Siku moja baada ya Kiongozi wa Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe na wabunge wenzake watatu kuzuiwa kuingia
bungeni juzi, uongozi wa Bunge umesisitiza kuwa kombati zao zinakiuka
kanuni.
Mbowe na wabunge wenzake wa CHADEMA, Tundu Lissu (Singida
Mashariki), Godbless Lema (Arusha Mjini) na Ezekiel Wenje (Nyamagana) walizuiwa
na askari kwa madai kuwa wamevalia sare za chama ambazo kikanuni
haziruhusiwi.
Uamuzi huo
uliibua hali ya sintofahamu kwa wabunge wa CHADEMA kutokana na Mbowe kuvalia
vazi hilo mara nyingi tangu aingie bungeni mwaka 2010.
Licha ya kanuni za
Bunge kuruhusu vazi la ‘safari suti’ kwa wanaume lenye mshono kama kombati
zinazovaliwa na baadhi ya wabunge wa CHADEMA, Tanzania Daima Jumatano limebaini
kuwa uamuzi huo unaacha maswali mengi yanayohitaji majibu.
Akizungumzia
uamuzi huo jana, Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alisema suti hizo za
wabunge wa CHADEMA zilikiuka kanuni ya 149 (3) (b) (i).
Kipengele hicho
cha kanuni kinasomeka kuwa inaruhusiwa suti ya Kiafrika au safari ya mikono
mirefu au mifupi yenye ukosi au shingo ya mviringo na yenye fulana au bila
fulana ndani, ya rangi moja, isiyokuwa na nakshi, pamoja au bila
baragashia.
Joel alifafanua kuwa yawezekana huko nyuma wamekuwa wakifanya
makosa kwa kuwaruhusu wabunge hao kuingia na suti hizo, lakini sasa kuanzia juzi
wameamua kuanza
kuchukua hatua ya kuwazuia.
“Zile wanasema sio sare
ya chama, lakini wote tunawaona kwenye mikutano na shughuli za chama ndizo
zinavaliwa na isitoshe tuliwahi kuwatahadharisha kuwa ziko kinyume na kanuni
wasizivalie bungeni ila wamekuwa wakiendelea kuzivaa,” alisema.
Licha ya
kanuni hiyo kuwa kimya kuhusu kuvaa sare za vyama bungeni, Joel alisema kuwa
uamuzi huo ulikuwa ni busara ya spika wa wakati huo, Samuel Sitta, lakini
haujaingizwa kwenye kanuni kimaandishi.
Tanzania Daima Jumatano lilitaka
kufahamu ni kwanini uamuzi huo ukaanza ghafla juzi baada ya wabunge wa CHADEMA
kurejea kutoka jijini Arusha, na Joel bila kufafanua alisema: “Kawaulize
walipanga nini wakiwa Arusha? Ndiyo maana tukaamua kuchukua hatua.
“Bora
tukaonekana tumewaonea kuliko kuendelea kufumbia macho kanuni. Tuwe wawazi
kombati zao zina nakshi kupitiliza kwa mujibu wa kanuni. Kwanini wakina Halima
Mdee na Vicent Nyerere tuliwaacha wakaingia? Mbona kombati za Zitto
zinatofautiana na wengine?”
Alipotakiwa kufafanua kama kweli walishaonywa
wasivae kombati hizo bungeni,
Mkurugenzi wa Mawasiliano na Habari wa
CHADEMA, John Mnyika alisema Joel hajui kanuni za Bunge ndiyo maana amekuwa
anampotosha spika na viongozi wa Bunge kufanya uamuzi wa
ajabu.
“Wametuzuia juzi kwa sababu ya maelezo ya akina Pinda na Serikali
ya CCM, sio kwa sababu ya ukiukwaji wa kanuni za Bunge. Kumekuwa na utamaduni wa
hovyo wa kutafsiri vibaya kanuni za Bunge kwa lengo moja tu, kuwadhibiti
CHADEMA,” alisema.
Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, alitolea mfano
akisema kuwa walizuiliwa kuingia ukumbini na askari polisi wasiokuwa na mamlaka
ya kuwazuia kuingia ndani bali walitakiwa wasubiri amri ya spika kuwatoa
ukumbini ndipo wawatoe.
“Hayo yote hawezi Joel kufahamu, anafanyia uzoefu
alioupata wakati anafanya kazi Makao Makuu ya CCM wakati wa Bunge la chama
kimoja,” alisema Mnyika.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Lissu
ambaye pia ni Mnadhimu wa kambi ya upinzani bungeni, alisema kuwa walishangazwa
na uamuzi huo wakati mavazi hayo wamekuwa wakiyavaa miaka yote na kuingia nayo
bungeni.
Lissu alisema kuwa hatua hiyo waliichukulia kama mkakati maalumu
wa Serikali ya CCM kutaka kuwazima kabisa kuhakikisha hawapati nafasi ya kuingia
bungeni ili kujibu tuhuma walizosingiziwa kuhusiana na mlipuko wa bomu jijini
Arusha.
“Sisi hali hiyo tulianza kuishtukia tangu asubuhi tulipoingia
kwenye eneo la Bunge, kama mligundua kulikuwa na askari wengi sana kila kona
kuliko kawaida kana kwamba nchi imepinduliwa. Kinyume na utaratibu wa kanuni
askari wa kawaida wameingizwa hadi bungeni,” alisema.
Hata hivyo, pamoja
na uamuzi huo, kanuni za Bunge hakuna mahali zinazuia mbunge kuvaa sare ya chama
chake isipokuwa kanuni zimeainisha aina za mavazi ya kuvaliwa na wabunge
wanawake na wanaume.
Kwa mujibu wa kanuni ya 149 (3)(b) kwa wanaume
wanaruhusiwa kuvaa (i) suti ya Kiafrika au safari ya mikono mirefu au mifupi
yenye ukosi au shingo ya mviringo na yenye fulana au bila fulana ndani, ya rangi
moja, isiyokuwa na nakshi, pamoja au bila baragashia;
(ii) vazi la
kimwambao yaani kanzu rasmi na nadhifu, koti, baraghashia na makubadhi au viatu;
(iii) suti kamili ya kimagharibi ya rangi kadiri isiyomeremeta; (iv) koti aina
ya blazer na tai, pamoja na suruali yoyote ya heshima; au (v) tarbushi na
kilemba cha Singasinga, au kilemba chochote kinachovaliwa kwa mujibu wa masharti
ya imani au mila.
Read more: http://talkbongo.blogspot.com/2013/06/chadema-wakatazwa-kuvaa-kombat-bungeni.html#ixzz2XLcNvHA1
Loading...
Post a Comment