Kaimu Mkurugenzi
Mkuu wa Bohari ya Dawa(MSD) Bw. Isaya Mzoro(kushoto) akieleza kwa
vyombo vya habari kuhusu utendaji na mipango wa bohari hiyo katika
mkutano uliofanyika ukumbi wa Idara ya Habari leo Jijini Dar es
salaam,kulia ni Murugenzi Msaidizi Idara ya Habari Bi Zamaradi
Kawawa.(Picha na Hassan Silayo- Maelezo)
……………………………………………………………………………….
Bohari ya Dawa (MSD) ni mojawapo
ya Idara chini ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, inayojiendesha
chini ya Bodi ya Wadhamini iliyoundwa kwa mujibu wa sheria namba 13 ya
mwaka 1993.
Bohari ya Dawa yenye makao yake
makuu mjini DSM, eneo la Keko Mwanga, Barabara ya Nyerere ina jumla ya
kanda tisa katika mikoa ya Mwanza, Tabora, Mbeya, Iringa, Dodoma Tanga,
Moshi, Mtwara na Dar Es Salaam
- MAJUKUMU YA MSD
Majukumu ya msingi ya Bohari ya
Dawa yako matatu, ambayo ni Kununua, Kuhifadhi na Kusambaza dawa,
vifaa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara kwenye hospitali, vituo
vya afya, zahanati za umma, na taasisi zilizoidhinishwa na Wizara ya
Afya na Ustawi wa Jamii.
- UTENDAJI
Utendaji wa MSD unaongozwa na Sera
ya Afya ya mwaka 2007 na Mpango Mkakati wa Kati wa miaka Mitano ( 2007
-2013). Lengo kuu la mpango mkakati huu ni kuboresha upatikanaji wa
dawa na vifaa tiba kwenye mnyororo mzima wa ugavi nchini.
- UPATIKANAJI WA DAWA
Upatikanaji wa dawa kwa Bohari ya
Dawa umekuwa unaongezeka (kulingana na bajeti ya serikali) mwaka hadi
mwaka.Tafiti zilizofanywa mwaka 2010-2011 na wadau mbali mbali (wakiwemo
GIZ na USAID) zimeonyesha kuwa hali ya upatikanaji wa dawa katika
hospitali za umma umeongezeka na kufikia kati ya asilimia 70 hadi 75.
Bohari hununua dawa, vifaa tiba na
vitendanishi vya maabara kwa ajili ya vituo vya kutolea huduma ya afya
kutoka vyanzo mbalimbali ndani na nje ya nchi. Hata hivyo asilimia 80
ya dawa huagizwa kutoka nje ya nchi huku asilimia 95 ya vifaa tiba
huagizwa kutoka nje ya nchi. Vitendanishi vya maabara kwa asilimia 100
huagizwa kutoka nje ya nchi.
Bohari ya Dawa hununua dawa na
vifaa tiba kwa kuzingatia miongozo ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Miongozo hiyo pamoja na mambo mengine inaelekeza kuwa Dawa, Vifaa na
Vifaa Tiba vyote lazima visajiliwe TFDA na PHLB kabla ya kuagizwa na
kusambazwa. Dawa, Vifaa na Vifaa Tiba hukaguliwa na wakala hizo. Aidha
ubora wake hupimwa na kukaguliwa kwa ushirikiano wa taasisi za serikali
kama vile TBS, GCLA na BICO(UDSM)
Bohari ya Dawa pia hununua dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara kwa kuzingatia sheria ya Manunuzi ya Umma.
- UHIFADHI
Mahitaji halisi ya maghala kwa MSD
ni mita za mraba 60,000. Katika kipindi cha nyuma MSD ilikuwa na
maghala yenye uwezo wa mita za mraba 20,845 ambayo ilikuwa inayamiliki
yenyewe na maghala ya kukodi yenye ukubwa wa mita za mraba 24,443.
