*******
Baada ya kufumuliwa mabao 3-0 na vinara wa ligi kuu soka Tanzania bara Dar Young Africas, leo hii maafande wa JKT Ruvu wamepunguza machungu baada ya kuwatungua vibonde wa ligi hiyo Africa Lyon bao 1-0 mchezo uliopigwa dimba la Chamazi jijini Dar es salaam.
Kocha msaidizi wa JKT Ruvu Greyson Haule alisema wapinzani wao leo wamecheza vizuri sana lakini bahati katika mchezo huo iliangukia upande wao.
“Hakika mchezo ulikuwa mgumu, lakini kiwango cha timu yangu kinaniridhisha siku hadi siku licha ya kuachwa na kocha wetu Charles Kilinda, lakini sasa tunaye mwalimu Keny Mwaisabula ambaye kiukweli kachangia mambo mengi sana” . Alisema Haule.
Haule aliongeza kuwa kushinda mchezo wa leo ni hatua kubwa kwao kwani wanajipa matumaini mazuri ya kufanya vizuri mechi zilizosalia.
Kocha huyo alisema sasa hesabu zao ni mchezo ujao dhidi ya maafande wa Tanzania Prisons “Wajelajela” ambao wanajiandaa kunyakua mzigo wa pointi tatu muhimu.
“Tunajiandaa kufanya vizuri na lazima shughuli iwe nzito na Prisons, tuna morali kubwa na mashabiki wetu wasiwe na wasiwasi kwasababu tuna uhakika wa kubakia ligi kuu msimu huu”. Aliongeza Haule.
Baada ya shughuli ya leo Taifa, hapo kesho kibarua kingine ni kati ya wekundu wa Msimbazi Simba watakaowakaribisha maafande wa Ruvu Shooting kutoka mkoani Pwani katika dimba la taifa.
Kuelekea katika mchezo huo, kocha msaidizi wa klabu ya simba, Jamhuri Kiwhelo Julio alisema wachezaji wote wapo salama na wanajiandaa kukumbana na wanajeshi hao ambao wako sawa kwa kila idara”.
“Shooting ni timu nzuri na kila mtu anajua, matokeo yoyote yatakayopatikana tutamshukuru Mungu, wachezaji wanajua ugumu wa mechi lakini kocha Liwieg kushirikiana na mimi tumefanya maandalizi kwa wachezaji wetu”. Alisema Julio.
Julio alisema kufungwa ni jambo la kawaida katika mchezo wa soka huku akitolea kipigo cha jana walichokipata Barcelona kutoka kwa Bayern Munich cha mabao 4-0.
“Jana kila mtu alikuwa anashangaa, lakini soka ni mchezo wa mahesabu, ukikosea unapigwa, na ndio maana jana Barca walicheza ovyo wakapigwa kipigo cha mbwa mwizi, na sisi tukifungwa sio ajabu”. Alisema Julio.
Kocha huyo aliwataka mashabiki wa simba kuwaombea dua njema wachezaji wao ili waamke salama hapo kesho, lakini pia wajitokeze uwanjani kuwashangilia vijana wao.
Kwa upande wa Ruvu Shooting, afisa habari wa klabu hiyo Masau Bwire alisema wamejiandaa kuwafunga simba wanaosikika wakisema wanataka kulinda heshima mechi zilizosalia baada ya kupoteza ubingwa wao msimu huu..
“Tumesikia maneno ya wana Simba kuwa wanataka kutufunga na kulinda heshima, mwalimu Mkwasa mnamjua, kafanya mambo yake na kesho mnyama hatoki kwetu”. Alijigamba Masau.
(Na Baraka Mpenja wa Fullshangwe Dar es salaam)
Post a Comment