*********
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam.
WASWAHILI
wana msemo wao, siku zote mla ndizi usahau, ila anayetupa maganda ni
ngumu kusahau. Siku zote jambo hilo litakuwa kichwani mwake, akiwaza na
kuwazua.
Huenda
chuki ikawa ndani yake kwa kuangalia tukio hilo, ila yule aliyekula
ndizi si ajabu akawa ameshasahau na kuendelea na maisha yake ya kila
siku.
Nimejikuta
nikianza hivi baada ya kuangalia muungano wa mashaka wa vyama vya
upinzani Tanzania, kama vile Chama Cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Chama Cha Wananchi (CUF) na NCCR-Mageuzi, inayoongozwa na
James Mbatia.
Kabla
sijaenda mbali zaidi, naomba niseme kuwa sina chuki na uamuzi wa
muungano huo kwa wapinzani wala chuki ya viongozi wanaongoza vyama hivyo
vya siasa vyenye hamu siku moja vishike dola.
Kwa
wale wanaofuatilia siasa za Tanzania, watakumbuka jinsi CUF
walivyotukanwa na kudhalilishwa na Chadema, ambao leo wamejirudi na
kuunda muungano. Mara kadhaa CUF waliitwa sehemu ya CCM na kila
walichohitaji kutenda, kilibezwa.
Mengi
yalisemwa likiwamo hilo la CCM B ambapo tulishuhudia sumu hiyo
ikienezwa kwa kasi katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Visiwani
ili CUF ionekane si lolote kwa siasa za nchi hii.
Baada
ya kuona haitoshi, Chadema bado wakaendeleza propaganda kwa wafuasi wao
kwa kusema chama hicho kinachoongozwa na Profesa Ibrahimu Lipumba kuwa
kinaongozwa na siasa za Liberal.
Mbunge
wa Nyamagana, Ezekiel Wenje, kwa kupitia chama hicho kinachoongozwa na
Mwenyekiti wao Freeman Mbowe, alizusha mzozo mkubwa kwa kuwaambia CUF
wana uhusiano na mashoga au wale wanaounga mkono ushoga na ndoa za
jinsia moja ulimwenguni.
Jambo
hilo lilisababisha mvurugano wa aina yake ndani ya Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, kiasi cha kuhofiwa ngumi kuzuka kutoka kwa baadhi
ya wabunge hao.
Kwa
wapenzi wa amani na waumini haswa wa siasa za kistaarabu, kauli ya
Wenje ilikuwa ya kihemko zaidi. Ilikuja kwa nia ya kupata kuandikwa au
kujulikana mtaani.
Kwa
bahati mbaya, kauli hii na nyinginezo zote zilizokuwa zinatolewa kwa
ajili ya kuwadhalilisha watu wa CCM na CUF, ziliishia hewani. Ni pale
leo tunapoona Chadema wanakubali kuungana na CUF.
Je,
Chadema ni lini wameikanusha ndoa ya CUF na CCM? Je, vyama hivi
vinavyodaiwa ni ndugu vimewezaje tena kukubali undugu na Chadema? Ni
ajabu mno.
Wahenga
wanaendelea kusema, ukiwa mchoyo usiwe mroho. Hata hivyo haitoshi,
wakasema tena, ukiwa muongo usiwe msahaulifu. Chadema ni wepesi kusahau
mambo.
Suala
hili litawatafuna hasa kama lengo lao ni kujenga propaganda hata zile
zisizokuwa na mashiko kwao. Hii si haki. Najua Chadema na CUF wana
malengo mazuri kwa ajili ya kuupitia vizuri suala la Rasimu ya Katiba
inayotingisha kwa sasa.
Najua
ndoa ya CCM kama kweli ilikuwapo, Chadema wao wameivunja na kufunga
upya. Lakini ni rahisi kusema muungano wa CUF na Chadema ni mwepesi mno
kuvunjika.
Hawa wote wanasumbuliwa na vita vya urais. Lakini pia sidhani kama kweli ndoa yao itashamiri kwa pande zote za Muungano.
Kwa mfano, Maalim Seif Shariff Hamad na Lipumba watawezaje kudumisha muungano wao kwa kusema kauli moja Visiwani Zanzibar?
Zanzibar
imekuwa ikikiangalia vibaya Chadema na kusema ni chama cha Wakristo na
hakina nafasi katika mioyo yao. Lakini hapo hapo, viongozi wao wanapanda
tena jukwaani kuimba wimbo wa muungano ambao ukiangalia kwa kina
unagundua umejaa utata.
Nasema
haya kwasababu tunajua vyema mwenendo wa wanasiasa wa upinzani wa
Tanzania na vyama vyao. Japo kwa sasa wanajiona wanaimba wimbo mmoja,
lakini kiu ya madaraka kwao, wote wakiutaka kuunda serikali au kambi ya
upinzani vinawasumbua.
Mara
baada ya kuungana, eti wapinzani hao wakatinga katika ofisi za Msajili
wa Vyama, Jaji Godfrey Mutungi, kwa nia ya kueleza dhamira yao ya
kupinga Rais Jakaya Kikwete kuusaini Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba.
Vyama
hivyo vya CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi, vinavyounda ushirikiano wa
kisiasa wa kupinga Rais kusaini muswada huo, vilimfafanulia Msajili huyo
kilichotokea bungeni hivi karibuni, kwa wabunge wa upinzani nje ya
ukumbi wa Bunge, wakati wale wa CCM wakipitisha muswada huo pamoja na
marekebisho yake.
Kinachopiganiwa
kwa sasa na hao wapinzani, ni kumtaka Rais Kikwete asisaini hadi
kufanyika kwa maridhiano ya Kikatiba, huku Lipumba akisimama kama
Mwenyekiti wa ushirikiano huo.
