Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimepuuza kauli ya Mwenyekiti wa Tume ya Katiba Mpya, Jaji Joseph Warioba, ya kuwataka wasikusanye maoni ya wananchi na kusema kuwa kitaendelea kufanya hivyo kwa kuwa hakuna sheria wala kanuni iliyokiukwa na chama hicho.
Akizungumza na wananchi wa Wilaya mpya Kakonko Jimbo la Buyungu mkoani Kigoma, Mkurugenzi wa Habari wa chama hicho, John Mnyika, alisema kauli ya Warioba inakinzana na muongozo wa mabaraza ya asasi ambao yeye mwenyewe aliusaini.
“Kauli ya Warioba ina mwelekeo wa kukiuka kifungu cha 18(6) cha Sheria ya Katiba, ambacho kinatamka bayana kwamba, asasi, watu wenye malengo yanayofanana na taasisi, kama Chadema zinaweza kukusanya maoni ya wanachama wao. Chadema inaendesha mabaraza yake ya katiba kwa mujibu wa sheria.
Chadema iliandika barua Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Julai 8, mwaka huu na 10 Julai, Tume ilijibu kuitambua Chadema kuwa taasisi yenye kuweza kukusanya maoni,” alisema Mnyika.
Aliongeza kuwa chama hicho kina wanachama wengi nchi nzima na muongozo wa kuhusu mabaraza ya asasi, taasisi na makundi ya watu wenye malengo yanayofanana uliotolewa na Tume na kusainiwa na yeye mwenyewe Warioba kama Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Alisema mwongozo huo umeruhusu asasi, taasisi na makundi ya watu wenye malengo yanayofanana ambazo zina mfumo wa kiuendeshaji kuanzia ngazi ya chini hadi taifa, kukusanya maoni kuanzia ngazi hizo na kuyawasilisha tume, kupitia ngazi ya taifa.
“Warioba ametoa kauli hiyo baada ya Chadema kukutana na wanachama na wapenzi wake na kuonekana kuna wananchi wengi ambao hawakufikiwa na Tume kutoa maoni yao,” alisema.
Mpaka sasa chama hicho kimefanya mikutano ya Mabaraza ya Katiba katika mikoa ya Mara, Simiyu, Mwanza, Geita, Kagera, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Tanga na Singida.
“Mikutano hiyo tunaifanya kwa kufuata taratibu halali za kisheria. Hivyo kauli ya Warioba imekiuka hata mwongozo aliousaini yeye mwenyewe, Chadema tunavyofanya…kukusanya maoni ya wanachama wetu ili hatimaye tuyawasilishe.
Sisi tunaendeshwa na falsafa ya nguvu ya umma, tuna umma mkubwa nyuma yetu, hatuwezi kukutana kwenye ukumbi pekee kama wanavyofanya CCM na taasisi nyingine. Tumeweka utaratibu wa kufanya mikutano na mikusanyiko, kupitia Rasimu ya Katiba Mpya, watu kukusanya maoni juu ya rasimu hiyo,” alisema Mnyika.
Hivi karibuni, Jaji Warioba wakati akifunga mjadala wa siku mbili wa Rasimu ya Katiba, uliofanywa na Baraza la Katiba la Wabunge Wanawake, alikemea vyama vya siasa kupenyeza maoni yao katika Mabaraza ya Katiba.
“Nazungumza wazi hapa leo, vyama vya siasa ni taasisi, vifuate utaratibu vijadili kama Baraza la katiba la Taasisi na kutuwasilishia maoni yao, sisi Tume hatutachukua maoni ya jukwaani wala ya kwenye helikopta,” alikaririwa Jaji Warioba akisema.
“Ukiangalia kwenye Katiba hii, utaona kuwa wananchi wanataka dira ya Taifa, dira ya uchumi, kisiasa na kijamii, lakini cha kushangaza mambo yanayozungumzwa ni machache tu ya madaraka, sasa haya mengine yataboreshwaje?,”alihoji.
Alitaka wanasiasa wasitafute mchawi katika mvutano na mjadala unaoendelea wa kipengele cha Rasimu ya Katiba kinachopendekeza serikali tatu, kwa kuwa kimetokana na maoni ya wananchi na si ya Tume.
Post a Comment