Utangulizi
Kumekuwepo na taarifa
kupitia baadhi ya vyombo vya habari kwamba kuna upungufu mkubwa wa dawa mseto za
kutibu malaria aina ya ALU katika vituo vya kutolea huduma za afya hapa
nchini.Taarifa hizo zilimnukuu Mkurugenzi wa shirika lisilo la serikali la
SIKIKA, katika mkutano na wahariri wa vyombo vya habari uliofanyika mjini Dar es
Salaam hivi karibuni.
Ufafanuzi
Taarifa alizotoa Mkurugenzi
wa SIKIKA, chanzo chake kimetokana na kunukuu taarifa zinazopatikana kutoka
katika mfumo wa kielektroniki wa wizara ambao unafuatilia takwimu za dawa za
malaria katika vituo vya huduma ujulikanao kama ‘SMS for
Life’.
Mfumo huu unatoa taarifa za
upatikanaji wa dawa za kutibu malaria aina mbili tu ambazo ni Alu na Quinine, na
sio dawa nyingine za kutibu Malaria.
Hivyo basi, dawa zingine
zote pamoja na zile za msaada, ambazo zinapokelewa na kusambazwa katika
hospitali zote nchini hazitolewi taarifa kwa kutumia mfumo huu wa “SMS for
Life”. Hivyo kusababisha wakati mwingine kuonekana hakuna dawa wakati dawa hizo
zipo vituoni.
Hali
halisi
Dawa za Alu zilizopokelewa
mwezi Januari 2013;-
- Vidonge vya watoto dozi 2,400,000 ambazo zitatosheleza kwa miezi 5
- Vidonge vya watu wazima dozi 5,688,720 zinatosheleza matumizi ya miezi 14
Shehena nyingine za dawa
za Alu zinatarajiwa kufika nchini mwezi Machi, 2013.
Aidha, kufikia tarehe 31
Disemba 2012 kulikuwa na dawa za Alu za watoto dozi 1,315,967 ambazo zilitosha
matumizi ya miezi 2. Vile vile, kulikuwa na dozi za Alu 2,283,610 za watu
wazima ambazo zinatosha matumizi ya miezi 2 na nusu.
Hitimisho
Wizara inapenda
kuwahakikishia wananchi kwamba kwa sasa kuna dawa za kutibu malaria vituoni za
kutosha. Vile vile, Bohari kuu ya Dawa (MSD) inaendelea na usambazaji wa dawa
hizi katika vituo vyote nchini. Aidha, taratibu za kuagiza na kuleta shehena
zaidi ya dawa za malaria kutoka nje ya nchi zinaendelea ili kuhakikisha kuwa
dawa za kutibu malaria zinapatikana kwa muda wote.
Regina L.
Kikuli
KAIMU KATIBU
MKUU
01/02/2013
Post a Comment