WAKATI wananchi wengi,
wakikabiliwa na ugumu wa maisha, madereva wa wabunge nao wameibua kilio chao
wakilalamikia ukali wa maisha. Madereva hao, walilazimika kumwandikia barua
Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila wakilalamikia haki zao kukaliwa na
wabunge. MTANZANIA imefanikiwa kunasa barua hiyo ya Julai, 2012 ambayo
imesainiwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Madereva wa Wabunge, Juvenille
Joseph.
Pamoja na mambo mengine,
barua hiyo inaishutumu Ofisi ya Bunge kushindwa kusimamia maslahi yao, hali
inayowafanya waishi kwa shida.
Katika barua hiyo,
madereva hao walilamikia suala la ukosefu wa mikataba ya kazi, huku wakitaka
posho na mishahara yao itenganishwe kutoka katika akaunti za
wabunge.
“Mheshimiwa Katibu wa
Bunge, sisi ni madereva wa waheshimiwa wabunge, tunaleta kwako hoja zetu ili
ziweze kupatiwa ufumbuzi wa kina katika ofisi yako.
“Kwa kipindi chote,
madereva wa wabunge hatukuwa na mikataba ya ajira zaidi ya makubaliano ya mdomo
baina ya dereva na mbunge.
“Ndiyo maana kunakuwa na unyanyasaji mkubwa kwa
baadhi ya waheshimiwa wabunge dhidi ya madereva wao.
“Tunaomba ofisi yako
izingatie kuwa kazi ya ubunge ni ya kipindi cha miaka mitano, bila mkataba ni
vigumu kujua suala la haki za kikazi.
“Hivyo basi, tunaomba
ofisi yako isimamie kuhakikisha kuwa wabunge wote wanatoa mikataba ya ajira kwa
madereva wao,” ilisema sehemu ya barua hiyo.
Madereva hao, walisema
wamekuwa wakilipwa fedha kidogo na wabunge na wengine kudhulumiwa kabisa, licha
ya kuwapo waraka unaoelekeza malipo halisi.
Waraka huo, wenye namba
FA.155/206/01/70 wa Novemba, 2008 unaelekeza dereva anatakiwa kulipwa Sh 470,000
kwa mwezi, ikiwa ni mshahara na posho ya siku 10 mbunge akiwa
jimboni.
Madereva hao, wamehoji
sababu ya Ofisi ya Bunge kuingiza mshahara na posho zao katika akaunti za
wabunge na kueleza kuwa huo ni mwanya mojawapo wa
manyanyaso.
“Pamoja na maelekezo
mazuri ya ofisi yako, lakini wabunge wengi hawalipi mshahara na posho za
madereva wao kama waraka unavyoelekeza.
“Kwa msingi huo,
tunaomba ofisi yako ichukue jukumu la kuziondoa fedha zote zinazomhusu dereva
katika akaunti ya mbunge na kuzipeleka katika akaunti za dereva wa
mbunge.
“Hii itapunguza
malalamiko yaliyopo na yanayoendelea, kwani kwa sasa mbunge anaona kama anafanya
hisani kumlipa dereva, kwa kuwa fedha anatoa kwenye akaunti yake,” ilisema barua
hiyo.
Madereva hao, pia
walilalamikia suala la Ofisi ya Bunge kushindwa kuwatengea mafao na kusema kuwa
hali hiyo inawafanya madereva wengi wa wabunge, kukosa mwelekeo wa maisha ya
uzeeni.
Akizungumza na MTANZANIA
kwa uchungu, mmoja wa madereva wa wabunge ambaye hakutaka jina lake litajwe,
alishangaa kuona hadi sasa ofisi ya Bunge imekaa kimya juu la malalamiko
yao.
“Kilio chetu hiki
kilianza tangu 2007, lakini hakuna juhudi zozote zilizofanywa kubadili hali ya
maisha yetu kama madereva wa wabunge.
“Barua yetu kwenda ofisi
ya Bunge, tuliipeleka tangu Julai, 2012 hadi leo Katibu wa Bunge hajatujibu hoja
zetu.
“Sisi tunashindwa
kuelewa kwanini wabunge wanashindwa kuzungumzia na kutetea maslahi yetu, wakati
wao wanajiita ni watetezi wa wananchi.
“Waraka huu wa malipo
kila mbunge alipewa, lakini wanachofanya hawa jamaa kila wanapopata waraka
unaohusu stahili za madereva, wanachana ili kupoteza ushahidi waendelee kutulipa
jinsi wanavyotaka wao,” alisema.
MTANZANIA ilifanya
jitihada za kumtafuta Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila ili aweze
kuzungumzia malalamiko hayo, lakini hazikufanikiwa baada ya simu yake ya
kiganjani kuita muda mwingi bila kupokewa.
Hata hivyo Ofisa Habari
wa Bunge, Owen Mwandumbya alisema: “Siwezi kuzungumza chochote juu ya suala
hilo, kwa kuwa hilo ni suala la Katibu wa Bunge.
“Hata hivyo siwezi kujua
barua hiyo kama ilimfikia mwenyewe au laa, hilo ni suala lake mwenyewe muulize
yeye atakuwa na majibu, mimi sijui lolote kuhusu malalamiko ya madereva wa
wabunge,” alisema.
Kwa upande wake, Mbunge
wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (CHADEMA), alisema hajui kama kuna kitu
kinachoitwa chama cha madereva wa wabunge.
CHANZO:MTANZANIA
Post a Comment