JAMHURI YA MUUNGANO
WA TANZANIA
WIZARA
YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
|
|
|
Simu: +255-22-2112035/40
|
S.L.P. 9223
|
|
Nukushi: +255-2122617/2120486
Barua Pepe: ps@moha.go.tz
|
Dar es Salaam
Septemba
19,2013
|
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
UFAFANUZI KUHUSU TUHUMA
DHIDI YA WATENDAJI WA OPERESHENI KIMBUNGA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mheshimiwa Jakaya
Mrisho Kikwete Julai 29, 2013 aliagiza kufanyika kwa opereheni maalum ya
kuondoa uhalifu katika mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita mbao kwa kiasi kikubwa
umechangiwa na kuwepo kwa wahamiaji haramu kutoka nchi jirani.
Operesheni Kimbunga inayoongozwa na Brigedia Jenerali Mathew
Sukambi imeanza rasmi Septemba 6, 2013 baada ya kutoa muda wawiki mbili kwa
wahamiaji wanaoishi nchini bila kufuata sheria kuondoka kwa hiari yao au
kuhalalisha ukaazi wao nchini.
Wakati Operesheni hii ikifikia katika Wiki yake ya Pili,
Serikali kupitia kiongozi wa Operesheni Brigedia Jenerali Mathew Sukambi
inawapongeza watendaji wote wa operesheni hii kwa kazi nzuri waliyoifanya kwa
unyenyekevu na kiuzalendo kuhakikisha kuwa zoezi la kuondoa uhalifu na kukamata
wahamiaji haramu linafanyika kwa nidhamu ya hali ya juu na mafanikio.
Aidha, kumekuwepo na tuhuma mbali mbali zinazotolewa kupitia
Vyombo vya Habari ambazo hazina ukweli.
Tuhuma za rushwa dhidi
ya watendaji wa Operesheni Kimbunga
Operesheni Kimbunga inahusisha watendaji kutoka vyombo mbali
mbali nchini vikiwemo Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Idara ya Uhamiaji,
Jeshi la Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na rushwa (TAKUKURU), Idara ya
Usalama wa Taifa, Idara ya wanyamapori na taasisi nyingine za serikali.
Mazingira ya kazi ya kuwakamata wahamiaji haramu na kuwahoji
ili kuthibitisha uraia wao ni ya wazi
hayawezi kuruhusu watendaji kuweza kupokea rushwa kama ilivyoripotiwa na Gazeti
moja hapa nchini kwani kwa kufanya hivyo ni ukiukwaji wa sheria.
Hata hivyo, wananchi wanapaswa kufahamu kuwa iwapo kuna
mtendaji wa operesheni hii ameomba na kupokea rushwa wanakiuka sheria, hivyo ni
vyema kama kuna mtu mwenye ushahidi wowote atoe taarifa kwenye ofisi za
TAKUKURU zilizopo mikoani na Wilaya zote nchini.
Zoezi la Operesheni
Kimbunga halilengi kunyanyasa wazee, watoto na wanawake wasio Raia walioolewa
na Watanzania
Operesheni Kimbunga haikulenga kuwanyanyasa Wazee, Wanawake
walioolewa na watoto wao wadogo wanaoishi nchini bila kufuata Sheria ya
uhamiaji.
Kuna waliokuwa
Wakimbizi 36,000 kutoka nchi ya Rwanda walioingia nchini miaka ya 1959 hadi
1961 waliokuwa wakiishi katika mkoa wa Kagera katika maeneo ya Kimuli, Nkwenda,
Mwase na maeneo mengine ambao walipewa uraia wa Tanzania kwa tajinisi mwaka
1983 isipokuwa watoto wao kwa kuwa wazazi wao hawakuwaombea uraia huo. Raia hao 36,000 waliopewa uraia wa tajinisi
hawakuguswa na operesheni hii kwani ni watanzania isipokuwa watoto wao ambao
hawakuombewa uraia na wanaishi nchini bila hadhi yeyote ya kiuhamiaji.
Pia kuna raia wa kigeni waliokuwa wanaishi bila kufuata
sheria za uhamiaji na Uraia ambao zamani walikuwa wakimbizi lakini hadhi ya
ukimbizi iliondolewa baada ya nchi zao kuwa salama na kutakiwa kurudi.
Hata hivyo, kama mheshimiwa Rais, Jakaya Mrisho Kikwete
alivyoagiza kuwa zoezi lifanyike likiwa na sura ya kibinaadam pale inapobidi,
raia hao wa kigeni waliokuwa wanaishi nchini bila kufuata sheria hususan wazee
wameruhusiwa kubaki na kusaidiwa kufuata taratibu ili kuhalalisha ukaazi wao.
Aidha, ieleweke kuwa kuzaliwa Tanzania pekee hakumpi mtu haki ya kuwa Raia moja kwa moja
mpaka taratibu nyingine zifuatwe. Kuna
watoto walizaliwa Tanzania na Raia wa nchi za nje waliokuwa wanaishi nchini
kabla ya kupatiwa uraia. Hao hawawezi kuwa raia moja kwa moja mpaka taratibu za
kisheria zifuatwe.
Aidha, Operesheni Kimbunga haikulenga kuvunja ndoa na
kusambaratisha familia. Lengo ni kuondoa
wahamiaji haramu.
Wanawake walioolewa na Watanzania wametakiwa kujiorodhesha
ili kupatiwa utaratibu wa ukaaji wao.
Wanaume walifunga ndoa na Watanzania wanatakiwa kurudi katika nchi zao
na wake na watoto wao na kwa wanaotaka kuishi nchini wanatakiwa kuomba vibali
vya kuishi kwa kufuata sheria na taratibu za uhamiaji.
Taarifa
hii imetolewa na Zamaradi Kawawa, Kiongozi wa Timu ya Habari na Mawasiliano ya
Operesheni Kimbunga, Septemba 20,2013, Biharamulo, Kagera.
Post a Comment