagiza tutafute namna ya kupata ufadhili wa fedha kwa ajili ya uchaguzi na kura ya maoni kwa ajili ya Katiba mpya,” alisema Biti.
Alisema nchi hiyo kwa sasa inahitaji Dola85 milioni kwa ajili ya kura ya maoni Machi mwaka huu, pia inahitaji Dola107 milioni kwa ajili ya kuandaa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Juni mwaka huu.
“Tunataka kuhakikisha kwamba fedha tulizozibajeti kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2013 zinapatikana. Pia tumeiomba Tume ya Uchaguzi kuhakikisha kwamba bajeti yake ni sahihi,” alisema.
Chaam cha Zanu-PF chini ya Rais Robert Mugabe, awali kilikataa suala la kura ya maoni kuhusu Katiba mpya kufadhiliwa na Umoja wa Mataifa (UN) kikidai kwamba mataifa ya magharibi yattumia fursa hiyo kuingilia zoezi hilo.
Waziri wa Sheria na katiba, Patrick Chinamasa alisema kwamba watahitaji kuhakikisha hata fedha hizo za wafadhili iwapo zitapatikana zinapitia kwenye Hazina ya nchi hiyo, suala ambalo mataifa mengi wafadhili yalikataa kulifanya awali. MWANANCHI
Post a Comment