Tume ya Mabadiliko ya Katiba jana ilizindua rasimu ya Katiba
Mpya inayopendekeza kuwapo kwa mabadiliko makubwa kwenye mfumo wa
utawala, yakiwamo ya kuwa na Serikali Tatu; Shirikisho la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Serikali ya Tanzania Bara na Serikali ya Zanzibar.
Mabadiliko mengine yaliyosheheni kwenye rasimu
hiyo ni kufutwa kwa viti maalumu vya ubunge, suala la maadili ya
viongozi wa taifa, umri wa urais kubaki kama ulivyokuwa na kuruhusiwa
kwa wagombea binafsi katika ngazi zote; urais, ubunge, udiwani mpaka
ngazi za mitaa.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mwenyekiti wa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba alisema Tume pia
imependekeza kuingizwa kwenye Katiba Mpya mambo kadhaa kama Tunu, Dira
na Misingi ya Taifa.
“Tulitaka kuifanya rasimu hii iwe fupi kadri
iwezekanavyo, lakini kutokana na wingi wa maoni tumeifanya iwe na Ibara
240. Katiba ya sasa ina Ibara 152,” alisema Jaji Warioba na kuongeza:
“Tumeendelea kuitambua misingi mikuu minne ya
taifa ambayo ni Uhuru, Haki, Udugu na Amani. Lakini pia tukaongeza
misingi mingine mitatu ambayo ni Usawa, Umoja na Mshikamano.
Tumependekeza Katiba yetu mpya iwe na misingi saba.”
Jaji Warioba alisema Tume pia imetambua mambo
kadhaa kuwa ni Tunu za Taifa: “Tunu ya kwanza ni Utu. Tunaamini kuwa
watu wote ni sawa, tusiwe na ubaguzi wala tofauti zozote. Tunu nyingine
ni Uzalendo, Uadilifu, Umoja, Uwazi Uwajibikaji na Lugha ya Kiswahili.”
Jaji Warioba alisema pia kuwa Tume imebainisha
malengo ya Taifa ambayo yatakuwa mwongozo wa Mihimili ya Dola; Serikali,
Bunge na Mahakama.
“Malengo hayo yatakuwa ya aina mbalimbali. Kuna
malengo ya kisiasa, kiuchumi, kimazingira na mengine mengi
yatakayofafanuliwa baadaye,” alisema.
Jaji Warioba alisema Tume pia imependekeza Katiba ijayo ionyeshe wazi maadili ya kijamii, kiutawala na kiuongozi.
“Tumependekeza kuwapo maadili ya viongozi, miiko
na kiundwe chombo cha kusimamia maadili. Tunapendekeza sekretarieti ya
maadili ya viongozi iliyopo, iwe tume kamili,” alisema.
MWANANCHI
Post a Comment