Na Rahma Suleiman, Zanzibar
WANANCHI
wa Zanzibar wanatarajiwa kunufaika na huduma za uchunguzi na matibabu
ya meno zitakazoendeshwa na taasisi ya Zanzibar Help Foundation kwa
ushirikiano na hoteli ya Doubletree By Hilton ya Dar es Salaam na hoteli
ya Al Beit Al Salaam ya Zanzibar.
Huduma
hizo zinatarajiwa kuwa za siku tatu kuanzia Disemba 5 hadi 7, mwaka huu
zikiendeshwa katika kambi itakayokuwepo katika jengo la ‘Zanzibar Help
Foundation Practice’, Vuga mkabala na tawi la CCM.
Huduma
hizo zitakazoanza saa 2:30 asubuhi, zitaendeshwa na madkatari bungwa
kutoka ‘Zanzibar Help Foundation’ na hospitali ya Aga Khan ya Dar es
Salaam, na zitaolewa bila ya malipo yoyote.
Akizungumza
na waandishi wa habari katika hoteli ya Al Beit Al Salaam, Mratibu wa
kambi hiyo, Ali Jivraji ambaye ni mwanafunzi wa ‘International School of
Tanganyika’ mwenye umri wa miaka 15, amesema kwa kutambua kwamba watu
wengi wanasumbuliwa na meno, ameamua kuendesha kambi hiyo.
Alisema
katika siku ya kwanza, huduma hizo zitatolewa kwa watoto wadogo, na
siku mbili za mwisho zitakuwa kwa watu wazima na vijana.
Alifahamisha
kuwa, lengo la kambi hiyo, ni kuwasaidia watu wenye matatizo ya meno
kupata tiba hasa ikizingatiwa kuwa, gharama za matibabu hayo ni kubwa na
kwamba wananchi wengi hawawezi kuzimudu kutokana na uhaba wa kipato
chao.
“Dhamira
yangu ni kuwafanya watu kufahamu umuhimu wa afya ya meno kwa
kuwakutanisha na madaktari wataalamu watakaowasaidia kuondokana na
matatizo waliyonayo,” alieleza.
“Ili tuishi, tunapaswa kula, na ili tule chakula chenye afya ni muhimu sana tuwe na meno yenye afya pia,” aliongeza Jivraji.
Aliishukuru
Wizara ya Afya Zanzibar na taasisi zote zilizofanikisha kufanyika kwa
kambi hiyo, na kuwahimiza wananchi wenye matatizo ya meno kujitokeza kwa
wingi, akisema hiyo n fursa adhimu ambayo hawapaswi kuikosa.
Naye
Mkurugenzi wa Zanzibar Help Foundation Dk. Feroz Jafferji, alisema
taasisi yake imekuwa ikitoa huduma mbalimbali za kiafya hasa katika
maeneo ya vijijini kwa miaka miwili na nusu sasa.
Alisema
mkakati wa baadae ni kuhakikisha wanafika katika maeneo mengi zaidi
ikiwemo Pemba, pamoja na kupata gari la kutoa huduma za meno (mobile
dental clinic) ili kurahisisha kazi hiyo.
MAELEZO ZANZIBAR
30 NOVEMBA 2013
Post a Comment