Ofisa
wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Hamidu Mwambugu akimpima uzito na
urefu mmoja wa washiriki wa Redds Miss Kanda ya Mashariki waliofika
bandani hapo kujua afya zao.
………………………………………………………………………..
Na Mwandishi Wetu, Morogoro
WANANCHI mkoani Morogoro wakiwemo
washiriki wa Redds Miss Kanda ya Mashariki 2013 wamejitokeza kupima afya
zao katika banda la Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), upimaji
unaoendelea katika maadhimisho ya Serikali za Mitaa mjini hapo.
Mbali na wananchi hao kujitokeza
pia wameupongeza Mfuko kwa jitihada zake mbalimbali za kuhakikisha
Watanzania wanakuwa na uhakika wa kupata matibabu wakati wowote kwa
kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na Mfuko wa Afya ya Jamii.
NHIF imekuwa na utaratibu wa
kupima afya za wananchi katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kuwasaidia
wananchi hao kufahamu mapema afya zao kutokana na kuwepo kwa ongezeko
la magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari, shinikizo la damu na mengine
mengi.
Wakizungumza na mwandishi wa
habari hii mara baada ya kupata huduma ya upimaji bure bandani hapo,
Ester Albert alisema kuwa “zoezi hili linaloendeshwa na Mfuko ni zuri
kwani linatusaidia sana sisi wananchi kujifahamu matatizo tuliyonayo
yakiwemo ya uzito kupita kiasi hivyo ni vyema wananchi tukaitumia vyema
fursa hii,” alisema.
Wananchi wanaopata fursa ya kupima
afya zao, watapata pia ushauri kutoka kwa wataalam waliopo bandani hapo
kulingana na majibu ya vipimo vyao ili waweze kujikinga na maradhi hayo
ambayo kwa sasa yanaongezeka kila kukicha.
Kwa upande wake Meneja wa NHIF,
Mkoa wa Morogoro, Rose Ongara aliwataka wananchi mkoani hapo kujitokeza
kwa wingi katika Uwanja wa Jamhuri ili kutumia fursa hiyo kufahamu afya
zao kwa kuwa upimaji huo ni bure kwa Mwananchi yoyote.
Alisema kuwa zoezi hilo
litahitimishwa siku ya Jumatatu Julai Mosi, 2013 hivyo wajitokeze kwa
wingi kuunga mkono juhudu za Mfuko na lengo lake la Afya bora kwa wote
Post a Comment