Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

VINARA YANGA WALAZIMISHA SARE, NDUGU WAWILI MTIBWA NA KAGERA WAIBUKA KIDEDEA LEO!


mkwakwani
Ligi kuu soka Tanzania bara imeendelea kushika kasi kwa mechi tatu kupigwa katika miji ya Tanga, Morogoro na Kagera.
Uwanja wa CCM mkwakwani jijini Tanga vinara wa ligi hiyo Yanga wamepunguzwa kasi baada ya kulazimisha sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya maafande wa Mgambo JKT.
Bao la Mgambo limefungwa dakika ya 37 kipindi cha kwanza kupitia kwa nyota wake Fulljelly Maganga wakati kwa upande wa Yanga wamesawazisha dakika ya 87 kupitia kwa winga mwenye kasi kubwa Simon Msuva .
Baada ya Mchezo huo kumalizika katibu mkuu wa Mgambo, Antony Mgaya alisema mechi ilikuwa ngumu lakini wamecheza vizuri na kuwahimili wapinzania wao waliojaa sifa kwenye vyombo vya habari.
“Yanga ni timu ya kawaida sana, wamecheza soka la kawaida na kama tusingefanya makosa dakika za lala salama walikuwa wameshatolewa nishai”. Alisema

Kwa upande wa Yanga kupitia kwa afisa habari wake Baraka Kizuguto walisema mwamuzi amechezesha chini ya kiwango na kuharibu ladha ya soka CCM Mkwakwani.
“Hakika kuna mambo ya ajabu, mwamuzi kachezesha ovyo kweli, kawabeba Mgambo, lakini sisi tunajipanga kwa mchezo ujao dhidi ya JKT Ruvu ambao lazima tuwafunge halafu tujitangazie ubingwa msimu huu”. Alisema Kizuguto.
Huko mashamba ya miwa Manungu Turiani Mkoani Morogoro, watengeneza sukari wa Mtibwa sugar wameshuka dimbani dhidi ya maafande wa JKT Oljoro na kuibuka na ushindi wa bao 1-0.
Bao la Mtibwa limefungwa kupitia kwa kiungo wake Twaa Ally dakika ya 37 ya kipindi cha kwanza.
Msemaji wa klabu hiyo Tobias Kifaru Lugalambwike alisema mchezo huo ulikuwa wa kusisimua kutokana na uwezo wa wapinzani wao.
“Tunajipanga dhidi ya Lyon watakaokuja nyumbani mchezo ujao, tunajipanga kupata ushindi na vijana wetu wapo katika morali kubwa sana”. Alisema Kifaru.
Mchezo mwingine umepigwa katika dimba la kaitaba Mkoani Kagera baina ya wenyeji wa uwanja huo vijana wa Abdallah Kibadeni “King Mputa”, Kagera Sugar dhidi ya vijana wa mitaa ya kishamapanda jijini Mwanza Toto Africa wanaonolewa na kocha John Tegete.
Kibaden alizungumza na mtandao huu na kutujuza matokeo kuwa wameibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Toto na kujisimika zaidi nafasi ya tatu ya ligi hiyo.
“Toto wamecheza vizuri na kama wangekuwa wanacheza hivi siku zote hakika wasingekuwa hapa walipo, lakini sisi tulijipanga zaidi na ndio maana tumewafunga nyumbani”. Alijigamba Kibaden.
Baada ya michezo hiyo Yanga bado wapo kileleni wakijikusanyia pointi 53 kibindoni na kuchanja mbuga kuelekea ubingwa wa ligi kuu msimu huu unaomilikiwa na watani zao wa jadi klabu ya simba ya Dar es salaam “Taifa Kubwa”, nafasi ya pili wapo Azam wenye poiti 47, Kagera wapo nafasi ya tatu wakiwa na pointi 40 huku Simba wakibaki nafasi ya nne na pointi zao 36 kibindoni.
 
(Na Baraka Mpenja wa Fullshangwe Dar es salaam)
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top