Mfuko wa Maendeleo ya
Jamii (TASAF) umeelezwa kama mfano halisi unaoweza kuigwa na jumuiya ya
kimataifa hususani katika eneo la uwezeshaji wa kipato kwa wananchi
maskini,dhana ya ushirikishwaji, upunguzaji wa umaskini , upatikanaji wa ajira
na ulinzi wa Jamii.
“ tunaweza kujifunza
mengi kutoka TASAF ni mfuko ambao unafanya kazi kubwa na nzuri, nimekwenda
Tanzania nimejionea mwenye. Wakati mwingine ili kufahamu lipi linawezekana, na
lipi haliwezekani, ni jambo jema sana kama ukienda na kushuhudia mwenyewe badala
ya kusoma au kusikia kutoka kwa watu wengine”
Hiyo ilikuwa ni kauli
ya Bw. Mawutor Ablo, Mkurugenzi wa Ulinzi wa Jamii, Wizara ya Ajira na Ustawi
wa jamii nchini Ghana. Bw. Ablo alikuwa mmoja wa wana-jopo watano waliokuwa
wakichangia majadiliano ya mada iliyohusu “ Mwelekeo wa Jamii katika Ajenda ya
Kimataifa ya Maendeleo baada ya mwaka 2015.
Majadiliano hayo ni
sehemu ya mada kadhaa zinazohusu Mkutano wa 51 wa Kimisheni ya Maendeleo ya
Jamii, mkutano huu wa wiki moja ambao maudhui yake ni “ kukuza uwezeshaji wa
watu katika kufanikisha uondoaji wa umaskini, ushirikiano wa kijamii, ajira
kamili na zenye tija”, unafanyika hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa
ukiwashirikisha mawaziri, wanazuoni, watafiti wa masuala ya kijamii na taasisi
zisizo za kiserikali.
Bw. Mawutor Ablo
amekwenda mbali zaidi kwa kusema tunapojadiliana kuhusu kile tunachotakiwa
kufanya baada ya 2015, miradi kama ya TASAF inatakiwa kuchukuliwa kama sehemu ya
mafaniko na mfano wa kuigwa. Wala hatuna sababu ya kwenda mbali, mifano hai na
yenye mafanikio ipo”. akasisitiza.
Kauli hiyo ya Bwa. Ablo
iliungwa mkono na mwana-jopo mwingine, Dkt. Timo Voipio ambaye ni Mshauri
Mwandamizi kuhusu Sera ya Jamii na Kazi za Heshima katika Wizara ya Mambo ya
Nje ya Norway.
Yeye alieleza kwamba
licha ya kwamba tafiti zake nyingi kuhusu maendeleo ya jamii amezifanyia Afrika,
lakini pia ameishi Tanzania kwa miaka kadhaa na amejionea mwenyewe kazi nzuri
inayofanywa na TASAF
“ inawezekana kabisa
kuwa na sera za ulinzi wa jamii, uwezeshaji wao, kuwapunguzia makali ya
umaskini na kubwa zaidi ushirikishwaji katika maamuzi ya mambo yanayowahusu”.
Nimeyaona haya kupitia TASAF, inawezekana kukawa na ugumu katika kubadili mfumo
wa maisha hususani kwa mwananchi maskini ambaye amezoea kulima muhogo
ukamwambia alime mahindiaina” akasema Dkt. Voipio.
Lakini hili inawezekana
kwa kupitia miradi kama ya TASAF ambayo inasisitiza sana ushirishwaji wa
wananchi wenyewe” kwa mujibu wa Dkt. Timo Voipio
Akizungumzia kuhusu
viashiria vya maendeleo ya binadamu, bila ya kuingia kwa udani, Dkt. Voipio
anasema Tanzania na Kenya kama nchi jirani zina ushindani Fulani linapokuja
suala la viashiria zima la viashiria hivyo kila nchi ikijitahidi kuipiku
nyingine. Ushidani ambazo anasema anaamini unafanyika katika nchi nyingi
majirani.
