Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Ibrahim Kilongo
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Jeshi la Polisi mkoani hapa limemkamata mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Haji Bakari (25) Mkazi wa Esso akiwa na kete 58 za madawa ya kulevya yanayodhaniwa kuwa ni Heroine ndani ya chumba anachoishi.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Ibrahim Kilongo alisema kwamba tukio hilo lilitokea tarehe 18/04/2013 muda wa saa 4:30 usiku maeneo ya Esso jijini hapa.
Kaimu Kamanda Kilongo alisema kwamba, mafanikio hayo yamepatikana baada ya jeshi la Polisi mkoani hapa kupata taarifa toka kwa raia wema juu ya kufanyika kwa biashara hiyo ndani ya nyumba moja iliyopo eneo hilo.
Alisema mara baada ya kupata taarifa hiyo waliifanyia kazi ambapo baaadhi ya askari waliokuwa doria walikwenda na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa akiwa kwenye chumba chake pamoja na wenzake 12 ambao walikuwa wakitumia madawa hayo.
“Mara baada ya askari hao kuingia kwenye chumba cha mtuhumiwa waliziona kete hizo zikiwa mezani huku watuhumiwa wengine wakiendelea kutumia madawa hayo” Alisema Kaimu Kamanda Kilongo.
Mpaka hivi sasa tayari watuhumiwa hao wameshafikishwa mahakamani leo asubuhi mara baada ya upelelezi wa awali kukamilika ili waweze kujibu tuhuma zinazowakabili.
Hivi karibuni Jeshi la Polisi mkoani hapa limepata mafanikio makubwa katika ukamataji wa madawa ya kulevya aina ya mirungi na bangi pamoja na operesheni ya kuteketeza madawa hayo hekari kadhaa yaliyokuwa wilayani Arumeru iliyofanyika mwanzoni mwa mwezi Machi.
Post a Comment