Rais wa Zanzibar Dkt
ALI MOHAMMED SHEIN akikagua gwaride la vikosi vya ulinzi wakati
wa Sherehe za Mapinduzi Matukufu ya
Zanzibar zilizofanyika katika uwanja wa Amaan
********
Leo Januari 12, Wazanzibari wanaadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi.
Mengi yametokea, mengi yametendeka, lakini kubwa zaidi ni kuwa
Wazanzibari wamebaki Wazanzibari.
Huu ni wakati wa kutafakari na kujitathmini. Miaka
50 katika umri wa binadamu si haba, yaliyotokea na kutendeka Zanzibar
kwa kipindi chote hicho pia si madogo.
Atakayesema kuwa hakuna maendeleo yaliyopatikana
katika miaka hiyo, labda hataki kuuona ukweli, lakini kimsingi maendeleo
yapo, tena siyo kidogo. Zanzibar ya mwaka 1964 siyo Zanzibar ya leo
mwaka 2014.
Katika miaka hii 50 kwa kiasi fulani Zanzibar
imepiga hatua, idadi ya shule imeongezeka, idadi ya hospitali na vituo
vya afya vimeongezeka, hata idadi ya majengo bora imeongezeka. Miji
imekua na watu pia wameongezeka, lakini bado hali ya maisha kwa jumla ni
ngumu, ingawa hicho ni kilio cha dunia nzima.
Ila zipo changamoto nyingi ambazo zinapaswa
kufanyiwa kazi, siyo na Serikali pekee, bali hata mtu mmoja mmoja katika
nafasi yake. Kuna tatizo kubwa la ukosefu wa ajira na vijana kutumia
dawa za kulevya.
Pengine vijana wanajiingiza katika vitendo vya
utumiaji wa dawa za kulevya kutokana na shida za maisha au sababu ya
kukosa la kufanya na wa kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili siyo Serikali
pekee bali hata wanajamii.
Kweli huduma za afya zimefika hadi vijijini,
lakini ukweli unabaki palepale kuwa vituo vingi vya afya havina wahudumu
wa kutosha, wala vifaa na dawa. Hili ni tatizo la Serikali. Isijivunie
tu kufungua vituo vya afya hadi vijijini, lakini inapaswa kuhakikisha
huduma za afya zinapatikana kwa uhalisia wake.
Shule nyingi zimefunguliwa kila pembe ya Visiwa
vya Unguja na Pemba; lakini je, elimu inayotolewa inakidhi haja? Vijana
wengi leo wanashindwa kufaulu vyema mitihani yao ya Kidato cha Nne na
cha Sita je, ni kwa sababu gani? Je, mazingira ya kujifunzia
yanaridhisha? Je, wapo walimu wenye taaluma stahiki? Je, vifaa vya
kufundishia vipo? Masuala kama haya ndiyo tunayostahili kujiuliza kabla
ya kujisifu kujenga maelfu ya shule ambazo badala ya kuwa maeneo ya
kujifunzia yanabaki kuwa magofu au maeneo ya kwenda kupotezea muda.
Waasisi wa Taifa letu waliahidi kupambana na
maadui watatu; maradhi, ujinga na umaskini, je, mapambano dhidi ya
maadui hao yamefikia wapi? Isije ikawa tunajidanganya kujenga majengo ya
kutolea elimu na afya, lakini hakuna elimu inayotolewa wala afya
inayopatikana, kwani kudhibiti Malaria pekee haijatosha kusema kuwa
tumeweza kukomesha adui maradhi.
Kuhusu umasikini, bado asilimia kubwa ya
Wazanzibari hasa waishio vijijini wanaishi katika dimbwi la umaskini,
je, kwa miaka 50 ya kujitawala, Serikali imefanya jitihada gani ya
kuwakomboa wananchi hawa kutokana na adui umasikini? Kipato cha
Wanzanzibari walio wengi bado ni chini ya dola moja kwa siku, je, kuna
jitihada gani za kuinua kipato cha mwananchi wa kawaida?
Lakini pamoja na hayo yote, kiwango cha uvumilivu
wa kisiasa Zanzibar kinazidi kuongezeka siku hadi siku. Tunaipongeza
Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), kwa kutuliza mori na jazba za
kisiasa.
Pamoja na yote hayo, tunapenda kuchukua nafasi hii
kuwapongeza Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla kwa kutimiza miaka 50
ya Mapinduzi ya Zanzibar, kazi ya kuyalinda haikuwa ndogo hata kidogo,
tunatarajia kuwa katika mwanzo huu wa karne mpya yatafanyika mapinduzi
zaidi katika sekta za elimu, uchumi na afya ili kupiga hatua zaidi
kimaendeleo.
MWANANCHI
Post a Comment