Taaarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu ilisema kuwa Rais Kikwete ameiongezea tume hiyo inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba siku 14, kuanzia Desemba 16 hadi 30, mwaka huu ili kuiwezesha kukamilisha kazi yake.
Tume hiyo ilipaswa kukabidhi Rasimu hiyo Desemba 15, mwaka huu kwa Rais Kikwete baada ya mchakato wa rasimu ya kwanza kukamilika kabla ya kupelekwa katika Bunge Maalumu la Katiba.
Kutokana na Tume kuongezewa muda huo, uwezekano wa kukabidhi Rasimu hiyo siku moja kabla ya mwaka kumalizika unakuwa ni mdogo na kufanya kukabidhi rasimu hiyo mwakani.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Kikwete amefikia uamuzi huo baada ya kupokea maombi ya Tume hiyo kuomba kuongezewa muda zaidi.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa Rais amefikia hatua hiyo kwa mamlaka aliyonayo chini ya Kifungu cha 8(3) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Ilieleza hii ni mara ya pili kwa Rais Kikwete kuiongezea Tume hiyo muda wa kufanya kazi yake, Kufuatia maombi ya kwanza, aliiongezea Tume hiyo muda wa siku 45 kuanzia Novemba Mosi hadi Desemba 15, mwaka huu.
Ilieleza kuwa chini ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Tume hiyo inatakiwa kufanya kazi kwa miezi 18.
Aidha, sheria hiyo inampa Rais mamlaka ya kuiongezea Tume hiyo muda wa kufanya kazi usiozidi siku 60.
Ilifafanua kuwa kwa uamuzi huo wa kuongezewa siku 14, Rais Kikwete atakuwa ameiongezea Tume hiyo muda wa kufanya kazi wa jumla ya siku 59 kati ya 60 ambazo anaruhusiwa kisheria kuiongezea Tume hiyo.
Aprili 6, mwaka jana, Rais Kikwete aliteua wajumbe 34 waliounda Tume ya Mabadiliko ya Katiba mpya ikiongozwa na Jaji mstaafu Warioba.
Julai 2, 2012 Tume hiyo ilianza kukusanya maoni yake kwa wananchi kupitia mikutano ya hadhara katika maeneo mbalimbali ya nchi zoezi lililokamilika Februari 4, mwaka huu.
Juni 3, mwaka huu, Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, alizindua rasimu hiyo katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam akiwa na Wazir Mkuu, Mizengo Pinda.
Mabaraza ya Katiba yalihusisha asasi na taasisi mbalimbali za kijamii, vikiwamo vya siasa, ambayo kwa mujibu wa mwongozo wa Tume, katika mikoa ya Tanzania Bara ukiondoa Dar es Salaam, kila kata iliwakilishwa na wajumbe wanne walioungana na madiwani wa kata na viti maalumu katika Baraza la Katiba la Wilaya.
Kwa upande wa Zanzibar, kulikuwa na mabaraza ya Katiba ya wilaya ngazi ya mamlaka ya serikali za mitaa 13.
Kila shehia visiwani humo iliwakilishwa na wajumbe watatu walioungana na madiwani wa wadi, viti maalumu na wale wa kuteuliwa waliopo kazini kwa sasa.
Baada ya kukabidhi rasimu ya pili kwa Rais, baadaye Bunge Maalumu la Katiba litakutana kuipitisha katiba ambayo baadaye itaamuliwa na wananchi kupitia kura ya maoni
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment