VPL KUANZA KUTIMUA VUMBI JUMAMOSI
Michuano
ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu wa 2013/2014 inaanza kutimua vumbi
kesho (Agosti 24 mwaka huu) katika viwanja saba tofauti huku mabingwa
watetezi Yanga wakianza kutetea ubingwa wao kwa kuikaribisha Ashanti
United kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Uwanja
wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro utakuwa mwenyeji wa mechi
kati ya Azam ya Dar es Salaam na wenyeji Mtibwa Sugar. Oljoro JKT
itaikaribisha Coastal Union kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta
Amri Abeid jijini Arusha.
Mgambo
Shooting itaoneshana kazi na JKT Ruvu ambayo hivi sasa iko chini ya
Kocha Mbwana Makata. Mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga
wakati Rhino Rangers itakwaruzana na Simba katika Uwanja wa Ali Hassan
Mwinyi mjini Tabora.
Mbeya
City iliyopanda VPL msimu huu itapimana ubavu na Kagera Sugar kwenye
Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya huku Ruvu Shooting
ikiialika Mabatini, Mlandizi timu ya Tanzania Prisons kutoka Mbeya.
Mzunguko
wa pili wa ligi hiyo utachezwa Agosti 28 mwaka huu. Baada ya hapo ligi
itasimama kupitisha mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya Gambia na
Tanzania (Taifa Stars) itakayochezwa Septemba 7 mwaka huu jijini Banjul.
VPL itaingia mzunguko wa tatu Septemba 14 mwaka huu.
TIKETI ZA ELEKTRONIKI KUANZA MZUNGUKO WA NNE
Tiketi
za elektroniki zitaanza kutumika katika mzunguko wa nne wa Ligi Kuu ya
Vodacom (VPL) utakaoanza Septemba 18 mwaka huu. Tayari benki ya CRDB
ambayo ndiyo ilishinda tenda hiyo imeshakamilisha ufungaji wa vifaa kwa
ajili ya matumizi ya tiketi hizo katika viwanja vyote.
Hivi
sasa Serikali ambayo ndiyo inamiliki Uwanja wa Taifa, Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) pamoja na CRDB zinashughulikia mfumo wa
tiketi hizo kwenye uwanja huo ambao ndiyo ulikuwa haujakamilika kwa
matumizi katika upande huo.
Mfumo
(system) iliyoko kwenye uwanja huo inapishana na ule utakaotumiwa na
CRDB, hivyo pande husika zinashughulikia suala hilo ili mifumo hiyo
iweze kuingilia.
Pia
mashine za kuchapia (printer) kwa ajili ya tiketi ambazo CRDB
wameziagiza kutoka nje ya nchi zinatarajiwa kuwasili mwishoni mwa mwezi
huu.
Hivi
sasa CRDB inashughulikia ufungaji wa vifaa vya matumizi ya tiketi za
elektroniki iwemo turnstiles kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi ambao
mwanzoni hakuwemo kwenye mpango huo kutokana na Mkoa wa Tabora kutokuwa
na timu ya Ligi Kuu.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Post a Comment