Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli
********
Viongozi
wa Serikali wakiwamo mawaziri, wameingia kwenye kashfa inayowaweka
katika wakati mgumu, baada ya kubadili matumizi ya nyumba za Serikali
walizonunua, kinyume na mikataba inavyoeleza.
Nyumba
hizo ambazo zilianza kuuzwa mwaka 2002 enzi ya utawala wa Rais wa Awamu
ya Tatu, Benjamin Mkapa ziliuzwa kwa mawaziri, makatibu wakuu na
watumishi wengine wa ngazi mbalimbali za umma.
Mikataba
ya kisheria ya ununuzi wa nyumba za Serikali inaeleza kuwa, mfanyakazi
wa Serikali anaponunua au kukopeshwa nyumba, hatakiwi kubadili matumizi
au kuuza hadi baada ya miaka 25 kupita.
Kwa
mujibu wa mkataba wa mauziano kifungu Na 9 na 10, mtumishi aliyeuziwa
nyumba au mrithi wake haruhusiwi kuiuza nyumba hiyo mpaka hapo
itakapotimia miaka ishirini na mitano (25), kuanzia tarehe ya
hatimiliki.
Gazeti
hili lilimtafuta Waziri wa Ujenzi, John Magufuli mwenye dhamana na
nyumba za Serikali kwa muda wa miezi miwili kutoa ufafanuzi wa suala
hilo bila mafanikio, huku akitoa sababu mbalimbali kwa mwandishi kukwepa
kuzungumzia suala hilo.
Hata
hivyo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Injinia Gerson Lwenge alisema kuwa
anahitaji kupata ripoti kamili kutoka kwa Wakala wa Nyumba za Serikali
(TBA), ili ajionee mikataba na afahamu ni wapi ilipovunjwa.
“Serikali
ina nia nzuri kabisa kuwauzia watumishi wake nyumba, lakini kama kuna
mikataba inakiukwa, basi TBA inafahamu kwa kina ni kwa vipi watu hao
wachukuliwe hatua,” alisema.
Uchunguzi
wa gazeti hili umebaini kuwa, viongozi wengi ambao nyumba zao zipo
katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na Mwanza wamezibadili matumizi na
kuwa za biashara.
Kwa Jiji
la Dar es Salaam baadhi ya nyumba zilizouzwa kwa vigogo hao wa Serikali
na kubadilishwa matumizi zipo katika maeneo ya Oysterbay.
Gazeti
hili lilishuhudia baadhi ya nyumba hizo zikiwa zimebadilishwa matumizi
na kuwa klabu za starehe, kupangishwa taasisi au balozi, huku nyingine
zikiwa tayari zimeuzwa.
Moja ya
nyumba hizo ni ya aliyewahi kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
anayeshughulikia Muungano, Mohamed Seif Khatib, iliyopo Oysterbay, Mtaa
wa Bongoyo katika Barabara ya Hillpark. Nyumba hiyo kwa sasa imevunjwa
na kujengwa klabu na baa iitwayo Ocasa.
Alipoulizwa
kuhusu nyumba hiyo na mkataba wake unavyosema, Khatib alisema kwamba
hajavunja sheria yoyote kwa sababu hajauza nyumba hiyo.
Alifafanua
kuwa yeye amebadili matumizi sehemu ndogo ya nyumba hiyo huku akimtaka
mwandishi aandike tu kuhusu sehemu kubwa na siyo mabadiliko aliyodai ni
madogo.
“Nyie
waandishi ndivyo mlivyo, kwa nini msiandike mazuri yetu. Mnapenda
kuandika mambo mabaya tu, mnataka tuishi kimaskini. Nyumba imejengwa
tangu enzi za ukoloni, mnataka mpaka leo ibaki hivyohivyo?” alihoji.
