Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

BALOZI IDDI APOKEA RIPOTI YA IDADI YA WATU KWA NGAZI YA UTAWALA YA SENSA YA WATU WA ZNZ


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo Zanzibar Mh. Omar Yussuf Mzee akitoa taarifa kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kwenye hafla ya uwasilishaji wa ripoti ya idadi ya watu kwa ngazi ya utawala ya sensa ya watu kwa upande wa Zanzibar hapo Hoteli ya Bwawani.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitoa Hotuba kwenye hafla ya uwasilishaji wa ripoti ya idadi ya watu kwa ngazi ya utawala ya sensa ya watu kwa upande wa Zanzibar hapo Hoteli ya Bwawani. Kushoto ya Balozi ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni ,Utalii na Michezo Mh. BIhindi Hamad na kulia ya Balozi ni Waziri anayesimamia Fedha Zanzibar Mh. Omar Yussuf Mzee.

Washiriki mbali mbali waliohudhuria hafla ya hafla ya uwasilishaji wa ripoti ya idadi ya watu kwa ngazi ya utawala ya sensa ya watu kwa upande wa Zanzibar hapo Hoteli ya Bwawani.
**********************************************
Washirika wa Takwimu katika Taasisi za Umma na zile Binafsi wanapaswa kuzitumia vizuri takwimu za matokeo ya idadi ya watu zilizopatikana ndani ya zoezi la sensa ya watu na makazi katika kupanga, kutekeleza na kutathmini mipango yao ya kiuchumi na ile ya Maendeleo.
Takwimu hizo ni vyema zikazingatiwa zaidi kwa kina katika Mikoa, Wilaya, Shehia na hata Kaya ambayo ndio maeneo wanayopatikana wahusika wakuu ambao ni Wananchi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo kwenye hafla fupi ya uwasilishaji wa ripoti ya idadi ya watu kwa ngazi za utawala ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 kwa upande wa Zanzibar iliyofanyika hapo katika ukumbi wa juu wa Hoteli ya Bwawani Mjini Zanzibar.
Balozi Seif ambe pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya Watu Tanzania aliwaambia watendaji na Wataalamu kutoka Taasisi za Umma na zile Binafsi kwenye hafla hiyo kwamba Tanzania imefanikiwa kujua idadi ya Rasilmali watu ambayo itaweza kusaidia mipango yake ya Kiuchumi .
Alitoa wito kwa watendaji wote wa Serikali wanaosimamia machapisho hayo ya sensa ya watu na makazi kuhakikisha kwamba wanakamilisha kazi hiyo kwa wakati ulikusudiwa kwa lengo la kukidhi mahitaji ya washirika wa Takwimu hizo.
Balozi Seif aliitahadharisha jamii yote Nchini kuelewa kwamba idadi ya watu imekuwa ikiongezeka kwa kasi wakati eneo la makazi yao ambalo ni ardhi liko vile vile na iwapo hakutakuwa na mipango makini linaweza kuleta athari kwa kizazi kijacho.
Balozi Seif alitoa mfano wa ongezeko kubwa ya idadi ya watu katika Mkoa wa Mjini Magharibi la wakazi laki 5.9 sawa na asilimia 46 ya wakazi wote wa Zanzibar husababisha shindikizo la utoaji huduma mbali mbali ikiwemo maji, afya usafiri umeme na miundo mbinu.
Alifahamisha kwamba viashiria vilivyoainishwa katika ripoti hiyo vitailazimu Serikali na Washirika wake kuimarisha Sera na Mipango ya Maendeleo kulingana na hali halisi ya idadi ya watu.
“ Kasi ya ongezeko la idadi ya watu ndani ya Mkoa Mjini Magharibi ni asilimia 4.2 . Hiki ni kiwango kikubwa cha kasi ya ongezeko la watu katika Mikoa kwa Zanzibar ambayo husababisha msongamano wa watu unaokadiriwa kufikia watu elfu 2,581 kwa kilomita ya mraba “. Alitahadharisha Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliyapongeza Mashirika ya UNDP, DFID, JICA, na Benki ya Dunia kwa michango yao ya uwezeshaji kiufundi na fedha iliyosaidia kufanikisha zoezi la sensa hadi kufikia hatua ya kutoa ripoti ya idadi ya watu kwa ngazi za Utawala.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo Zanzibar Mh. Omar Yussuf Mzee alisema ipo mipango ya kuangalia sababu za msingi zilizopelekea Mkoa Mjini Magharibi kuwa na idadi kubwa ya watu.
Alisema Serikali kupitia Taasisi zake italazimika kufanya utafiti wa kina utakaowezesha kutafuta mbinu za kitaalamu za kupunguza ongezeko hilo kwa kuweka vishawishi vitakavyovutia watu bila ya kuleta migongano.
Mh. Omar Yussuf alifahamisha kwamba Sensa ya Watu imeisaidia Serikali kuliona tatizo hili kubwa ambalo pasipokuwa na utaratibu muwafaka wa kukabiliana nalo mapema linaweza kuleta athari ya kuvurugika kwa ustawi wa Jamii.
“ Inatisha kuona ardhi ya Mkoa wa Mjini Magharibi pekee imebeba idadi kubwa ya watu inayokadiriwa kufikia laki 5.9 ambayo hailingani na mahitaji yaliomo ndani ya mkoa huo “. Alieleza Waziri Omar Yussuf.
Mapema Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Nd. Mohd Hafidh Rajab alisema Ripoti iliyotolewa ya mgawanyiko wa idadi ya watu kuanzia Taifa hadi Kata itasaidia dira za maendeleo kwa Serikali zote mbili.
Nd. Hafidh alisema takwimu zilizopatikana kufuatia kumalizika kwa upembuzi wa matokeo ya sensa ya idadi ya watu zitatoa fursa sahihi kwa wahusika wa mipango ya maendeleo kupanga mipango yao kulingana na idadi ya watu waliomo kwenye maeneo husika.
Mtakwimu Mkuu huyo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar alitoa mfano wa utambuzi wa Mkoa wa Kusini Pemba ambao umebainika kuwa na idadi kubwa ya wakazi iliyofikia asilimia 5.4 kwa kaya moja.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
13/4/2013.
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top