MAMLAKA ya hifadhi ya bonde la Ngorongoro (NCAA), inakusudia kuita wataalam wa ardhi kupima na kuhakiki mipaka yake baada ya kubaini kuwa baadhi ya watu zikiwezmo kampuni za uwindaji zimesogeza mipaka yao hadi ndani ya eneo la hifadhi.
Akizungumza na wananchi wa vijiji vya Kakesio na Osinoni, kata ya Kakesio mara baada ya kufanya ziara ya kukagua mipaka kati ya NCAA na kampuni ya uwindaji ya Mwiba holdings ya wilayani Meatu, Kaimu Mhifadhi Mkuu wa NCAA, Amiyo Amiyo alisema upimaji na uhakiki wa mipaka utafanywa na wataalam kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi Jijini Dar es Salaam.
“Baada ya kufanya ukaguzi, ambao pia ulishirikisha wananchi, Mamlaka tumebaini utata wa mipaka kati yetu na kampuni ya Mwiba. Tutahakiki na kupima upya mipaka yetu kwa kuwaita wapimaji kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam, kitengo cha ardhi ili kuondoa tatizo hili,” alisema Amiyo
Mipaka kati ya hifadhi ya Ngorongoro na kampuni ya mwiba huzingatia mipaka ya kijiografia kati ya mkoa wa Arusha na Simiyu (zamana Shinyanga) na wilaya za Ngorongoro na Meatu.
Ziara ya Amiyo ambaye ni Mkuu wa Idara ya Himasheria ndani ya NCAA ilitokana na malalamiko ya wananchi wa vijiji hivyo kuwa wamekuwa wakikamatwa na askari wa kampuni ya Mwiba wakikutwa wakichunga kwenye maeneo yaliyo ndani ya mipaka ya hifadhi ambako wanaruhusiwa kisheria kuishi na kuchunga.
Diwani wa Kata ya Kakesio, Njiloi Nanguu aliueleza msafara wa maafisa wa NCAA kuwa mgogoro huo wa mipaka unahatarisha amani baada ya wananchi kutishia kukabiliana na askari wa Mwiba kupinga kukamatwa na kupigwa faini ya papo hapo inayofikia hadi sh. 700,000 wakiwa ndani ya mipaka ya hifadhi wanakoruhusiwa kuchunga.
Kauli ya diwani huyo iliungwa mkono na Mwenyekiti wa kijiji cha Osinano, Johanes Tiamasi na Solomon Iyata ambaye ni mwakilishi wa vijana katika baraza la wafugaji kutoka kata ya Kakesio walioiomba serikali kuchukua hatua za haraka kumaliza tatizo kwa faida ya pande zote zinazohusika.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), wilaya ya Ngorongoro, William Ole Telele yeye alisema eneo lenye mgogoro wa mpaka una umuhimu mkubwa kwa wafugaji na wakazi wa Kata ya Kakesio kwani ndilo lenye malisho na maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na kunywesha kifugo.
on Wednesday, April 24, 2013
Post a Comment