Katika
mvutano huo, Lipumba anasema, “Tumefanya mazungumzo na Msajili,
tulifika kumsabahi na kumweleza yaliyojiri bungeni kuhusu Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba na mchakato ulianzia tume mpaka kura ya maoni ya
katiba, ila Zanzibar haikushirikishwa,” alisema Lipumba.
Kuonyesha
kile walichokuwa wanakihitaji tangu awali, CUF na Chadema wanatangaza
maandamano. Ilikuwa lazima. Ni kawaida kwa maandamano kwa watu hawa.
Wanapohitaji
lao hakuna wa kuwazuia. Na ndio maana tumeshuhudia watu wakipoteza
maisha kutokana na wapinzani, hasa wanaotoka katika Chama cha Chadema
kulazimisha hata pale wanapozuiwa au kushauriwa kwa vuzuri tu na jeshi
la Polisi.
Naomba
nieleweke. Nchi hii ni yetu wote. Tukisema tushiriki kwa pamoja
kuibomoa, maisha yetu yatakuwa mashakani. Watanzania sasa katika nchi za
Bara la Afrika hatuna marafiki wengi.
Hata
wale tuliokuwa na uswahiba nao kama vile Rwanda tumeingia kwenye
uhusiano mbovu. Nchi ya Kenya na Uganda pia hawa si wenzetu. Kama hivyo
ndivyo, tukiibomoa Tanzania, tutaishi maisha ya kutanga tanga na huenda
hawa wenzetu wakashindwa kutupokea.
Kuna
kila sababu ya kuhakikisha nchi hii inaongozwa kwa ushirikiano na
kusikilizana pia. Kila mmoja amuheshimu mwenzake. Hakuna sababu ya
kuitana lugha za kuudhi.
Nitamshangaa
Wenje na wengineo wanapozalisha siasa za chuki na uhasama bila sababu
za msingi. Profesa Lipumba alisema Oktoba 10 mwaka huu ndio siku ya
kitaifa ya kupinga kusainiwa kwa Sheria hiyo na kwamba maandamano
yatakayofanyika yatakuwa ya amani.
Kuna
mengi yanayohitaji kufanywa kwa ajili ya Tanzania inayokumbwa na
matatizo ya kila aina. Kwa bahati mbaya, baadhi yao wanakosa uzalendo na
kiu yao kubwa ni kujiwekea mazingira ya maisha yao.
Mbunge
wa Ubungo kwa kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John
Mnyika yeye anasema kuwa ushirika wao utatumia njia za kidemokrasia
kushinikiza Rais asisaini Sheria hiyo.
“Tutatumia
njia za kidiplomasia kupinga na kuwaandaa wananchi kwa kutumia njia
hizo, kwani jambo hili limekuja kwa muda muafaka kutokana na kauli
zilizotolewa na viongozi wa masuala hayo, Jaji Joseph Warioba na Waziri
wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe,” alisema Mnyika, ikiwa ni ishara
ya kuutumikia muungano wao.
Muungano
ambao bado una mashaka, ukizingatia kuwa wanasiasa wetu mara kadhaa
wanachofanya wao ni kujiwekea mazingira ya kunufaika wenyewe.
Kwanza
wenyewe siku zote hawapendani. Kinachofanywa kwa sasa ni kuzuga tu na
ndio maana katika muungano huo bado kuna vyama ambavyo
havijashirikishwa.
Chama
kama NRA hiki licha ya kuwa na muda mrefu tangu kuasisiwa kwake, lakini
muungano huo hawajashiriki, hivyo utashangaa wapinzani hawa
wanazungumza ushirikiano upi wakati mara kwa mara wamezoea kutengana?
Nadhani
huu ni wakati sasa wa kuangalia namna gani tunafanya siasa zenye
kujenga jamii bora. Wapinzani kwa kupitia muungano huu wenye utata kwa
CUF, Chadema na NCCR Mageuzi wanapaswa kufahamu umuhimu wa mchakato huo.
Hatuhitaji
malalamiko yasiyokuwa na mashiko. Ni mara kadhaa wapinzani hasa Chadema
wamekuwa wakilalamika lakini mwisho wa siku wanaacha kama ilivyo.
Mbaya
zaidi, wakati mwingine ili wajionyeshe wao ni wenye huruma na
Watanzania hufikia kutoka katika wakati mgumu, kama ule wa Bajeti ambayo
matokeo yake hadi leo yanawatoa watu machozi.
Huu
ni wakati wa kuangalia siasa zenye kujenga nchi na sio kubomoa, huku
wanasiasa hao wakiacha hoja za mizaha kwa ajili ya kulinda majina yao
bila sababu za msingi.
Mengi
yanaweza kuja na kuondoka, lakini kumbukumbu mbaya za upinzani
zitaendelea kuumiza kichwa hasa pale hoja nyepesi kuwa CUF wapo chini ya
CCM.
Hata
hivyo haitoshi, wakasimangwa tena kwa kuambiwa wana urafiki na chama
kinachounga mkono ushoga, ingawa leo hoja hizo zimetiwa kapuni kwa zuga
ya muungano usiokuwa na kichwa wala miguu.
Mwisho
kabisa ni wakati wa vyama vya upinzani kuwa makini katika kujadili
mambo ya Katiba ili waiache serikali na wale waliopewa jukumu hilo
watupikie Katiba yetu kwa ajili ya Watanzania wote.
Hii
ni kwasababu makundi yote yamefanikiwa kutoa maoni yao, wakiwamo
wanasiasa na vyama vyao vya siasa, hivyo chokochoko zao hazina mashiko
na zinaweza kuibua mtafaruku usiokuwa na kichwa wala miguu.
Post a Comment