Mke wa Rais Mama Salma Kikwete ametunukiwa tuzo ya kimataifa ya
jitihada za kuendeleza rasilimali watu katika taifa kwa mwaka 2012 na
Taasisi ya Bright Entertainment Network (BEN) ya nchini Uingereza.
Tuzo
hizo pamoja na cheti amekabidhiwa leo na Waziri wa Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara katika ofisi za Taasisi ya
Wanawake na Maendeleo (WAMA) zilizopo Ikulu jijini Dar es Salaam.
Waziri
Dk. Mukangara alikabidhiwa tuzo hiyo na Taasisi ya BEN mwezi wa sita
mwaka huu alipokuwa nchini Uingereza kwa shughuli za kikazi ili
aifikishe kwa Mama Kikwete.
Dk. Mukangara alisema
kuwa tuzo hiyo ambayo inafahamika kwa jina la “Country Human
Development – 2012 Award” inatolewa kwa mshindi anayeteuliwa na Taasisi
ya BEN ikiwa ni miongoni mwa waliowania kutoka nchi za Bara la Afrika ,
Carribbia, Asia na Pasifiki.
“Ushindi
huu wa kimataifa Mama Kikwete umeupata kutokana na juhudi na harakati
zako za kuwainua kimaendeleo wananchi wa matabaka mbalimbali hapa nchini
hasa wasichana na kina mama kupitia Taasisi uliyoiasisi na kuendelea
kuiendesha ya WAMA.
Sote
tunakubalina kutokana na kazi tunazozishuhudia ambazo Taasisi yako
chini ya uongozi wako inazifanya, hakika umestahili kutunukiwa tuzo hii
ya jitihada za kuendeleza rasilimali watu katika taifa hongera sana”, alisema Waziri Dk. Mukangara.
Kwa
upande wake Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa WAMA alimshukuru
waziri Dk. Mukangara kwa kuchukua dhamana ya kupokea tuzo hiyo na
kuifikisha kwake pia aliishukuru Taasisi ya BEN kwa kuona umuhimu wa
kazi anazozifanya na kumchagua kuwa mmoja wa washindi wa tuzo hiyo kwa
mwaka 2012 kwani watu walioshiriki ni wengi kutoka ndani na n je ya bara
la Afrika.
“Ninashukuru
sana kwa tuzo hii niliyoipata ambayo inazidi kunipa moyo na ninaahidi
nitaendelea kufanya kazi kwa kujituma kadri Mwenyezi Mungu
atakavyoniwezesha na sintarudi nyuma kuwasaidia watanzania eti kwa kuwa
nimepata tuzo kwani sikutegemea kuwa ipo siku nitapata tuzo kutokana na kazi ninazozifanya za kuisaidia jamii”.
Hii tuzo ni kwa ajili ya watanzania
wote na wafanyakazi wa taasisi ya WAMA kwani bila ya watanzania
nisingeweza kupata tuzo kama hii”, alisema Mama Kikwete.
Mwenyekiti
huyo wa WAMA alisema taasisi zote za maendeleo zitaendelea kufanya kazi
kwa bidii ili ziweze kutimiza malengo ya Maendeleo ya Milinia kwa
wakati uliokusudiwa.
Kazi
zinazofanywa na Taasisi ya WAMA zilizopelekea Mwenyekiti wa Taasisi
hiyo kupewa tuzo ni uraghibishi wa kuboresha hali ya maisha kwa watoto,
wasichana na wanawake hasa kwa upande wa afya, elimu na uchumi na
kuwasaidia mitaji kinamama wajasiriamali.
Zingine ni kupambana na mimba za utotoni hasa kwa wanafunzi wa shule za msingi na Sekondari na kuendesha mapambano
dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi kwa kina mama, hususani
kupunguza maambukiziya Virusi vya Ukimwi (VVU) kutoka kwa mama kwenda
kwa mtoto.
Post a Comment