Mwaka 2014 Uwe Ni Wa Kusonga Mbele…
Ndugu zangu,
Tumeingia
Mwaka Mpya wa 2014. Kwangu binafsi mwaka 2013 umekuwa wa bahati mbaya
ya kukumbwa na balaa lililonirudisha nyuma kwa takribani miezi minne.
Tukio
la mwezi Machi mwaka jana, la kushambuliwa na kuteswa kwa ndugu yangu
na mwanafamilia mwenzangu kwenye tasnia ya habari, Absalom Kibanda, sio
tu lilinigusa na kunitia hofu, bali, kukatokea pia ‘ kituko’ cha mwaka
cha mimi kuhusishwa na uovu ule.
Nilifahamu
kuwa nchi yetu ina mambo mengine ya ovyo ovyo, lakini, kamwe sikufikiri
ningeingizwa kwenye mambo ya ovyo ovyo ya staili iliyonitokea mimi.
Hakika,
jambo lile halikunifedhehesha mimi tu, bali, umati wa watu
walionifahamu kwa miaka mingi kupitia kalamu yangu nao walifedheheshwa
pia. Waliponipigia simu kunipa pole ajabu mimi niliyejibu nilijikuta
nikiwapa pole wao. Kwangu inabaki kuwa ni moja ya ‘ Kumbumbu ya aibu’-
Memories of shame.
Nami,
kama ilivyo kwa wengine, nina kiu ya kuujua ukweli wa kilichomtokea
Kibanda. Hatuwezi kulala kwa amani bila kujua haswa ni akina nani
waliomfanyia unyama ule Absalom Kibanda.
Kwa
wale ndugu zangu waliohusika kwa namna moja au nyingine kwenye kazi ile
ya kunifedhehesha na kunidhalilisha kwa lengo moja kuu la KUNICHAFUA
mbele ya macho ya jamii. Ndugu zangu ambao wengine ni rafiki zangu na
wanafamilia wenzangu kwenye tasnia ya habari na wenye kujiita wanasiasa
wapenda demokrasia, ningependa niwahakikishie, kuwa mimi kama Maggid,
nawahesabu bado ni ndugu na rafiki zangu. Sina kinyongo nao. Nitapenda
kuendelea na udugu na ushirikiano wetu kama Watanzania, na wao wala
wasisite kunishirikisha kwenye mambo ya msingi kwa ajili ya nchi yetu.
Ndugu zangu,
Kwangu
mwaka 2014 nadhamiria uwe ni wa kusonga mbele. Na ningependa sote tuwe
na dhamira hiyo ya kusonga mbele kama watu binafsi na kama taifa.
Tutangulize zaidi maslahi mapana ya nchi yetu.
Kwa
misukosuko niliyopata mwaka huu, kuna ambayo nimeshindwa kuyafanya kama
nilivyodhamiria na kuweka bayana kwenye ‘hotuba’ yangu ya mwisho wa
mwaka jana.
Mwaka
2014, mbali ya kazi zangu za kila siku kwenye Jumuiya ya Karibu
Tanzania Association, nitapenda nitimize dhamira yangu ya kuupanda Mlima
Kilimanjaro. Nitapenda pia nijikite kwenye kuhamasisha juhudi za
maendeleo kwa Wanawake na Vijana wa Vijijini. Nitapenda pia niimarishe
Jukwaa la ‘ Kwanza Jamii Dialogue’ kwa maana ya mijadala ya wazi
kuhusiana na masuala muhimu ya kitaifa.
Naam, nitapenda kujikita kwenye yale yenye pia kuibua mijadala endelevu kwa maendeleo ya nchi yetu.
Pamoja
na yote hayo, mwaka 2014 nitajitahidi, kama mzazi, kutenga muda zaidi
wa kuwa na familia yangu; mke wangu mpenzi na wana wangu.
Nawatakia nyote HERI YA MWAKA MPYA!
Maggid Mjengwa,
Iringa.
0754 678 252
Post a Comment