Mnamo tarehe 23 April,
2013 majira ya saa tisa alasiri, huko wilayani Liwale mkoani Lindi, kundi la
watu wanaodhaniwa kuwa ni wakulima wa Korosho walijaribu kuzuia gari lililokuwa
na malipo ya korosho wakipinga malipo ya pili ya Korosho na kuanza kufanya
vurugu na uhalibifu mkubwa wa mali, ambapo
mpaka sasa taarifa za
awali zinaonyesha kuwa nyumba kumi na nne (14) zimechomwa moto, baadhi ya mifugo
imejeruhiwa na kuangamizwa na kufanyika uharibifu wa miundombinu ya
barabara.
Kufuatia tukio hilo,
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema ametuma timu maalum ikiongozwa na
Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini DCP Issaya Mngulu kwenda
kuongeza nguvu mkoani humo kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa katika
kuhakikisha kuwa hali ya amani na utulivu inarejea haraka na wale wote
waliohusika kufanya vitendo vya uhalifu wanakamatwa na kufikishwa mahakamani ili
sheria iweze kuchukua mkondo wake, mpaka sasa jumla ya watuhumiwa kumi na tisa
(19) wamekamatwa kwa mahojiano.
Aidha, Jeshi la Polisi
nchini linalaani vikali vitendo hivyo vya wananchi kujichukulia sheria mkononi
na badala yake kuwataka wananchi kufuata njia ya kufanya majadiliano pale ambapo
kutakuwa na migogoro ya aina yoyote ndani ya jamii. Majadiliano yatasaidia
kuepusha madhara yanayojitokeza ikiwemo watu kupoteza maisha, uhalibifu wa mali
na misongamano ya wahalifu magerezani.
Wakati hatua hizo za
kisheria zinaendelea kuchukuliwa, Jeshi la Polisi linawaomba wananchi kuwa
watulivu na waendelee kutoa ushirikiano ili kuweza kuwabaini wahalifu hao
wachache wanaochochea vitendo vya vurugu na kufanya uhalibifu wa mali ili
hatiamae waweze kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Taarifa zaidi juu ya tukio
hili zitaendelea kutolewa na uongozi wa mkoa wa Lindi baada ya tathmini ya
uharibifu uliofanyika kukamilika.
Imetolewa
na:-
Advera Senso-
SSP
Msemaji wa Jeshi la
Polisi (TZ).
Post a Comment