CHAMA cha Waandishi wa Habari za
Michezo Tanzania (TASWA) kinasikitika kuwajulisha wadau wake kuwa
bonanza la wanahabari lililopangwa kufanyika kesho viwanja vya Sigara
(TCC) Chang’ombe sasa litafanyika viwanja vya Leaders Klabu, Kinondoni
Dar es Salaam siku hiyo hiyo ya Aprili 6,2013.
Uamuzi huo wa kushtukiza umefikiwa
kwenye kikao cha dharura kilichofanyika jana usiku kati ya TASWA ambao
ni waandaaji na wadhamini wa bonanza hilo Kampuni ya Bia Tanzania (TBL)
kutokana na kushindwa kuafikiana baadhi ya mambo na menejimenti ya
viwanja hivyo.
Tunawaomba sana radhi wanahabari
kwa usumbufu mkubwa ambao wataupata kutokana na mabadiliko haya, lakini
tunaamini yamefanyika kwa dhamira nzuri yenye nia ya kuboresha bonanza
letu na kwa kiasi kikubwa litafana kwa asimilia 100.
Dhamira ya TASWA ni kuona inakuwa
na bonanza zuri lisilokuwa na aina yoyote ya kwikwi, hivyo tayari
tumeshamalizana na menejimenti ya viwanja vya Leaders Klabu na kila kitu
kitakuwa safi kuliko maelezo.
Pia tunaishukuru menejimenti ya
viwanja vya Sigara kwa ushirikiano iliotupa kwa nia ya kufanya bonanza
hilo eneo lao, ingawa ndoto zetu hazikutumia, lakini tunaamini siku za
usoni tunaweza kufanya nao kazi.
Tunasisitiza lengo la bonanza letu
ambalo mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe
ni kuwaweka pamoja waandishi wote wa habari bila kujali ni wa siasa,
michezo, uchumi, afya na mambo mengine pamoja na wafanyakazi wa vyombo
mbalimbali vya habari, ili kubadilishana mawazo na kufurahi pamoja.
Awali bonanza letu ilikuwa
lifanyike Leaders Klabu, lakini tulilihamishia viwanja vya Sigara
kutokana na wadau wengi kuomba wapate nafasi ya kwenda kutazama mechi ya
Kombe la Shirikisho kati ya Azam ya Tanzania na Barrack Young
Controllers ya Liberia kesho. Hata hivyo tunaamini wahariri wa habari za
michezo watajipanga vizuri kulingana na mabadiliko hayo na hakuna
litakaloharibika.
Pia katika kuboresha bonanza hilo
litakalotumbuizwa na bendi ya Extra Bongo na kundi la taarabu la Jahazi
Modern, kutafanyika mchezo wa soka kati ya wanahabari ambao wameoa na
wale ambao hawajaoa utakaofanyika baada ya michezo ya kawaida baina ya
vyombo vya habari kumalizika.
Bonanza litaanza saa tatu asubuhi
kwa washiriki kucheza michezo mbalimbali ikiwemo soka, netiboli, wavu,
kuruka kichura, aina mbalimbali za riadha, kuvuta kamba na kucheza
muziki. Bonanza litamalizika saa moja usiku.
Ahsanteni.
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
05/04/2013
Post a Comment