Eneo la
Kinondoni, palipokuwa na nyumba ya aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Afya
katika Serikali ya Rais Kikwete, nayo kwa sasa imevunjwa na kujengwa
ghorofa, huku kibao cha mkandarasi kikionyesha kuwa ujenzi wa jengo la
biashara unaendelea.
Hata
hivyo, uchunguzi wa gazeti hili umeonyesha kuwa nyumba nyingine za
viongozi wa Serikali zilizobadilishwa matumizi zipo eneo la Msasani na
Masaki.
Nyumba
nyingine iliyobadilishwa matumizi inamilikiwa na waziri mmoja eneo la
Barabara ya Hindu, Kinondoni mkabala na Barabara ya Ali Hassan Mwinyi,
ambayo imebadilishwa na kujengwa nyumba za kupangisha watu.
Mjini Arusha baadhi ya nyumba za Serikali zilizouzwa na kubadilishwa matumizi zipo eneo la Uzunguni.
Moja ya
nyumba hizo ipo karibu na Ikulu ndogo mjini humo, ambayo hivi sasa
imebadilishwa na kuwa baa. Nyumba hiyo ipo Mtaa wa Haile Selassie.
Katika Jiji la Mwanza, nyumba zilizobadilishwa matumizi zipo katika eneo la Isamilo na Kapiripointi.
Historia ya nyumba za Serikali
Nyumba za
watumishi wa Serikali zilianza kujengwa na watawala wa Kijerumani na
Waingereza. Nyumba hizo ambazo sasa idadi yake inakadiriwa kufikia
10,000 ni za daraja la tatu, pili na la kwanza, kulingana na nyadhifa za
watumishi wa Serikali.
Sababu za
kuuza nyumba hizo hazikuwekwa bayana, lakini maelezo mengine
yanaonyesha kuwa hatua hiyo imefikiwa ili kuwasaidia watumishi wa
Serikali kuwa na nyumba. Hata hivyo, maelezo mengine yanaonyesha kwamba
nyumba hizo ziliuzwa kwa kuwa ni mzigo kwa Serikali.
Hadi kufikia mwaka 2012, nyumba za Serikali zilizouzwa kwa watumishi wa umma ni 6,000.
Wakala wa Majengo
Mkurugenzi
wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Elius Mwakalinga alisema kuwa kuna
masharti ya nyumba za Serikali ambayo miongoni mwake ni kutobadili
matumizi na kutohamisha mali hiyo hadi baada ya miaka 25.
Mwakalinga
alisema pia kwamba mfanyakazi wa umma hatatakiwa kuhamisha mali hiyo
wala hatimiliki kwa mtu wa tatu na iwapo atahitaji kufanya ukarabati,
basi atatakiwa kuomba kibali.
“Kama
kweli kuna watu wanaofanya ujanja katika hilo, hata kama ni viongozi,
watashughulikiwa kulingana na sheria,” alisema Mwakalinga.
Waziri Lwenge
Akizungumzia
zaidi suala hilo, Naibu Waziri Lwenge alihoji maswali kadhaa, ikiwamo
sababu za watumishi kubadili nyumba hizo na kuzifanya klabu au maeneo ya
biashara na wakapewa ruhusa na mamlaka ya mipango miji. Hata hivyo,
alisisitiza kuwa hajaifahamu kwa kina mikataba hiyo inasema nini.
Lwenge
alisema kwamba wizara yake itaketi na wanasheria wake na kuangalia upya
mikataba hiyo, ili iwapo kuna vipengele vyenye upungufu virekebishwe.
“Inawezekana
kuna vitu vinakosekana kwenye mikataba hiyo, au havijafafanuliwa na
ndiyo maana watumishi wa Serikali wanavitumia vibaya kuvunja masharti ya
mikataba yenyewe,” alisema.
Lwenge pia alisema kwamba kuna mambo mengi kwenye mikataba hiyo anayodhani yanatatiza na kuhitaji kutupiwa jicho.
