DK. SLAA |
DK. MWAKYEMBE |
*********
WAZIRI wa Uchukuzi na Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, ametuhumiwa kuhusika na vitendo vya kifisadi, kinyume kabisa na msimamo wake kabla hajapewa uwaziri.
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dk. Willibrod Slaa, ndiye aliyerusha tuhuma hizo juzi mjini hapa alipokuwa akihutubia mamia ya wakazi wa wilaya hii katika mkutano wa hadhara.
Dk. Slaa aliwaeleza wana Kyela Dk. Mwakyembe ambaye awali alionyesha umakini katika uchapaji kazi, amebadilika mara tu baada ya kupewa uwaziri na kujiingiza katika vitendo vya kifisadi, ikiwemo hatua yake ya kugawa eneo la wazi kwa Shirika la Sukita ambalo liko chini ya CCM kinyume na taratibu.
Katibu huyo aliyeongozana na Mbuge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Sugu), mbunge wa Mbozi Magharibi, David Silinde, na viongozi wengine waandamizi alisema Dk. Mwakyembe mbali na utoaji wa zabuni hiyo kwa Sukita pia anazo tuhuma zingine zaidi ya sita za vitendo vya ufisadi vinavyodaiwa kufanywa na Mwakyembe na kwamba anajiandaa kuziweka hadharani.
“Ndugu wananchi najisikia furaha jinsi mlivyojaa katika uwanja huu na hii inanidhihirishia mmechoka na vitendo vya kifisadi vinavyofanywa na mbunge wenu pamoja na chama chake.
“Sisi kama wapinzani tunasikitika hasa pale alivyosema atawataja kwa majina wauza unga, lakini hadi leo hajawataja kwa hali hiyo inaonyesha wazi kuwa kiongozi huyo ni mbabaishaji,” alisema Dk. Slaa.
Pamoja na hayo aliwataka wananchi wa Kyela waungane na wananchi wengine nchini kuunga mkono jitihada za umoja wa vyama vya CHADEMA, NCCR Mageuzi na CUF ambao wameamua kuunganisha nguvu zao kwa pamoja kuhakikisha katiba inapatikana bila ya uchakachuaji, ili itumike kwa maslahi ya watanzania na si kwa maslahi ya wachache.
Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, aliwataka wananchi wa Kyela kuwaunga mkono kwa jitihada wanazozifanya bungeni kwani wameamua kufanya hivyo kwa maslahi ya taifa na hawatarudi nyuma mpaka kieleweke.
TANZANIA DAIMA
Post a Comment