Maandalizi
ya mbio za 12 za Kilimanjaro Marathon zinazotarajiwa kufanyika Machi 2,
2014 huko Moshi yanaendelea kushika kasi baada ya waandaaji wa mbio hizo kutangaza ada za ushiriki pamoja na ratiba ya mbio hizo.
John
Addison, Mkurugenzi Mkuu wa Wild Frontiers, waandaaji wa mbio hizo
alisema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana kwamba mbio ndefu
za 42km Kilimanjaro Premium Lager Marathon zitaanza saa 12:30 asubuhi
huku mbio za 10km Gapco Disabled Marathon zikianza saa 12:45 asubuhi,
Nusu Marathon km 21 saa 1 kamili asubuhi na mbio za kujifurahisha za
Vodacom 5km Fun Run zitaanza saa moja na robo asubuhi. Alisema ratiba
hii imepangwa kwa mtiririko huu ili kuwapa fursa washiriki wa kila mbio
kuona mandhari ya mji wa Moshi na Mlima Kilimanjaro.
Alisema kuwa
viingilio vya mbio ndefu za Full Marathon km 42 viingilio itakuwa ni
dola 60 kwa washiriki wa kimataifa, Tsh 6,000 kwa raia wa Afrika
Mashariki na dola 30 kwa raia wa kigeni wanaoishi au kufanya kazi Afrika
Mashariki wakati huku Nusu Marathon viingilio ikiwa ni dola 60 kwa
washiriki wa kimataifa, shilingi 4,000 kwa raia wa Afrika Mashariki na
dola 30 raia wa kigeni wanaoishi Afrika Mashariki
Aidha,
washiriki wa kimataifa kwenye mbio za walemavu za GAPCO watalipia dola
10, shilingi 3,000 kwa raia wa Afrika Mashariki na dola tano kwa raia wa
kigeni wanaoishi Afrika Mashariki. Mbio hizo za walemavu zitahusisha
shindano la mbio za kutumia baiskeli za mikono (Handcycle) na viti
vyenye magurudumu (Wheelchair) tu. Washiriki wa kimataifa na raia wa
kigeni waishio Afrika Mashariki watalipa dola mbili na raia wa Afrika
Mashariki watalipa shilingi 3,000 mbio za kujifurahisha za Vodacom 5km
Fun Run.
Kwa mujibu
wa Addison, umri wa kushiriki mbio za kilomita 42 ni miaka 21, miaka 18
kwa nusu marathon na mbio za walemavu huku kwenye mbio za kujifurahisha
ikiwa ni miaka kumi. “Tutasajili washiriki kwa muda wa siku mbili kabla
ya mbio ambapo kwenye hoteli ya Keys Hotel mjini Moshi tarehe 28
Februari na tarehe 1 Machi kuanzia saa 4 asubuhi mpaka saa 11 jioni kila
siku na pia uandikishwaji utafanyika Arusha tarehe 27 Februari katika
eneo ambalo litatangazwa badae,” alisema.
Mbio hizo
zinadhaniwa kuwa kati ya mbio kubwa zaidi duniani za kitalii na ndio
tukio kubwa zaidi la kimichezo Tanzania. Kilimanjaro Marathon ya mwaka
huu inatarajiwa kuwa na washiriki zaidi ya 6,000 wakiwemo takribani
wageni 600 kutoka nchi zaidi ya 40.
Kilimanjaro
Marathon 2014 inadhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager (wadhamini
wakuu), Vodacom Tanzania (5km Fun Run), GAPCO (10km Disabled Run), FNB
Tanzania, TPC Sugar, Simba Cement, KK Security, Kilimanjaro Water, Keys
Hotel, TanzaniteOne na UNFPA.
Post a Comment