JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA WAZIRI MKUU
SERIKALI ya Tanzania
imeasaini mikataba ya makubaliano (MoUs) mitano ambayo itasadia kutoa fursa za
biashara, mafunzo na masuala ya sayansi na teknolojia kwa Watanzania.
Mikataba hiyo imetiwa saini jana jioni (Alhamisi, Oktoba 17, 2013) mbele ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda
na Waziri Mkuu wa China, Mhe. Li Keqiang mara baada ya viongozi hao kufanya
mazungumzo rasmi ya Kiserikali jijini Beijing, China.
Mikataba hiyo ni Mkataba wa
Ushirikiano baina ya Tanzania na China kwenye masuala ya Sayansi na Teknolojia;
Mkataba wa Kuruhusu bidhaa za baharini ziweze kuuzwa China; Mkataba wa
Ushirikiano baina ya Tanzania na China kwenye masuala ya Utalii. Mingine ni
Mkataba wa Makubaliano baina ya Tanzania na China wa kuanzisha Ukanda wa Kisasa
wa viwanda vya nguo pamoja na kukuza zao la pamba na wa mwisho ni mkataba wa
kutoa vitalu namba 60 na 61 kwa ajili ya ujenzi wa ubalozi wa China jijini Dar
es Salaam.
Katika mazungumzo yao,
Waziri Mkuu ambaye yuko katika siku ya pili ya ziara ya kikazi yake ya siku
tisa kwa mwaliko wa Serikali ya nchi hiyo, alimweleza Waziri Mkuu wa China
kwamba anaishukuru Seriklai ya nchi hiyo kwa misaada mbalimbali ambayo China
imekuwa ikiitoa kwa Tanzania.
“Tunaishukuru kwa misaada
mbalimbali na mikopo ambayo imekuwa ikitolewa kwa masharti nafuu ikilinganishwa
na mikopo ya kibiashara ambayo hutolewa na nchi nyingine na kawaida ina gharama
kubwa kwa Taifa,” alisema Waziri Mkuu wakati akizungumza na waandishi wa habari
mara baada ya kumaliza mazungumzo na mwenyeji wake.
Alisema alitumia fursa hiyo
kusisitiza uwekezaji kwenye sekta za kilimo, nishati, elimu na miundombinu hasa
reli, bandari na teknohama. Kwenye kilimo, Waziri Mkuu alikumbusha suala la
upatikanani wa soko kwa zao la tumbaku lakini akaomba uwepo umuhimu wa pekee
kwa wawekezaji wa viwanda vya kusindika korosho katika mikoa ya kusini.
“Katika ziara yangu nitapenda
kusisitiza haja ya uwekezaji kwenye zao la korosho... nitazungumza na maafisa
wanaohusika ili tuone jinsi ya kulipa msukumo zao hili ambalo lina soko kubwa
sana hapa China,” alisema.
Alimweleza Waziri Mkuu wa China
dhamira ya Serikali ya Tanzania kulipa deni la dola za marekani milioni 24.6
ambalo lilitolowa kama mkopo kwa ajili ya kufufua kiwanda cha nguo cha urafiki.
“Tumeahidi kuanza kulipoa deni hilo
katika mwaka wa fedha 2014/2015. Waziri wa Fedha alishaandika barua kwa
Serikali ya China tangu mwezi Septemba kuonyesha nia ya Serikali ya kulipa deni
hilo,” alisema Waziri Mkuu
Kesho (Ijumaa, Oktoba 18,
2013) Waziri Mkuu atafungua mafunzo ya siku
10 kwa maafisa 20 kutoka idara na taasisi za serikali za hapa nchini
yanayoendeshwa kwa pamoja baina ya Chuo cha Uongozi cha China na Taasisi ya
Uongozi ya Tanzania; atatembelea kiwanda cha Aluminium hapa Beijing, atakutana
Bodi ya Tumbaku, Kampuni za Umeme za China Power Investment (CPI) na State Grid Corporation. Pia
atakutana na kampuni ya mafuta ya CNOOC. Jioni atakutana na Watanzania
waishio Beijing kwenye ubalozi wa Tanznaia nchini China.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, OKTOBA 17, 2013
Post a Comment