SALAAM,
JANA na leo,
zimetolewa habari tofauti kuhusiana na kalbu ya Simba ambazo uongozi umeona ni
vema uzitolee ufafanuzi kwa lengo la kuweka rekodi sawa. Ufuatao ndiyo ufafanuzi
wa taarifa hizo.
1. SIMBA KUZUIWA
HOTELINI
SAA mbili kabla
ya mechi ya jana baina ya Simba na Coastal Union ya Tanga, mmiliki wa Saphire
Court Hotel alitoa taarifa kwa uongozi wa Simba kwamba ataizuia timu isiondoke
hotelini kwa vile anaidai Sh milioni 25 na anataka alipwe zote
jana.
Ikumbukwe kwamba
Simba imekuwa ikikaa hotelini hapo kwa muda mrefu sasa wakati inapoweka kambi.
Pia, wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba walifanya mkutano na wachezaji wote
wa Simba katika hoteli hiyo usiku wa kuamkia jana.
Wamiliki wa
hoteli hiyo hawakutoa taarifa yoyote kwa uongozi wakati huo juu ya dhamira yao
hiyo.Wamiliki hao hawakutoa taarifa asubuhi ya mechi na walisubiri mpaka wakati
timu inataka kuondoka ndiyo wakachukua hatua hiyo.
Kwa uongozi wa
Simba, hatua hiyo ilikuwa ya ghafla mno. Ifahamike kwamba kabla ya hatua hiyo,
uongozi wa Simba ulikuwa umemlipa mmiliki huyo kiasi cha zaidi ya Sh milioni 30
katika kipindi cha miezi 10 iliyopita.
Mara baada ya
mechi dhidi ya Libolo ya Angola, Saphire walilipwa Sh milioni 15 na Simba. Hii
maana yake ni kwamba klabu yetu ina utaratibu wa kulipa madeni yake na si watu
wasiolipa kama hatua hiyo ya wamiliki wa Saphire inavyotaka
kueleza.
Uongozi wa Simba
tayari ulitoa ahadi ya kumaliza deni lote inalodaiwa baada ya kulipwa fedha zake
inazodai zinazotakiwa kulipwa wakati wowote mwezi huu au ujao. Simba inadai
zaidi ya Sh milioni 500 kwa wadai wake wawili (Etoile du Sahel ya Tunisia na
Push Mobile) na inataraji kulipwa fedha hizo.
Itakapolipwa
fedha zake hizo, Simba itakuwa na uwezo wa kulipa madeni yake yote inayodaiwa na
watu binafsi na makampuni bado ikabaki na fedha za kufanya mambo mengine ya
kimaendeleo.
Wakati ikisubiri
ilipwe fedha zake inazodai, Simba itaendelea kulipa madeni yake taratibu kwa
kadri itakavyoweza. Ifahamike kwamba kwa sasa chanzo kikuu cha mapato ya klabu
ni fedha za mapato ya milangoni na za udhamini wa bia ya KILIMANJARO ambazo
hazikidhi mahitaji yote ya timu.
Kwa kuzingatia
nakisi hii ya mapato na matumizi, Simba SC imeanza mchakato wa kutafuta
wafadhili na wadhamini kokote walipo duniani ili kuongeza mapato yake. Tayari
mawasiliano yameanza na wenzetu wa Sunderland ya England kupitia mradi wao wa
Invest in Africa ili Simba nayo ifaidike.
Simba SC inaomba
pia umma ufahamishwe kwamba klabu ya soka kudaiwa si dhambi. Iwapo klabu kubwa
na tajiri duniani kama vile Manchenster United, Real Madrid na Liverpool zina
madeni, inakuaje madeni ya Wekundu wa Msimbazi (tena ambayo klabu ingeweza
kuyalipa yote iwapo wadeni wake nayo wangewalipa kwa wakati) yaonekane kama kitu
kigeni?
Uongozi unaahidi
kwamba utalipa madeni yake yote kwa kadri utakavyojaaliwa. Kwenye lugha ya
kibenki, credit worthiness ya mteja inamaanisha mteja ambaye anakopa na kulipa.
Simba inapenda kusisitiza kwamba ni taasisi ya kuaminika na yenye heshima kubwa
na bado inavutia watu na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi.
Hata hivyo,
uongozi wa Simba unafikiria kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wamiliki wa
Saphire Court Hotel kwa kitendo chake cha kuwazuia wachezaji na viongozi wa
Simba hotelini kabla ya mechi ya jana.
Simba inachukulia
kitendo kile kama hujuma na kisheria kinaangukia katika kundi la Forced
Imprisonment, kwa mmiliki kuwazuia watu kinguvu. WAMILIKI hawakutoa notisi kwa
uongozi au taarifa yoyote ya mdomo au maandishi kabla ya kuchukua hatua
hiyo.
Lengo lilikuwa ni
kuchafua heshima na hadhi ya Simba kwa hoteli ambayo imetoka kulipwa Sh. milioni
15 wiki mbili tu zilizopita. Uongozi wa Simba SC unaapa kuilinda na kuitetea
hadhi ya klabu yetu kwa nguvu zetu zote, akili zetu zote na maarifa yetu
yote.
2. WACHEZAJI,
BENCHI LA UFUNDI KUFUKUZWA
KUNA taarifa
zimeenezwa pia kwamba kuna wachezaji wa Simba wamesimamishwa au kufukuzwa
kuchezea Simba. Habari hizi nazo hazina ukweli wowote
Ukweli ni kwamba,
uongozi wa Simba umetoa ruksa kwa benchi la ufundi kupanga timu ambayo litaona
inafaa kwa mechi husika. Uongozi hautaingilia, kwa namna,njia au aina yoyote ile
utendaji wa benchi la ufundi.
Hakuna mchezaji
yeyote aliyesimamishwa hadi sasa. Pia uongozi unakanusha taarifa kuwa Daktari
Mkuu wa Klabu, Cosmas Alex Kapinga, kuwa naye ameachia ngazi. Habari hizi hazina
ukweli kwani daktari huyo ana ruhusa ya kikazi ya wiki mbili
inayojulikana.
HITIMISHO
KATIKA namna ya
kipekee kabisa, uongozi wa Simba unapenda kutoa shukrani za dhati kabisa kwa
washabiki wake waliojitokeza Uwanja wa Taifa na kuisapoti timu kwa asilimia 100.
Uongozi unathamini sana mchango wa wanachama wake na unaahidi kufanya kila
unachoweza kuwarejeshea tena furaha mioyoni mwao.
Uongozi pia
unatumia nafasi hii kuwapongeza wachezaji na benchi la ufundi ambao walicheza
mechi ya jana katika mazingira magumu. Walicheza bila ya kufanya warm up na
wakitoka kuwa wamezuiwa hotelini jambo ambalo lingeweza kuwaondoa
mchezoni.
Imetolewa
na
Ezekiel
Kamwaga
Ofisa
Habari
SIMBA
SC
on Monday, March 11, 2013
Post a Comment