Kwa sasa maghala mapya ya kisasa
yenye ukubwa wa mita za mraba 10,000 ambayo yamejengwa kwa msaada wa
pamoja kati ya Shirika la misaada la Kimataifa la serikali ya Marekani
(USAID) na Mfuko wa Kimataifa wa Kupambana na UKIMWI, Malaria na Kifua
Kikuu (GFATM)pamoja na Global Fund yamekamilika katika kanda za Dar es
Salaam, Dodoma na Mbeya. Mwishoni mwa mwaka jana ghala la Keko
lilizinduliwa, mwaka huu mwezi Mei ghala la Dodoma lilizinduliwa na
Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Ujenzi wa maghala mengine ya
kisasa yenye ukubwa wa mita za mraba 8,000 unaendelea katika kanda za
Tabora na Tanga na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu (
Agosti, 2013).
- USAMBAZAJI DAWA NA VIFAA TIBA
Tangu mwaka 2010
MSD imekuwa ikipeleka dawa moja kwa moja hadi katika hospitali, vituo
vya afya na zahanati kwa mikoa Kumi. Hatua hii ilitokana na maagizo ya
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, katika jaribio la kwanza la kupeleka
dawa na vifaa tiba moja kwa moja hadi vituo vya kutolea huduma za tiba
katika kanda ya Tanga.
Jaribio hilo
lilifanikiwa kwa kiasi kikubwa ambapo mnamo mwaka 2011/2012 mikoa
mingine tisa ikaingizwa katika utaratibu wa kufikisha Dawa na Vifaa Tiba
moja kwa moja hadi hospitali, vituo vya Afya na zahanati. Mikoa hiyo ni
pamoja na Shinyanga, Lindi, Dodoma, Kigoma, Manyara, Dar es salaam,
Rukwa, Pwani na Ruvuma
Katika mwaka huu
wa fedha MSD inaendeleza mpango huo wa kupeleka dawa moja kwa moja hadi
vituo vya kutolea huduma za afya katika mikoa mikoa 15 iliyokuwa
imebaki.
- MABORESHO
- Bohari ya Dawa kwa kushirikiana na wahisani ina mpango wa kupanua maghala kwa kukamilisha ujenzi wa awamu ya pili ili kuongeza nafasi za kuhifadhia Dawa na Vifaa Tiba. Tayari maghala ya kisasa yaliyokamilika yameanza shughuli za kuhidadhi Dawa na Vifaa tiba.
- MSD inatumia mfumo wa EPICOR 9 tangu mwezi Agosti, 2012. Wafanyakazi katika ngazi zote wanapatiwa mafunzo endelevu katika utoaji huduma kwa haraka na ufanisi.
- Kuongea na Taasisi shiriki katika Mnyororo wa ugavi(TFDA & TBS na TRA) ili kupunguza muda wa kugomboa bidhaa
- CHANGAMOTO
- Ongezeko kubwa la Mahitaji kulinganisha na uwezo wa Serikali.
- Ucheleweshaji wa kufikishwa pesa MSD kutoka Hazina.
- Halmashauri kutokutumia vyanzo vingine vya fedha (NHIF, CHF, Basket Fund, Cost Sharing) kununua dawa na kutegemea fedha za Serikali kuu(kupitia MSD) tu.
- Uhaba wa viwanda vya dawa nchini
- Taratibu za ununuzi kuchukua muda mrefu (miezi 6 – 9). (Ununuzi wa dawa unafuata taratibu zinazotakiwa kufuatwa na bidhaa nyingine za kawaida, hazina utofauti wa taratibu wala kipaumbele)
- Baadhi ya Zahanati na Vituo vya Afya kutoleta Maombi ya Dawa na vifaa tiba katika Kanda za MSD (Kama utaratibu unavyoelekeza)
- MATARAJIO
- Kushirikisha sekta binafsi katika kusambaza dawa na vifaa tiba.
- Kubandika orodha ya dawa na vifaa tiba vilivyokabidhiwa kituoni mara tu baada ya kukabidhi.
- Kuendelea kuweka nembo ya GOT kwenye vidonge ili kuzitambua dawa ambazo ni mali ya umma.
- Kushirikisha sekta binafsi katika kutoa huduma ya dawa na vifaa tiba wakati MSD haina bidhaa hizo kwenye maghala yake.
- Kuendelea kuwahimiza waganga wafawidhi wa vituo vya kutolea huduma kutayarisha na kuleta Maombi ya Dawa na Vifaa Tiba kwa wakati uliopangwa.
Isaya Mzoro
Post a Comment