Mkuu
wa Wilaya ya Kusini Haji Makungu Mgongo akifungua warsha ya sera ya
Taifa ya Ardhi iliyowashirikisha Masheha wa Wilaya hiyo. Kushoto ni
Mratibu wa Mradi wa SMOLE Saleh Kombo na kulia ni mkufunzi wa warsha
Mlenge Hassan.
Masheha
wa wilaya ya kusini wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya Haji Makungu Mgongo
(hayupo pichani) alipokuwa akifungua warsha ya sera ya ardhi katika
afisi ya Wilaya Makunduchi. (Picha na Ramadhani Ali- Maelezo Zanzibar)
NA RAMADHANI ALI – MAELEZO ZANZIBAR
Masheha
wa Wilaya mbili za Mkoa wa Kusini Unguja wameshauri kuwepo Mahakama ya
Ardhi na kitengo cha usajili wa Ardhi kuanzia ngazi ya wilaya katika
Sera mpya ya ardhi inayoandaliwa ili kupunguza migogoro mingi
inayoikabili sekta hiyo.
Ushauri
huo wameutoa katika Warsha ya kuelimisha na kukusanya maoni ya wadau
kwa ajili ya sera ya Taifa ya Ardhi iliyoandaliwa na Mradi wa usimamizi
endelevu wa ardhi na Mazingira (SMOLE) awamu ya pili Afisi ya Wilaya
Kusini Makunduchi na Halmashauri ya Wilaya ya Kati Dunga.
Wamesema
matatizo ya ardhi hasa vijijini yamekuwa makubwa na ufumbuzi wake
huchukua muda mrefu kutokana na kukosa vitengo vinavyoshughulikia ardhi
na Mahamakama ya ardhi katika ngazi za Wiaya.
“Kesi
zinazohusu ardhi ni nyingi na mahakama ya ardhi ipo mjini hili ni
tatizo kubwa hivyo sera mpya inayoandaliwa ifikirie kuanzisha mahakama
za ardhi kuanzia ngazi ya Wilaya,” alisema Sheha wa Chwaka Msaraka
Pinja.
Katika
Sera mpya ya Ardhi inayotayarishwa, Masheha wa Wilaya ya Kusini na
Kati wamependekeza sheria za ardhi ambazo hivi sasa zinasimamiwa na
taasisi tano ziwekwe katika taasisi moja ili kupunguza urasimu katika
kuzitekeleza.
Taasisi
hizo ni Idara ya Ardhi na Usajili, Idara ya Misitu na Mali
zisizohamishika,Idara ya Mipango miji na vijiji, Idara ya upimaji na
ramani na Idara ya Mazingira.
Sheha
wa shehia ya Mzuri Khamis Ramadhani ameshauri sheria za ardhi zilizopo
zifanyiwe mapitio upya na ikiwezekana zipunguzwe kwani hivi sasa ni
nyingi na utekelezaji wake unapelekea kuwa mgumu.
Aidha
viongozi hao wa shehia wametaka sera ya ardhi iweke wazi idadi ya Eka
ambazo mtu mmoja anatakiwa azimiliki kwa shughuli za maendeleo na watu
wanaojikusanyia maeneo makubwa ya ardhi yachukuliwe na kupewa watu
ambao hawana ardhi.
“Kuna
baadhi ya watu wanamiliki mashamba makubwa kila sehemu na wala
hawayatumii, wakati umefika yachukuliwe na serikali na wapewe wananchi
wengine kwa shughuli za kilimo na maendeleo mengine,” alipendekeza
sheha Mumeangu.
Aidha
wameishauri Serikali kuanzisha majengo ya ghorofa na tabia ya kuuziwa
ardhi wageni ama kukodishwa kwa miaka mingi iachwe na wamependekeza
kipindi cha kukodishwa ardhi kisizidi miaka 20.
Mratibu
wa mradi wa SMOLE Saleh Kombo amewaeleza viongozi wa Wilaya hizo mbili
kwamba serikali kwa kushirikiana na serikali ya Finland imo katika
mchakato wa kutayarisha Sera rasmi ya ardhi katika kusimamia ardhi
ndogo iliyopo ikiwa ni juhudi za kupunguza umaskini kupitia MKUZA
awamu ya pili na amewashauri kushiriki kikamilifu katika mchakato huo.
Amesema
Serikali imechukua uwamuzi huo kwa kujua kuwa ardhi ni rasilimali
kubwa katika nchi na ardhi ya Zanzibar imekuwa ikipungua kwa kasi
kutokana na mmongonyoko wa fukwe wakati idadi ya watu imekuwa
ikiongezeka kwa kasi.
Post a Comment