Naye mshiriki mwingine
wa majadiliano hayo, Bwa, Stephen Pursey, ambaye ni Mkurugenzi wa Muunganiko wa
Sera na mshauri wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la kazi duniani ( ILO) yeye
alibainisha kwamba suala la upatikanaji wa ajira ni jambo ambalo limekuwa
likizungumzwa na kujadiliwa na kila mtu achia mbali serikali.
Hata hivyo anasema
ingawa ukosefu wa ajira ni tatizo linaloendelea duniani kote. Bado anaamini
kuwa ajira zinaweza kutengenezwa kupitia ubunifu wa sera na
kuwajibika.
Akasema bado anakumbuka
kauli ya Bado Rais Mstaafu wa Tanzania Benjamin Mkapa ambaye katika mikutano
ya Kamisheni
kuhusu Athari za
Utadawazi katika Jamii,alivyokuwa akielezea namna alivyokuwa akiwabana mawaziri
wake wanapowasilisha maandiko yao katika Baraza la Mawaziri
“ Mkapa alikuwa
akitueleza kwamba kila waziri aliyekuwa anawasilisha mpango wake katika Baraza
la Mawaziri alikuwa akimuuliza ni ajira ngapi zitazalishwa kutoka na mpango au
mradi unaowasilishwa”.
Ni wazi kwamba
ufuatiliaji wa aina hii uliwafanya mawaziri husika kuhakikisha kwamba suala la
ajira lilikuwa linapewa uzito wa peke yake, na hili ni jambo ambalo linaweza
kuwa mfano wa kuigwa kama kweli tunataka kupunguza tatizo la ajira hususani
kwa vijana” akasisitiza Bw. Stephen Pursey
Akasema ajira au
uwezeshaji wa kipato si lazima ziwe kazi za maofisini tu. Hata kwa kuwapatia
wanakijiji tenda ya kutengeneza madawati kwaajili ya shule yao, au ujenzi wa
barabra ya eneo lao, tayari unakuwa umewapatia ajira na kipato hataka kama
ajira hiyo ni ya muda lakini tayari umewawezesha.
Kama hilo halitoshi,
Mtaalamu huyo kutoka ILO alikwenda mbali zaidi kwa kusisitiza haja na umuhimu
wa kuwa na vipaumbele vinavyotekelezeka.
Anasema haiwezekani
kuwa na vipaumbele vingi, tafsri ya kuwa na vipaumbele vingi iwe katika eneo
lolote lile, maana yake ni moja tu huna kipaumbele.
Akaongeza kwamba watu
wanajua nini wanataka hata kama watu hao ni maskini, wanajua nini wanataka
wakati gani, mahali gani na kwa mazingira gani, kwa hiyo tunapotafakari nini
kifanyike baada ya 2015 lazima pia tuheshimu matakwa ya watu, wao wanajua nini
wanataka badala ya kuwapandikizia au kuwaamulia.
Muhimili wa Maendeleo ya
Jamii, ni kati ya mihimili mitatu inayounda maendeleo endelevu na ambayo
Jumuiya ya Kimataifa imekuwa ikiyafanyia kazi katika nyanja mbalimbali
hususani kupitia utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia na mkazo
mkubwa ukiwa katika kupunguza au kuondoa umaskini, kupungua pengo kati ya
walio nacho na wasio nacho, utafutaji wa vyanzo vya ajira hususani kwa vijana,
ulinzi wa jamii, elimu, hifadhi ya mazingira na ukuaji wa
uchumi.
Kupitia mkutano huu wa
Kamisheni ya Maendeleo ya Jamii washiriki wanajadiliana na kukusanya mawazo
ambayo yatachangia katika maadalizi ya sera ya Jamii na kuchangia mwelekeo
vipaumbele vya nini kifanyike baada ya mwaka 2015, mwaka ambao utekelezaji wa
Malengo Nane ya Maendeleo ya Millenia utafikia
ukingoni
Post a Comment