Waziri wa Maliasili na
Utalii Balozi Khamis Kagasheki(Pichani) na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani wa
Marekani Bwana David Hayes kwa pamoja watazindua Kituo cha Wageni cha Jumuiya ya
Hifadhi ya Wanyamapori (Wildlife Management Area - WMA) cha Burunge
Mkoani Manyara na kukikabidhi kwa wananchi.
Uzinduzi huo ambao
utafanyika tarehe 5 Februari 2013 ni sehemu ya maadhimisho ya jumuiya za WMA
ambazo zilianzishwa nchini mwaka 1998 kwa mujibu wa Sheria ya
Wanyamapori.
Pia, ni kuonyesha
mafanikio ya Programu ya kuendeleza WMA ambayo inafadhiliwa na Serikali ya
Marekani. Vilevile ni ishara kuwa Serikali ya Marekeni itaendelea kuunga mkono
shughuli za uhifadhi nchini Tanzania, hususan mapambano dhidi ya
ujangili.
Kituo cha Wageni cha
Burunge ni sehemu tu ya misaada inayotolewa na Serikali ya Marekani katika
Programu ya Kuendeleza WMA nchini kote. Kwa WMA ya Burunge misaada mingine ni
ujenzi wa barabara za kufanikisha uhifadhi, kujenga kituo cha askari wa
Wanyamapori na kujenga lango kuu la kuingilia kwenye eneo la WMA
hiyo.
Jumuiya za Hifadhi za
Wanyamapori ni maeneo ya wanyamapori yanayohifadhiwa na kulindwa na Wananchi kwa
manufaa yao na taifa. Tangu zianzishwe mwaka 1998 kuna jumla ya WMA 17 nchini
ambazo zimesajiliwa rasmi na wahusika kuruhusiwa kufanya matumizi endelevu
katika maeneo hayo. Aidha, kuna maeneo 21 ambayo yako katika hatua mbalimbali za
kuanzishwa WMA.
[MWISHO]
George
Matiko
MSEMAJI
WIZARA YA MALIASILI NA
UTALII
4 Februari
2013
Post a Comment