Alitaja mfano wa mtumishi aliyestaafu na kuiachia nyumba hiyo familia yake, ambayo haifahamu masharti ya mikataba.
“Nia yetu
ni kusaidia wafanyakazi. Ni hilo tu, hatuna jingine, lakini kama kuna
upungufu kama huo ni lazima uangaliwe. Ila nashukuru kwa kuwa waandishi
mnafanya kazi ya kubaini vitu kama hivi,” alisema.
Manispaa Kinondoni
Msemaji
wa Manispaa ya Kinondoni, Sebastian Kaiohela alisema kuwa TBA wana kazi
yao na nyumba zao na wanaifahamu mikataba ya wateja wao.
“Sina
uhakika kama TBA ina nyumba maeneo ya Oysterbay, ila kwa upande wa
nyumba za Serikali zinazosimamiwa na manispaa, tuna orodha ya mikataba
na waliobadili matumizi,” alisema.
Ushawishi kutoka kwa wawekezaji
Uchunguzi
wa gazeti hili ulibaini kuwa baadhi ya viongozi na watumishi wengine wa
Serikali wamepangisha nyumba hizo kwa kampuni binafsi, baadhi kujenga
maduka ya biashara na ofisi nje ya uzio wa nyumba hizo.
Ilibainika
kuwa, viongozi wengi wanaomiliki nyumba hizo huingiwa tamaa ya kuziuza
au kubadili matumizi kwa sababu ya ushawishi wa wawekezaji wa nje, ambao
huahidi kuwalipa kiasi kikubwa cha fedha na kuzirudisha nyumba hizo
baada ya miaka 20.
Septemba
mwaka jana, nyumba ya Serikali iliyoko eneo la Mafiati, mjini Mbeya,
yenye namba 162, Block ilipigwa mnada na Kampuni ya Udalali ya J.A
Kandonga.
Nyumba
hiyo inadaiwa kuuzwa kwa mfanyabiashara wa jijini Dar es Salaam kwa
Sh250 milioni kutoka kwa mfanyakazi wa Serikali, Simboleo Gibson.
Mohamed Seif Khatib
Akizungumzia
zaidi kuhusu nyumba aliyoinunua serikalini Khatibu ambaye pia ni Katibu
wa NEC Oganaizesheni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), alisema kwamba
sehemu kubwa ya nyumba yake ameibadilisha kuwa nyumba ya kuishi na kuwa
ghorofa yenye vyumba kadhaa ili iwe katika hadhi nzuri, huku pia akikiri
mabadiliko katika eneo ilipo baa ya Osaka.
“Sehemu
kubwa nimebadilisha kuwa makazi ya kuishi vilevile sasa kwa nini nyinyi
mnataka kukuza hili jambo katika sehemu ndogo tu? Haya andika utakavyo,
andika nimebadili matumizi kama unavyotaka,” alifoka Khatib.
Rais Kikwete
Rais Jakaya
Kikwete, aliwahi kusema kuwa Serikali yake imefikia uamuzi wa
kuzirejesha baadhi ya nyumba za Serikali zilizouzwa kwa watumishi wa
umma, baada ya kubaini kwamba zilijengwa katika mazingira nyeti.
Kikwete
aliyasema hayo Ikulu Dar es Salaam alipokuwa akijibu maswali ya wahariri
wakuu wa vyombo mbalimbali vya habari aliokutana nao chini ya kivuli
cha utaratibu aliojipangia wa kuzungumza na wananchi kila mwishoni mwa
mwezi.
“Hatukusudii
kuzichukua nyumba zote…kwa mfano kuna OCD kauziwa nyumba ya OCD iliyo
katika eneo la polisi, na yule OCD aliyeuziwa kahamishwa kutoka Mtwara
kwenda Mafia…au kastaafu na nyumba kapangisha…Kwa kweli kuna maeneo
ambayo lazima tufanye marekebisho,” alisema Kikwete.
Post a Comment