Mbunge
wa jimbo la Iringa mjini mchungaji Peter Msigwa akiwa katika Helkopta
ya Dr Slaa kuelekea Mbambabei Songea katika mikutano ya Chadema
Katibu Mkuu wa Chadema, Willibrod Slaa na mwenyekiti wake Freeman Mbowe
wakielekea kuzungumza na waandishi wa habari, Makao Makuu ya chama
hicho Dar es Salaam jana kuhusu kuanza kwa ‘Operesheni Pamoja Daima’ ya
kuzunguka nchi nzima ili kuimarisha chama hicho. Picha na Fidelis
Felix
Na Fidelis Butahe, Mwananchi.............................................................................................................
- Ziara hiyo inaanzia katika mikoa ya
Tanga, Mwanza na Ruvuma, huku viongozi wa chama hicho wakijigawa katika
makundi sita; matatu yakitumia helkopta na matatu yatawafikia wananchi
kwa kutumia usafiri wa magari.
Mwandishi wetu kutoka Dar es Salaam anaripoti kuwa,Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuanzia leo, kinarusha helkopta tatu
kwa siku 14 mfululizo, katika kutekeleza kampeni iliyopewa jina la
Operesheni Pamoja Daima (ODB) itakayoendeshwa katika mikoa yote nchini.
Ziara hiyo inaanzia katika mikoa ya Tanga, Mwanza
na Ruvuma, huku viongozi wa chama hicho wakijigawa katika makundi sita;
matatu yakitumia helkopta na matatu yatawafikia wananchi kwa kutumia
usafiri wa magari.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema jana
jijini Dar es Salaam kuwa, lengo la operesheni hiyo ni kukiimarisha
chama hicho na kuwafumbua macho wananchi kuhusu mchakato wa Katiba Mpya.
“Tumejigawa katika makundi sita na makundi matatu
kati ya hayo yatatumia helikopta kila moja, makundi mengine yatawafikia
wananchi kwa misafara ya ardhini,” alisema Mbowe na kuongeza;
“Viongozi wakuu wa chama, wabunge, wenyeviti wa
mikoa, wilaya, majimbo na kanda kila mmoja atashiriki kwa nafasi yake
katika operesheni hii. Tutafanya mikutano kwa wiki mbili, ila tunaweza
kuongeza wiki nyingine moja.”
Alisema chama hicho kimejipanga kuwafikia wananchi
wengi kadri itakavyowezekana, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi
wake wa ndani kuanzia ngazi ya mashina, uchaguzi mdogo wa madiwani
katika Kata 27 nchini utakaofanyika Februari 9, mwaka huu pamoja na
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
“Naomba tueleweke, katika hili hatufanyi kampeni
hata kidogo, huu ni mwendelezo wa maandalizi ya chaguzi mbalimbali. Kama
mnakumbuka tulianza kujiandaa na uchaguzi wa mwaka 2015 baada ya
kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2010,” alisema Mbowe na kuongeza;
“Kwa sasa tunachokifanya ni kuongeza nguvu na
umakini zaidi. Makundi yataanzia katika mikoa ya Tanga, Mwanza na
Ruvuma, tutapita kila Kata ambazo utafanyika uchaguzi wa madiwani.”
Mbowe alisema operesheni hiyo itapiga kambi katika
Jimbo la Kalenga ambalo kwa sasa lipo wazi baada ya mbunge wake ambaye
pia alikuwa Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk William Mgimwa kufariki dunia
Januari 1, mwaka huu nchini Afrika Kusini.
“Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) haijatangaza
kufanyika uchaguzi katika jimbo hilo, Chadema tutafika Kalenga na
tutafanya mkutano maalumu na kutoa pole kwa wakazi wa jimbo hilo
kutokana na msiba mkubwa wa mbunge wao,” alisema Mbowe.
Operesheni hiyo inafanyika siku chache tangu chama
hicho kikuu cha upinzani nchini kipite katika mgogoro ambao
ulisababisha aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wake, Zitto Kabwe kukimbilia
mahakamani ili kunusuru uanachama wake.
Wakati Zitto akinusurika kufukuzwa kutokana na
zuio la mahakama, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoani Arusha, Samson
Mwigamba na Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo walifukuzwa
uanachama, likiwa ni hitimisho la mchakato ulioanza kwa kuwavua nyadhifa
zao pamoja na Zitto.
Daftari la wapigakura
Mbowe alisema msimamo wa chama chake ni kutaka
daftari la kudumu la wapigakura lifanyiwe marekebisho kabla ya kupigwa
kwa kura za maoni kwa ajili ya kupitisha Katiba Mpya.
“Tutagomea upigaji wa kura na tutawahamasisha
wananchi kugomea kupiga kura. Serikali ya CCM isijidanganye kwa kuweka
mikakati ya kukwamisha zoezi hili,” alisema Mbowe.
Alisema kama Serikali inataka amani iendelee
kuwepo isifanye mzaha katika mchakato wa Katiba Mpya kwa maelezo kuwa
Katiba siyo mali ya vyama vya siasa, bali ni mali ya wananchi.
“Katiba siyo ya Chadema, CUF wala NCCR-Mageuzi.
Sheria inaeleza wazi kwamba daftari la wapigakura ni lazima lifanyiwe
marekebisho mara mbili baada ya Uchaguzi Mkuu na kabla ya kuanza
Uchaguzi Mkuu mwingine lakini hilo halijafanyika mpaka sasa licha ya
Uchaguzi Mkuu kufanyika miaka minne iliyopita,” alisema Mbowe.
Alisema wapo Watanzania waliohama maeneo yao ya
awali, waliopoteza vitambulisho, waliofikisha umri wa kupiga kura na
kusisitiza kuwa kuwaacha watu hao nje ya mfumo wa kupiga kura ni
kuwanyima haki yao ya Kikatiba.
“Kwa mujibu wa utafiti tulioufanya tumebaini kuwa
wapo watu zaidi ya milioni 5 wanaohitaji kuingizwa katika daftari la
wapigakura,” alisema Mbowe na kuongeza;
“Kama Katiba haitapita kwa sababu ya kutokuboreshwa kwa daftari la wapigakura hatutarudi katika Katiba ya sasa hiyo ni ndoto.”
credit: Matukio daima blog
|
Post a Comment