Nyumba zaidi ya saba za
kuishi na nane za maduka pamoja na mifugo; vyote vikimilikiwa na viongozi wa
CCM, akiwamo mbunge na madiwani wilayani Liwale, vimeteketezwa kwa moto na
kuharibiwa na wahalifu.
Mali hizo
zikiwamo za viongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Ilulu, Liwale,
vimeteketezwa kwa kilichdaiwa kuwa ni kupinga kulipwa malipo kidogo ya korosho,
msimu wa mwaka jana.
Taarifa ya
Polisi, ilisema jana kuwa watu wanaodhaniwa kuwa wakulima wa korosho, walijaribu
kuzuia gari lililokuwa na malipo ya korosho, wakipinga malipo ya pili ya zao
hilo na kufanya vurugu na uharibifu wa mali.
Hata hivyo,
Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima, alionesha wasiwasi
bungeni akisema huenda kuna baadhi ya watu, wakiwamo wanasiasa walio nyuma ya
matukio hayo ili kuficha uovu wao na wengine kujinufaisha kwa maslahi
binafsi.
Waliochomewa
nyumba katika vurugu hizo, ni Mbunge wa Liwale, Faith Mitambo, Mwenyekiti wa CCM
wa Wilaya ya Liwale, Mohammed Mngomambo, Katibu Mwenezi wa CCM wa Wilaya,
Abdallah Chande na Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Ilulu, Hamza
Mkunguru.
Wengine walioathiriwa na
vurugu hizo ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale, Diwani wa CCM,
Abas Mtalilo ‘Chigogola’ na madiwani wenzake, Hassan Myao, Musa Mkoyage, Mzee
Salehe na Amina Mnoche.
Akizungumza na
mwandishi jana, Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, Hemed Ndimane alisema
duka lake la vyakula lilivamiwa na mali zote kuporwa. Ng’ombe watano
waliouawa kwa kukatwa mapanga, ni mali ya Mkunguru.
Naye Mitambo
alisema nyumba zake mbili zilichomwa moto huku moja ikiteketezwa kabisa,
nyingine ikibomolewa paa na kunyofolewa milango na
madirisha.
Mbunge huyo
alisema Chigogola alichomewa nyumba ya
vyumba 11, pikipiki mbili, trekta dogo
‘power tiller’ na ng’ombe wake 12 waliuawa.
Alisema
Mngomambo alichomewa nyumba kama alivyofanyiwa Chande; sawa na madiwani wote wa
kata za mjini Lindi.
Ingawa Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Lindi, George Mwakajinga alisema atatoa taarifa baadaye,
lakini taarifa ya makao makuu ya Polisi, Dar es Salaam, ilisema mpaka jana
watuhumiwa 19 walikuwa wamekamatwa kwa mahojiano. Vurugu hizo zilizoanza juzi
asubuhi, eneo la Liwale ‘B’.
Kwa mujibu wa
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Abdallah Ulenga, Kamati ya Ulinzi na Usalama
ilikutana jana baada ya tukio hilo huku Kamanda akisisitiza kuwa hadi jana
mchana walikuwa wakiendelea na vikao, kabla ya kutoa taarifa kamili kwa vyombo
vya habari.
Ulenga alisema
wananchi hao walivamia maduka na nyumba za viongozi hao na kuziteketeza kwa
moto, kutokana na madai kwamba walipata malipo ya pili ya Sh 200 badala ya Sh
600 kwa kilo.
“Lazima
tufahamu ni kwa nini, kama mauzo yalikuwa Sh 1,100 kwa kilo, wataalamu
wanatakiwa watoe maelezo juu ya malipo hayo yaliyofanywa Liwale,” alisema
Ulenga.
Bei ya korosho
kwa kilo ilikubaliwa kuwa Sh 1,200 kwa kilo, lakini baada ya kushuka kwa bei
katika soko la dunia, ilishuka na kuwa kati ya Sh 1,000, Sh 1,070 na
1,100.
