Takriban watu 260,000
walifariki dunia wakati wa ukame ulioikumba Somalia kuanzia mwaka 2010 hadi
2012, utafiti umebaini.
Nusu ya waliofariki
dunia walikuwa ni watoto wenye umri chini ya miaka mitano, inaeleza ripoti ya
shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO, pamoja Mtandao wa Kuonya
Mapema Kuhusu Majanga ya Ukame unaofadhiliwa na Marekani.
Idadi ya vifo ilikuwa
kubwa kuliko ile iliyokadiriwa ya watu 220,000 waliofariki wakati wa ukame wa
mwaka 1992.
Janga hilo
lilisababishwa na ukame mkali, uliochochewa na mapigano kati ya makundi hasimu
yaliyokuwa yakigombea madaraka.
Umoja wa Mataifa kwa
mara ya kwanza ulitangaza hali ya ukame Julai 2011 katika mikoa ya Somalia ya
Bakool uliopo kusini na ule wa chini wa Shabelle, ambayo ilikuwa inadhibitiwa
na kundi la wanamgambo wa Al – Shabab wenye mafungamano na Al – Qaeda.
Lakini kundi hilo
lilikanusha kuwepo kwa hali hiyo na kuyapiga marufuku mashirika kadhaa ya
misaada ya nchi za magharibi kufanya shughuli zake katika maeneo hayo.
Baadaye ukame
ulisambaa katika maeneo mengine ukiwemo mkoa wa kati wa Shabelle na Afgoye na
katika kambi za watu wasiokuwa na makaazi katika maeneo yaliyokuwa yakidibitiwa
na serikali katika mji mkuu Mogadishu.
Mchumi Mwandamizi wa
shirika la FAO, Mark Smulders amesema, ukweli kuhusu ukubwa wa janga hilo la
kibinadamu umeibuka kwenye utafiti uliofanywa kwa kushirikiana na Mtandao wa
Kuonya Mapema Majanga ya Ukame, Fews Net.
“Kwa kawaida,
kukadiria vifo wakati wa dharura ni sayansi isiyo rasmi, lakini kutokana na
ubora na kiwango cha takwimu zilizokuwepo, tuna uhakika na utafiti huo”,
amesema ofisa wa Fews Net Chris Hillbruner.
“Utafiti huo unaeleza
kuwa, kilichotokea Somalia ni moja ya majanga mabaya kabisa ya ukame kuwahi
kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 25 iliyopita, “ ameongeza.
Inakadiriwa kuwa 4.6%
ya jumla ya idadi ya watu na 10% ya watoto chini ya umri wa miaka mitano
walifariki dunia huko maeneo ya kusini na kati mwa Somalia, imeeleza ripoti
hiyo.
“Ripoti hiyo
imethibitisha kuwa hatua za ziada zingechukuliwa kabla ya ukame huo
haujatangazwa, amesema Phillippe Lazzarini, Mratibu wa Shughuli za Kibinadamu
wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia.
Somalia ilikumbwa na
ukame mkali mwaka 2011, ulioathiri zaidi ya watu milioni 13 katika eneo lote la
Pembe ya Afrika.
Maelfu ya watu
walikimbia makaazi yao wakisaka chakula. Umoja wa mataifa ulitangaza ukame huo
kumalizika Februari 2012.
Kwa zaidi ya miaka 20
ya vita vya weyewe kwa wenyewe, Somalia imeshuhudia wababe wa kivita wa koo,
wanasiasa mahasimu na vikundi vya wanamgambo vikigombea madaraka, hali
iliyoruhusu kushamiri kwa ukosefu wa utawala wa sheria.
Septemba mwaka jana,
serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa iliingia madarakani baada ya
miaka nane ya utawala wa mpito, hatua iliyoleta utengamano katika baadhi ya
maeneo.
chanzo bbc swahili
Post a Comment