Ukosefu wa walimu, upungufu
wa vitabu na mazingira duni ya kujifunzia, ni baadhi ya sababu zilizotolewa kwa
wingi na wadau wa elimu waliohojiwa na Tume ya Kuchunguza Matokeo ya Kidato cha
Nne mwaka 2012 iliyoundwa na Waziri Mkuu.
Hayo yalielezwa
jana na Mwenyekiti wa tume hiyo, Profesa Sifuni Mchome alipokuwa akizungumza na
waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
“Watu wengi
wanasema sababu za matokeo kuwa mabaya ni shida ya walimu, vitabu vichache na
vingine vimepitwa na wakati, wanazungumzia pia usimamiaji wa shule na ukaguzi,”
alisema Profesa Mchome.
Profesa Mchome
alisema kuwa, maelezo hayo ni kutoka kwa wadau mbalimbali waliotembelea kwenye
tume hiyo, kutuma baruapepe, maandiko ama kutoa maoni kupitia kwenye tovuti ya
tume hiyo.
“Pia wapo
waliozungumza kwenye shule 26 za Mkoa wa Dar es Salaam ambazo wajumbe
walizitembelea kuzungumza na walimu, wajumbe wa bodi za shule na wanafunzi,”
alisema Profesa Mchome.
Alibainisha
kuwa, katika kila shule waliyotembelea walizungumza na watu wasiopungua 40,
ambao kwa ujumla wake alisema walitoa maoni mazuri.
Profesa
Mchome alifafanua kuwa, kwa sasa wajumbe wa tume hiyo wapo mikoani wakizungunza
na wadau mbalimbali ili kuweza kupata sababu ya matokeo
mabovu.
Alisema kuwa
wananchi wajitokeze kwa wingi ili kuweza kutoa maoni juu ya sababu
zinazokwamisha elimu nchini.
Profesa
Mchome alisema kuwa, mpaka sasa maelfu ya watu wametoa maoni yao kwa njia
mbalimbali ikiwamo kufika moja kwa moja katika ofisi za tume, kupitia tovuti ya
tume, baruapepe, kuandika maandiko mbalimbali pamoja na kufika kutuma ujumbe
mfupi wa simu.
Alisema
tayari tume yake imezungumza na makundi 12 ya wadau mbalimbali wa elimu yakiwamo
ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Wamiliki wa Shule Binafsi (TAMONGSCO),
Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na Baraza la Mitihani la Taifa
(Necta)
Hata hivyo
alisisitiza kwamba mahojiano ya Necta na Tet ni ya awali. Kwa sasa wajumbe wako
katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Tanga, Manyara, Arusha, Morogoro, Pwani, Simiyu,
Shinyanga, Mbeya na kati ya Machi 24 na 26 watakuwa katika Mkoa wa Dodoma,
Unguja na Pemba
Post a Comment