Mwenyekiti wa
Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Lindi, Killian Kapamba alisema hajui kama vurugu
hizo ni za ununuzi wa korosho au za kisiasa, kwa kuwa mali za viongozi wa
kisiasa ndizo zilizoharibiwa.
Alisema inakuwa
vigumu kubaini sababu za vurugu hizo kwa kuwa pia Chama cha Msingi cha Ushirika
cha Umoja, ambacho ndicho chenye jukumu la kutoa malipo hayo, kilikuwa
hakijaanza kutoa malipo ya pili kwa wakulima na wanachama.
Hata hivyo,
taarifa kutoka Polisi zilisema baadhi ya viongozi waliodaiwa kuhusika na
uchochezi huo, wamekamatwa.
Akizungumza
bungeni jana, Malima alieleza kusikitishwa na vitendo vya wananchi kuchukua
hatua mkononi na kuharibu mali bila kutoa fursa ya matatizo yao
kushughulikiwa.
Malima ambaye
alionesha wasiwasi wa wanasiasa kuwa nyuma ya vurugu hizo, alisema hayo baada ya
Mbunge wa Viti Maalumu, Zainabu Kawawa (CCM), kuliwasilisha suala hilo
bungeni.
Zainabu wakati
akitoa hoja hiyo, aliitaka Serikali kutengeneza utaratibu utakaowezesha
wakulima hao kulipwa fedha wanazodai, ambazo ni Sh 400 walizopunjwa katika
malipo ya korosho.
“Naomba nieleze
masikitiko yangu juu ya tukio la jana (juzi) usiku katika wilaya ya
Liwale…wakulima wa korosho wameghadhabika na kuamsha mapambano kati yao na
polisi, hadi kusababisha uharibifu wa mali zikiwamo nyumba za viongozi,” alisema
Kawawa.
Alisema wakulima
hao walichukua hatua hiyo, baada ya kutotimiziwa malipo ya korosho ya Sh 1,200
kwa kilo. Alisema awali walilipwa Sh 600 tu, baadaye wakapewa Sh 200 na hadi
sasa hawajamaliziwa Sh 400 zilizobaki.
“Kwa maana hiyo
wakulima hao walilipwa Sh 800 tu, wanachodai ni tofauti ya Sh 400, nimezungumza
na Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika amenieleza kuwa bei ya korosho
imekuwa ikibadilikabadilika,” alisema Zainabu.
Aliiomba
Serikali iingilie kati mgogoro huo kwa kuahidi kama inaweza kufidia Sh 400, ili
mkulima wa korosho alipwe Sh 1,200.
Akijibu hoja
hiyo, Malima alisema: “Hii lazima tukubaliane kuwa kuna vitu vimejificha
humu, sehemu zote ambazo zinalimwa korosho ikiwamo Mkuranga, kuna matatizo
ambayo yanasababisha korosho kutouzwa na matatizo haya hayalingani kote,
yanatofautiana,” alisema.
Alisema
kwingine matatizo ya wakulima wa korosho yanatokana na vyama vya ushirika wakati
kwingine kuna matatizo ya wanunuzi.
“Sasa mimi
nashangaa kwa nini vurugu za namna hii zinaibuka? Kuna sababu nyingi, pengine
hata hawa viongozi wa ushirika wanahusika ili kuficha maovu yao au hata tu
masuala ya kisiasa,” alisema
Malima.
Kutokana na
vurugu hizo, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Said Mwema, ametuma timu maalumu
ikiongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini, Issaya
Mngulu, kwenda kuongeza nguvu mkoani humo kwa kushirikiana na uongozi wa
mkoa.
Timu hiyo imetakiwa
kuhakikisha hali ya amani na utulivu inarejea haraka na waliohusika na uhalifu,
wanakamatwa na kufikishwa mahakamani, ili sheria ichukue mkondo
wake.
Post a Comment