Mkuu wa wilaya ya Mafia, Sauda Mtondoo, akizungumzaz katika kikao cha wadau wa elimu wilayani humo, kushoto kwake ni Mbunge wa Jimbo hilo Abdulkarim Shah, (BUJI) na kulia kwa DC ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo Mohammed Kimbau.
Wanafunzi wa shule ya Sekondari Kilindoni, mjini Mafia, wakifuatilia majadiliano katika kikao cha wadau wa elimu wilayani humo, kikao kilichofanyika katika ukumbi wa bwalo la magereza.

Na Mwandishi Wetu, Mafia
WAKATI Tume iliyoundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuchunguza kilichosababisha wanafunzi wengi wa kidato cha Nne kufeli katika mitihani ya mwaka 2012, ikiendelea na kazi yake, Wadau wa elimu wilaya Mafia wamejitokeza na kuweka mikakati ili kunusuru sekta hiyo.
Wakizungumza katika kikao kilichofanyika katika bwaro la Magereza, mjini Mafia jana, wadau hao walisema kilichosababisha hali hiyo ni kukosekana kwa ushirikiano baina ya walimu, wazazi na walezi.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo Mohammed Hamis Kimbau, alisema hali mbaya ya elimu imekuwa changamoto sio kwa wazazi na wanafunzi, bali ni kwa makundi yote ndani ya jamii kushirikiana ili kuona haja ya kuifanya wilaya hiyo kuwa na matokeo yanayoridhisha.
Hata hivyo, Kimbau alisema hali hiyo inaweza kuboreshwa ikiwa serikali inaongeza kasi ya uthamini wa wadau wanaohangaika kila siku na wanafunzi hao, kwa maana ya walimu na kamati za shule, ambazo wakati mwingi hujikuta zikifanya kazi bila kuwa na miongozo.
Mkuu wa wilaya ya Mafia, Sauda Mtondoo, alisema hali mbaya ya elimu wilaya humo imeendelea kuwa na changamoto kuanzia mwaka 2011, ambapo hali hiyo iliporomoka kwa kiasi cha asilimia 35.2, lakini imeendelea kuboreshwa.
Pia Mtondoo alisema kwamba mwaka 2012, hali hiyo ilifikia asilimia 13, ikiwa ni moja ya jitihada za kujikomboa kuwa katika nafasi ya saba kimkoa, ambayo binafsi amekuwa ikimsikitisha na kutaka hatua za makusudi zinachukuliwa ili kuikwamua wilaya hiyo kielimu.
Alisema kwamba mwaka 2012, jumla ya wanafunzi 1087 walimaliza elimu ya msingi, ikiwa ni wavulana 503 na wasichana 584, lakini ni asilimia 53.4 tu sawa na wanafunzi 580, waliofanikiwa kufauli na kuendelea na sekomndari.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa lengo kuu la mkutano huu ni kufanya majadiliano juu ya Maendeleo ya elimu katika wilaya hiyo ya Mafia, na hasa baada ya matokeo ya mitihani ya wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari kwa mwaka 2012 kuwa sio nzuri.
Alisema Mwaka jana 2012 jumla ya wanafunzi 442 waliofanya mtihani wa kuhitimu kidaato cha nne katika wilaya ya Mafia yaliyotangazwa February 2013 hakuna mwanafunzi yeyote aliyepata daraja la kwanza wala la pili, wanafunzi wawili tu walipata daraja la III, wanafunzi 91 walipata daraja la IV na wanafunzi 349 sawa na asilimia 78% walipata sifuri.
“Takwimu zilizopo zinaonesha kwamba ufaulu wa mwaka 2012 umeshuka kwa asilimia 13 ukilinganisha na wa mwaka 2011, ambapo ufaulu wake ulikuwa na kuongezeka kwa asilimia 35, hivyo nimeona haja ya kukutana na kutafakari hali hiyo,” alisema Mkuu huyo wa wilaya.
Alisema mbali na wilaya hiyo kushika nafasi ya 7 Kimkoa vile vile asilimia ya ufaulu imeshuka kwa asilimia 14.6 ukilinganisha na ufaulu wa mwaka 2011 (68%), hali ambayo jamii inapaswa kukaa chini na kujadiliana ili kuweka maboresho.
