Na Benedict Liwenga-Maelezo, Dodoma
Kila mkoa unastahili kuwa na kiwanja cha Ndege daraja la 3 (C) chenye uwezo wa kuhudumia ndege za abiria zenye kubeba abiria 70, kwa mujibu wa sera ya uchukuzi ya mwaka 2003.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Uchukuzi, Mhe. Charles Tizeba wakati akijibu swali lililoulizwa bungeni na Mhe. Mustapha Boay Akunaay (Mbulu) aliyetaka kujua serikali itajenga lini Uwanja wa Ndege wa Manyara ilioahidi kujenga mwaka 2003.
Mhe. Tizeba ameliambia Bunge kuwa kwa kuwa uwezo wa serikali kujenga viwanja vya ndege katika kila mkoa ni mdogo, Wizara inazingatia ushauri wa Bunge kwamba tuandae miradi ambayo serikali itakuwa na uwezo wa kuitekeleza katika kila bajeti.
Amesema kinachofanyika kwa sasa ni kutekeleza miradi hiyo kwa awamu, “mfano kwa sasa miradi ya viwanja vya ndege inayoendelea ni Kigoma, Bukoba. Tabora, Mafia, Songwe na Mwanza”.
Kwa mwaka huu wa fedha 2013/2014 miradi ya viwanja vya ndege vya Sumbawanga, Shinyanga na Mtwara itatekelezwa kwa fedha za mkopo toka Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (European Investment Bank).
Mhe. Tizeba amesema miradi ya viwanja vya ndege iliyopo katika hatua za awali za utekelezaji ikiwa ni pamoja na kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ni vya Iringa, Njombe, Songea, Mtwara, Tanga, Kilwa Masoko, Lindi, Musoma, Singida na Lake Manyara (Karatu).
Kuhusu uwanja wa ndege wa mkoa wa Manyara Mhe. Tizeba amesema kuwa makubaliano ni kuwa kwanza mkoa uandae ramani ya mipango miji ambayo itaainisha eneo ambalo litajengwa kiwanja cha ndege. Swali la nyongeza liliulizwa kwa Mhe. Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mhe. Akunaay ambalo lilitaka kujua serikali ina mpango gani kushughulikia matatizo ya viwanja vingi vya ndege kukosa taa kwa ajili ya safari za usiku, Mhe. Naibu Waziri wa Uchukuzi Tizeba alikili kuwa viwanja vingi vya ndege kutokuwa na taa lakini akaahidi kuwa serikali itajitahidi kutatua tatizo hilo.
Post a Comment