KUSHOTO: Askofu Fransisco Padilla. KULIA: Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi la Olasiti siku lilipopigwa bomu. |
*****
Hatimaye Kanisa la Mtakatifu Joseph
Mfanyakazi la Olasiti jijini hapa lililopigwa bomu Mei 5 mwaka huu na
kuahirishwa uzinduzi wake, limezinduliwa jana na Balozi wa Papa na
Mwakilishi wa Vatican nchini Tanzania, Askofu Fransisco Padilla.
Kabla ya uzinduzi wa kanisa hilo, ibada hiyo ilianza kwa kubariki
makaburi matatu ya Regina Laizer (50), James Kessy (16) na Patricia
Assey (10), ambao wote waliuawa Mei 5 mwaka huu, wakati walipokuwa
kwenye ibada ya uzinduzi wa kanisa hilo, baada ya bomu kurushwa na mtu
asiyejulikana na kusababisha majeruhi zaidi ya 60.
Akizungumza wakati wa mahubiri, Askofu Padilla alisema mara baada ya
tukio hilo alikwenda kwa kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa
Francis anayeongoza Kanisa hilo lenye wafuasi bilioni 1.2, naye
alimwamuru arudi Tanzania mkoani Arusha, ili awape pole waumini wote
waliofikwa na tukio hilo.
"Sasa nawapa pole sana na amenituma nije kupatakasa mahali hapa, pawe
patakatifu kwa ajili ya utoaji wa huduma za Kimungu," alisema Askofu
Padilla.
Askofu Padilla alisema alitumia muda mwingi kuwaasa waumini kuwa na
umoja na mshikamano katika kujenga kanisa, ili kuwe na matunda mazuri
kwa kanisa.
"Nasema hivi sababu nitafurahi kuja kuona watoto wenu wametoka hapa
kuwa watawa, masista na mapadri na wakiongoza ibada hapa, nitafurahi
sana," alisema Askofu Padilla.
Alisema kuwa Kanisa hilo baada ya kuzinduliwa litumike kuwa msingi wa
kusaidia wasio na uwezo na siyo kulitumia jengo hilo kwa njia isiyofaa
wala kuleta matunda kwa kanisa.
Aidha alisema pindi wanapopata majaribu ya shetani, wasikate tamaa,
kwani hawana budi kuimarisha imani zao, kwani shetani hana mamlaka ya
kuangusha nguvu za Mungu kwa sababu anawalinda kila wakati.
Alisisitiza kuwa ni vema kanisa hilo ambalo limekumbwa na tukio la
aina yake, likatumika katika kuibua vipaji vya miito na kuwahubiria
wengine juu ya wokovu ili nao waokoke.
Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Jimbo la Arusha, Josephat Lebulu,
aliyekuwa mwenyeji wa Balozi huyo, alisema ni vema waumini wakajua kuwa
mipango ya Mungu haiwezi kuangamizwa na shetani, hivyo walishindwa
kuzindua kwa wakati ule uliopangwa kwa sababu ya vikwazo vya shetani na
sasa wamemshinda shetani na wamezindua kanisa hilo.
"Mjue wazi mpango wa Mungu hauwezi kuangamizwa na mtu yeyote na ndio
sababu leo tupo hapa tukiweka wakfu katika kanisa letu na kubariki
makaburi ya waumini wetu waliofia imani yao ya Katoliki," alisema Askofu
Lebulu.
Alisema hata katika Biblia inasema wakati ule Mfalme Herode alipanga
kuangamiza watoto wote wa kiume ili amwangamize Yesu, lakini alishindwa
na ndivyo hata leo shetani atajiinua na atashindwa.
Askofu Lebulu alisema watu wote watatu waliofariki kwa kupigwa na
bomu kanisani hapo, walifariki, lakini waliobaki wamepata uponyaji na
nguvu ya maombi zaidi ya hapo mwanzo kabla ya tukio hilo.
Baada ya kueleza maneno hayo aliongozana na Askofu wa Jimbo la
Mahenge, Agapite Ndorobo na Askofu Fransisco Padilla, kwenda kwenye
makaburi yaliyopo mbele ya kanisa hilo na kuyanyunyizia maji ya baraka.
Uzinduzi huo umefanyika ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya
Jubilei ya Jimbo la Arusha, ambayo kilele chake, kinatarajia kufanyika
leo katika Kanisa la Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu na kuhudhuriwa
na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, pamoja na maaskofu na mapadri mbalimbali
kutoka ndani ya mkoa, nje na ughaibuni.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, alisema kwa furaha kubwa
amefarijika sana kumwona Balozi wa Papa akirudi Arusha kukamilisha
kazi aliyoacha kwa sababu ya kukatishwa na mwovu shetani .
"Nakukaribisha sana hapa Olasiti na nakuhakikishia mwovu shetani
ameshindwa kabisa na ametoweka na ameshindwa kabisa na wakati wote wa
misa nilifurahi na kuruka kusikia kuwa hakuna jambo lingine," alisema
Mulongo.
Post a Comment