“Penye mchakato wa Maendeleo hapakosi changamoto, halmashauri hii ya Mafia kama zilivyo Halmashauri nyingine hapa nchini inazo changamoto nyingi katika utoaji wa elimu bora ikiwemo uhaba, upungufu na uchache wa Miundombinu, ufinyu wa bajeti, upungufu wa rasilimali watu, ukosefu wa chakula kwa wanafunzi, utoro na mimba za utotoni kwa watoto wa kike, ushiriki mdogo wa jamii katika kuchangia Maendeleo ya elimu shuleni na uwezo mdogo wa Kamati za shule katika kutekeleza na kusimamia majukumu yao kutokana na kukosa mafunzo,” alisema Mkuu huyo wa wilaya.
Aliongeza kusema kuwa halmashauri ya wilaya ya Mafia katika kukabiliana na hali hiyo na kuondoa tatizo la ufaulu mdogo wa wanafunzi wa kidato cha IV pamoja na darasa la VII wilaya imeweka mikakati mbalimbali ikiwemo, kuongeza idadi ya walimu wa shule za msingi kutoka walimu 196 hadi kufikia walimu 299 sawa na 52.5%.
Pia alisema kuboresha maslahi ya walimu kwa kuwapatia sitahili zao kwa wakati ikiwa ni pamoja na kuwapatia nyumba na nyenzo nyingine muhimu katika mchakato wa utoaji wa elimu na kufanya ziara za mara kwa mara za ufuatiliaji wa taaluma shuleni, kuwachukulia hatua za kisheria wazazi na watu wengine wanaosababisha utoro wa wanafunzi ikiwemo mimba za utotoni kwa watoto wa kike na kuendelea kuzijengea uwezo Bodi na Kamati za shule, ili ziweze kutekeleza wajibu wake.
Mkuu wa wilaya alitoa shukurani kwa Asasi na Mashirika yanayojishughulisha na masuala kielimu wilayani humo kwa kusaidia kuboresha hali ya mazingira ya shule kwa maeneo ya vijijini.
“Mashirika kama vile TACAIDS, CHAMAMA, SEA SCAP, ACTION AID, KWA PAMOJA TUWALEE, TANPESCA, ALPHACRUST, PAN AFRICA, ASASI ZA KIDINI, KARIBUNI ONLUS, yamesaidia kwa michango mikubwa ya hali na mali katika kuleta ufanisi wa elimu,” alisema Mkuu huyo wa wilaya.
Alisema kutokana na matokeo hayo mabaya ipo haja kwa wadau kutafakari kwa makini sualahilo ili kuweza kujenga hoja zenye mantiki zitakazotuwezesha kuinua ubora wa elimu katika wilaya hiyo kwa masilahi ya maendeleo ya vijana wa wilaya hiyo.
Mbunge wa Mafia, Abdulkarim Shah, alisema katika kikao hicho kuwa hali ya Elimu katika wilaya hiyo ni mbaya na imesababisha usumbufu kwa jamii, lakini zipo jitihada kadhaa zilizofanywa na serikali kuu katika kuhakikisha hali inaboreshwa.
Alisema kwamba ili sekta hiyo iweze kuleta mafanikio kwa jamii, wadau wanapaswa kutambua kuwa elimu ndio silaha inayoweza kuikomboa wilaya hiyo ambayo ni kisiwa.
Afisa Elimu ya Msingi, Ayubu Bangula, alisema katika kikao hicho kuwa ni kweli hali ya elimu wilayani humo imeendelea kushuka kwa kasi ambapo kwa zaidi ya miaka ya hivi karibuni ambapo imefikia asilimia 68.
Afisa Elimu ya Sekondari wilayani Mafia, Selevester Mwenekitete, alisema changamoto za elimu ya sekondari zinatokana na idadi ndogo ya wanafunzi wanaotakiwa kujiunga na sekoindari kushindwa kufanya hivyo.
Alisema wakati jamii ikitafakari matokeo ya mwaka 2012, lakini hali hiyo inaweza kujirudia kutokana na mwamko mdogo wa mahudhurio kwa wanafunzi waliochanguliwa kujiunga na sekondari mwaka 2013.
Mwanekitete alisema kwamba asilimia 40 ya wanafunzi wote waliochaguliwa wameshindwa kuripoti katika shule husika, hatua ambayo alisema isipochukuliwa kama kielelezo, inaweza kuifanya wilaya hiyo kupiga hatua za kurudi nyuma badala ya kusonga mbele.