SERIKALI
ya Tanzania imeasaini mikataba ya makubaliano (MoUs) mitano ambayo
itasadia kutoa fursa za biashara, mafunzo na masuala ya sayansi na
teknolojia kwa Watanzania.
Mikataba hiyo imetiwa saini leo jioni (Alhamisi, Oktoba 17, 2013) mbele ya Waziri
Mkuu Mizengo Pinda na Waziri Mkuu wa China, Mhe. Li Keqiang mara baada
ya viongozi hao kufanya mazungumzo rasmi ya Kiserikali jijini Beijing,
China.
Mikataba
hiyo ni Mkataba wa Ushirikiano baina ya Tanzania na China kwenye
masuala ya Sayansi na Teknolojia; Mkataba wa Kuruhusu bidhaa za baharini
ziweze kuuzwa China; Mkataba wa Ushirikiano baina ya Tanzania na China
kwenye masuala ya Utalii. Mingine ni Mkataba wa Makubaliano baina ya
Tanzania na China wa kuanzisha Ukanda wa Kisasa wa viwanda vya nguo
pamoja na kukuza zao la pamba na wa mwisho ni mkataba wa kutoa vitalu
namba 60 na 61 kwa ajili ya ujenzi wa ubalozi wa China jijini Dar es
Salaam.
Katika
mazungumzo yao, Waziri Mkuu ambaye yuko katika siku ya pili ya ziara ya
kikazi yake ya siku tisa kwa mwaliko wa Serikali ya nchi hiyo,
alimweleza Waziri Mkuu wa China kwamba anaishukuru Seriklai ya nchi hiyo
kwa misaada mbalimbali ambayo China imekuwa ikiitoa kwa Tanzania.
“Tunaishukuru
kwa misaada mbalimbali na mikopo ambayo imekuwa ikitolewa kwa masharti
nafuu ikilinganishwa na mikopo ya kibiashara ambayo hutolewa na nchi
nyingine na kawaida ina gharama kubwa kwa Taifa,” alisema Waziri Mkuu
wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza
mazungumzo na mwenyeji wake.
Alisema
alitumia fursa hiyo kusisitiza uwekezaji kwenye sekta za kilimo,
nishati, elimu na miundombinu hasa reli, bandari na teknohama. Kwenye
kilimo, Waziri Mkuu alikumbusha suala la upatikanani wa soko kwa zao la
tumbaku lakini akaomba uwepo umuhimu wa pekee kwa wawekezaji wa viwanda
vya kusindika korosho katika mikoa ya kusini.
“Katika
ziara yangu nitapenda kusisitiza haja ya uwekezaji kwenye zao la
korosho… nitazungumza na maafisa wanaohusika ili tuone jinsi ya kulipa
msukumo zao hili ambalo lina soko kubwa sana hapa China,” alisema.
Alimweleza
Waziri Mkuu wa China dhamira ya Serikali ya Tanzania kulipa deni la
dola za marekani milioni 24.6 ambalo lilitolowa kama mkopo kwa ajili ya
kufufua kiwanda cha nguo cha urafiki.
“Tumeahidi
kuanza kulipoa deni hilo katika mwaka wa fedha 2014/2015. Waziri wa
Fedha alishaandika barua kwa Serikali ya China tangu mwezi Septemba
kuonyesha nia ya Serikali ya kulipa deni hilo,” alisema Waziri Mkuu
Kesho (Ijumaa, Oktoba 18, 2013) Waziri Mkuu atafungua
mafunzo ya siku 10 kwa maafisa 20 kutoka idara na taasisi za serikali
za hapa nchini yanayoendeshwa kwa pamoja baina ya Chuo cha Uongozi cha
China na Taasisi ya Uongozi ya Tanzania; atatembelea kiwanda cha
Aluminium hapa Beijing, atakutana Bodi ya Tumbaku, Kampuni za Umeme za China Power Investment (CPI) na State Grid Corporation. Pia atakutana na kampuni ya mafuta ya CNOOC. Jioni atakutana na Watanzania waishio Beijing kwenye ubalozi wa Tanznaia nchini China.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, OKTOBA 17, 2013
Post a Comment